• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 4:42 PM
Wauzaji pombe ‘mwitu’ kuona cha mtema kuni

Wauzaji pombe ‘mwitu’ kuona cha mtema kuni

NA CHARLES WASONGA

MISAKO dhidi ya watu wanaokiuka sheria ya Udhibiti wa Matumizi ya Pombe (ADCA) ya 2010 sasa itaendeshwa na maafisa spesheli wenye kibali maalum.

Hii ni baada ya Waziri wa Usalama wa Ndani, Kithure Kindiki kutoa nguvu ya kisheria kwa Mamlaka ya Kitaifa ya Kupambana na Matumizi ya Pombe na Mihadarati (NACADA) kutekeleza sheria hiyo kwa kuhalalisha majukumu ya maafisa hao kupitia tangazo kwenye gazeti rasmi la serikali.

Katika tangazo hilo kwenye toleo la Ijumaa, Desemba 1, 2023 la gazeti hilo, Prof Kindiki ameorodhesha majina ya maafisa hao watakaoendesha operesheni dhidi ya wavunjaji sheria ya pombe kote nchini.

Kwa misingi hiyo, na kulingana na sehemu ya 51 ya sheria hiyo ya ADCA, maafisa wa NACADA wenye kibali maalum, wakati wowote, wanaweza kuingia mahala popote, watakapoamini kuwa mtu au watu wanavunja sehemu fulani za sheria hiyo.

Lakini sharti wapate kibali kutoka kwa mwenye nyumba au mahala pa biashara au waranti iliyotolewa na hakimu au Jaji wa Mahakama Kuu, kabla ya kuendesha ukaguzi.

Aidha, sheria inafafanua kuwa, saa za utekelezaji wa msako huo itakuwa kuanzia saa kumi na mbili asubuhi hadi saa kumi na mbili jioni katika, siku yoyote ya wiki.

Maafisa wa NACADA watakaotekeleza msako huo hawataruhusiwa kutumia nguvu isipokuwa ikiwa wameandamana na afisa wa polisi.

Awali, maafisa wa mamlaka hiyo walikuwa wakitegemea polisi kuisaidia katika utekelezaji wa sheria zake.

Afisa Mkuu Mtendaji wa NACADA Anthony Omerikwa amepongeza hatua hiyo ya Waziri Kindiki akisema inatoa nafasi kwa asasi hiyo kutekeleza majukumu yake kwa misingi ya sheria.

Aliongeza kuwa hatua hiyo imejiri wakati mwafaka, msimu wa sherehe unapokaribia na ambapo visa vingi vya ukiukaji wa sheria za kudhibiti pombe hushuhudiwa.

 

  • Tags

You can share this post!

Niliyoyachukulia ni mambo madogo tu yamenivunia heshima...

Serikali kutambua rasmi vazi la uponyaji la Mijikenda...

T L