• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 7:55 PM
Wanne washtakiwa kwa kumjeruhi Profesa akiombea ploti yake

Wanne washtakiwa kwa kumjeruhi Profesa akiombea ploti yake

NA TITUS OMINDE

WASHUKIWA wanne, wanaume watatu na mwanamke mmoja, wameshtakiwa kwa kushambulia Profesa nguli wa Hisabati wakati alipokuwa akifanya maombi kutakasa kiwanja chake kipya.

Washukiwa hao ambao miongioni mwao ni daktari na mfanyakazi wa Kenya Ordinance Factory (KOF), mahakama ya Eldoret imeambiwa kwamba walimvamia profesa, ambaye pia ni mchungaji kwa kuwa kero kwa maombi ya kelele usiku.

Washtakiwa walikuwa wakitoa ushahidi Jumanne katika mahakama ya Eldoret katika kesi ambapo wameshtakiwa kwa pamoja kwa shambulio lililomsababisha mlalamishi madhara ya mwili kinyume na kifungu cha 251 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu.

Kulingana na shtaka, Dkt Geoffrey Masika Wechuli anayefanya kazi katika Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Kapsabet, James Nyamweya Mwamba ambaye ni mfanyakazi wa Kiwanda cha kutengeneza silaha cha KOF, Maurice Obiero na Ednah Saeyi Khaemba, pamoja na wengine ambao hawakuwa mahakamani, walimshambulia kinyume cha sheria Profesa Wilfred Sawanda.

Mwendeshaji wa mashtaka aliambia mahakama kuwa kisa hicho kilitokea usiku wa Novemba 9, 2014, katika mtaa wa Racecourse katika kaunti ndogo ya Kapseret.

Washtakiwa walikana shtaka hilo na wameachiliwa kwa dhamana.

Ingawa hivyo, Dkt Masika alikiri mahakamani kuwa mlalamishi alivamiwa na majirani wenye hasira ambao walikerwa na maombi ya kelele na maneno yaliyodhaniwa kuwa mazingaombwe kutoka kwa mlalamishi na washirika wake.

“Kama majirani tulikerwa na kelele za ajabu zilizokuwa zikitokea kwenye boma la profesa huyo na tulitoka nje ili kujua kilichokuwa kikiendelea na ndipo baadhi ya majirani wenye hasira walidaiwa kumvamia na kumjeruhi,” Dkt Wechuli aliiambia mahakama.

Hata hivyo, Dkt Wechule alijitenga na majirani waliodaiwa kumshambulia profesa.

Dkt Khaemba ambaye alikiri kwamba Profesa Sawanda alishambuliwa, aliambia mahakama kuwa hakumshambulia profesa huyo kutokana na kiapo chake cha cha udaktari.

Hata hivyo alikubaliana na ripoti ya matibabu iliyowasilishwa mahakamani ikionyesha kuwa profesa huyo alijeruhiwa.

“Ninakubaliana na ripoti ya matibabu iliyowasilishwa katika mahakama hii na daktari mwenzangu kutoka Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Moi. Hata hivyo, sikuwa miongoni mwa watu waliomvamia mlalamishi nikikumbuka kwamba nilikula kiapo cha kulinda maisha,” daktari huyo aliambia mahakama.

Daktari huyo aliambia mahakama kuwa wakati wa kisa hicho cha usiku wa manane, majirani walipata mishumaa iliyowashwa katika boma hilo kando ya ua na kuwafanya watilie shaka kilichokuwa kikiendelea katika boma husika.

Naye Nyamweya alikanusha vikali kumshambulia jirani yake ingawa alikiri kuwa aliamshwa na majirani wengine kutokana na maombi hayo ambayo yalidhaniwa kuwa uchawi.

Licha ya ushahidi husika, Profesa Sawanda ametilia mkazo kwamba maombi hayo yalikuwa ya kutakasa boma lake.

Hakimu mwandamizi Mogire Onkoba aliahirisha kusikilizwa kwa kesi hiyo hadi Januari 24, 2024.

  • Tags

You can share this post!

SHINA LA UHAI: Hofu maambukizi ya TB yakiongezeka miongoni...

Kindiki afanya mkutano muhimu Lamu kukoleza vita dhidi ya...

T L