• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 6:55 PM
Bobi Wine na Besigye washutumu Jenerali Muhoozi Kainerugaba

Bobi Wine na Besigye washutumu Jenerali Muhoozi Kainerugaba

NA CHARLES WASONGA

VIONGOZI wa upinzani nchini Uganda wamemsuta mwanawe rais wa nchi hiyo, Yoweri Museveni, Muhoozi Kainerugaba, kufuatia madai yake kwamba anaweza kuteka Nairobi ndani ya wiki mbili.

Waliokuwa wagombea urais, Robert Kyagulanyi, almaarufu Bobi Wine na Kizza Besigye wamesema kauli hiyo ni mbaya na inaweza kuvuruga uhusiano wa kidiplomasia kati Kenya na Uganda.

Aidha, Bobi Wine alisema kauli ya Muhoozi, ambaye ni kamanda wa jeshi la nchi kavu nchini Uganda, inaakisi hali mbaya ambayo raia wa Uganda wamepitia chini ya uongozi wake jeshini.

“Wapendwa Wakenya, sasa mwaelewa hali ngumu ambayo tumeishi chini ya utawala wa Museveni na mwanawe, ambaye alimtunuku kwa cheo kikuu jeshini na kumtwika wajibu wa kusimamia majeshi ya ardhini. Ndani ya ujumbe huo wa Twitter kunaonekana zimwi ambaye hufurahia anapowatesa wananchi!” Bobi Wine akasema kupitia ujumbe wa Twitter.

Tayari Museveni amemwondoa kuliongoza jeshi la ardhini lakini akampandisha cheo kutoka Luteni Jenerali hadi Jenerali.

Kwa upande wake, Bw Besigye, ambaye zamani alikuwa afisa katika Jeshi la Uganda (PDF) alidai kuwa kauli ya Muhoozi iko na hatari ya kuwakumbusha raia kuhusu uhusiano mbaya kati ya aliyekuwa Rais wa Kenya Jomo Kenyatta na aliyekuwa Rais wa Uganda Idi Amin.

“Rais Jomo Kenyatta na makamu wake wa Rais Arap Moi walifanya kazi kwa bidii kusaka suluhu kuhusu vitisho kutoka kwa Idi Amin. Jenerali Amin, kama Jenerali Museveni, alikuwa akiwapa silaha wanajeshi wake,” akaandika Besigye, kupitia ukurasa wake wa Twitter.

  • Tags

You can share this post!

Ruto apunguzia Jumwa madaraka

Wetang’ula kufanya uamuzi mkubwa

T L