• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
SHINA LA UHAI: Hofu maambukizi ya TB yakiongezeka miongoni mwa wanaume

SHINA LA UHAI: Hofu maambukizi ya TB yakiongezeka miongoni mwa wanaume

NA PAULINE ONGAJI

MNAMO Agosti 29, 2023, Bw Alex Kinyanjui,19, mkazi wa eneo la Kaloleni, Voi, Kaunti ya Taita Taveta, aligundulika kuugua maradhi ya kifua kikuu (TB).

Kulingana na Bw Kinyanjui, kwa muda alishuhudia dalili kadhaa.

“Nilikuwa nakohoa, kuhisi baridi sana hasa wakati wa asubuhi, na nilikuwa natokwa na jasho jingi usiku,” aeleza.

Lakini ilimchukua muda kabla ya kukubali kwenda hospitalini na kufanyiwa uchunguzi kubaini iwapo kwa kweli alikuwa anaugua.

“Mara ya kwanza nilidhani ni mafua tu ya kawaida nikawa najiambia yataisha, na hivyo nilipuuza kwenda hospitalini. Badala yake, nilikuwa nanunua dawa za kukabiliana na makali ya dalili nilizokuwa nashuhudia.”

Matibabu

Lakini muda ulivyokuwa unasonga, ndivyo dalili zilivyozidi kuongezeka. Wakati huu alijaribu kupokea matibabu katika hospitali kadhaa ambapo hakufanikia.

“Nilienda hospitalini kwa mara ya kwanza Julai 27, 2023, lakini nikaambiwa kuwa nilikuwa na minyoo. Wakati mwingine nikaenda katika kituo kingine cha afya na kuambiwa kuwa nilikuwa na maradhi ya mkamba (bronchitis), lakini hata baada ya matibabu, sikupata nafuu.”

Wakati huu afya yake ilikuwa imedorora zaidi na mwili wake kuwa dhaifu sana.

“Nilikuwa dhaifu sana ndiposa nikaenda hosipitalini nikapimwa, nikapigwa picha za eksirei na kupatikana na TB, ambapo Agosti 29 nilianza rasmi matibabu ya miezi sita,” anaeleza.

Bw Kinyanjui anawakilisha idadi kubwa ya wanaume wanaougua TB hapa nchini.

Bw Alex Kinyanjui wakati wa mahojiano na Taifa Leo mjini Voi, Kaunti ya Taita Taveta. PICHA | LUCY MKANYIKA

Huku Kenya ikiendelea kukumbwa na uhaba wa dawa za kutibu TB, takwimu zinaonyesha kwamba visa vya maradhi haya miongoni mwa wanaume vilikaribia mara mbili zaidi ya vile vilivyoripotiwa miongoni mwa wanawake.

Idadi ya wanaume waliogundulika kuwa na TB ilikuwa asilimia 56.5 ikilinganishwa na wanawake ambayo ilikuwa asilimia 32.5 na asilimia 11 miongoni mwa watoto.

Ongezeko

Kulingana na Bw Peter Ng’ola, mwanachama wa bodi ya Shirika la Stop TB Partnership, kuna masuala tofauti ambayo yamechangia ongezeko hili miongoni mwa wanaume.

“Mojawapo ya vichocheo hivi ni mtindo wa maisha ambapo wanaume wengi huvuta sigara, na pia kwa kawaida hujipata kwenye hatari ya kuwa wazi kwa kemikali katika maeneo ya kazi, kama vile mazingira ya uchimbaji migodi,” aeleza.

Aidha, kulingana na Bw Ng’ola wanaume hawazingatii lishe bora na pia kwa kawaida hawatafuti huduma za afya mapema wanapougua.

Isitoshe, wataalam wanasisitiza kwamba takwimu hizi hazitokani tu na utambuzi duni wa maradhi haya miongoni mwa wanaume ikilinganishwa na wanawake.

“Sababu kuu ni kwamba dalili za TB hazijitokezi mapema kwa wanaume, suala linalochelewesha utambuzi,” aeleza Bw Ng’ola.

Lakini zaidi ya yote, utafiti unaonyesha kwamba wanaume hawapokei au wanachelewa kwenda hospitalini kupimwa na kupokea matibabu dhidi ya maradhi haya.

Ushahidi unaonyesha kwamba masuala kama vile kupoteza mapato na vizingiti vya kifedha, vile vile unyanyapaa, huathiri uamuzi wa wanaume kutafuta huduma za afya.

Uamuzi wa kutafuta huduma za afya aidha zinaathiriwa pia na tahasuba ya kiume zinazowazuia wanaume kutokubali kwamba wanaugua na hivyo wanahitaji matibabu.

“Pia, huenda mifumo ya huduma za afya iliyopo inawafanya wanaume wahisi kana kwamba wanapoteza uwezo wao kuwa usukani,” aeleza Bw Ng’ola.

Hii ni hatari sio tu kwao, bali kwa jamii yote kwa jumla.

“Wanaume husambaza maradhi haya kwa jamii kwa muda mrefu ikilinganishwa na wanawake. Aidha, kutokana na kwamba wanaume hutangamana na wenzao kwa wingi, hii inaongeza hatari ya wao kusambaza maradhi haya,” aeleza Bw Ng’ola.

Haya yakijiri, TB inaendelea kuwa mzigo mkubwa kwa mfumo wa afya nchini.

Maradhi haya yanasalia kuwa tishio kwani yako kileleni kwenye orodha ya magonjwa yanayosababisha vifo vingi nchini Kenya.

Mwaka wa 2020, visa vya maradhi haya vilikadiriwa kuwa 140,000 huku idadi ya wanaougua TB sugu ikifikia 2,500. Aidha, watu 33,000 walifariki kutokana na ugonjwa huu.

Ili kukabiliana na mzigo unaotokana na maradhi haya, wataalam wanasema kwamba ili ndoto ya kuangamiza maradhi ya TB itimizwe basi sharti harakati za utambuzi wa maradhi haya miongoni mwa wanaume ziimarishwe.

“Aidha, tunapoangazia suala la jinsia katika matibabu ya TB, hata tunapowapa wasichana na wanawake kipaumbele, hatuapswi kupuuza mahitaji ya wavulana na wanaume,” aeleza Bw Ng’ola.

Kulingana na mtaalam huyu, kuangazia mzigo unaowakumba wanaume katika matibabu ya TB sio tu suala la afya ya wanaume, bali linaathiri jamii yote kwa ujumla.

“Jitihada na sera za kitaifa na kimataifa za kukabiliana na maradhi ya TB sharti ziangazie wanaume pia.”

Mkakati wa Shirika la Afya Duniani WHO wa kukabiliana na TB unasisitiza usawa katika kufikia huduma za utambuzi na matibabu ya maradhi haya.

Hapa nchini, mkakati wa kitaifa wa mwaka 2019-2023 umewatambua wanaume kama kikundi kilicho hatarini hasa unapozungumzia masuala ya TB.

Wataalam wanasisitiza kwamba umewadia wakati wa mfumo wetu wa afya kutambua mahitaji ya wanaume.

“Tunapaswa kuanza kufikiria jinsi ya kutenga huduma maalum za kliniki zinazowalenga wanaume.”

  • Tags

You can share this post!

Mkahawa wapokeza wateja mafunzo ya bure kuhusu uhifadhi wa...

Wanne washtakiwa kwa kumjeruhi Profesa akiombea ploti yake

T L