• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 6:07 PM
Covid: Uganda kuanza kuunda chanjo yake – Rais Museveni

Covid: Uganda kuanza kuunda chanjo yake – Rais Museveni

Na DAILY MONITOR

RAIS Yoweri Museveni amesema Uganda itaanza kutengeneza chanjo yake ya corona, baada yake kufunga kabisa taifa hilo la Afrika Mashariki kutokana na ongezeko la maambukizi ya virusi hivyo.

Museveni alisema mipango ya kutengeneza chanjo hiyo iko karibu kukamilika.

Hospitali nchini humo zimejaa huku madaktari wakisema wamelemewa na idadi kubwa ya wagonjwa wa Covid-19, inayosababishwa na virusi vya corona.

“Tunajiandaa kutengeneza chanjo yetu. Kwa hakika itakuwa bora kuliko zote sababu itakabili aina zote za virusi vya corona,” alifichua Museveni alipotangaza hatua kali za kuzuia msambao wa virusi hivyo mnamo Ijumaa.

Kulingana na rais huyo, utengenezaji wa chanjo hiyo ya Uganda ulicheleweshwa na ukosefu wa wagonjwa wa Covid-19.

“Hapo Agosti tulikuwa na shida. Hatukuwa na wagonjwa wa kutosha. Sasa kuna wagonjwa wengi (wa kufanyia majaribio),” alisema na kuongeza kuwa anawasiliana na wadau kadhaa kote ulimwenguni kusaidia katika mzozo wa chanjo.

Museveni aliendelea: “Chanjo tulizopata zinatoa kinga kwa aina chache tu za virusi, kama ile ya kwanza ya Wuhan na iliyoanzia India. Chanjo zilizoko huenda zikose kutoa kinga kamili.”

Alisema kuwa Uganda pia inatengeneza aina mbili za dawa za kutibu Covid-19.

“Hazijachapishwa bado, lakini nina aina mbili za dawa zinazotengenezwa na watu wangu kimyakimya tu. Katika moja, wametibu watu 70 na 58 wamepona,” akahoji.

Rais huyo alidokeza kuwa wanatarajia kufikia Juni 25 wanasayansi wa Uganda watakuwa wamefanya majaribio kwa watu 120 wanaohitajika ili dawa iweze kuidhinishwa.

Kulingana na Museveni, kufikia 2022 Uganda itakuwa ikijitegemea kwa matibabu baada ya kuona ilivyo hatari kutegemea mataifa mengine.

“Kufikia mwaka ujao, Uganda haitakuwa ikitegemea mataifa ya kigeni kwa dawa. Tutakuwa na dawa zetu na chanjo,” alisisitiza.

Huku maswali kuhusu uwezo wa mitishamba katika kutibu Covid-19 yakiibuka, kiongozi huyo alisema: “Tuko na wanasayansi waliosoma ambao wanafahamu matibabu ya kitamaduni. Mmoja wao anafahamu mimea inayotumiwa kutibu surua na maambukizi ya aina tofauti ya virusi.”

Museveni, ambaye Ijumaa alifunga nchi yake kwa siku 42 kufuatia ongezeko la maambukizi ya corona, alidai kwamba mmoja wa wataalamu wake aliponya wagonjwa 30 kwa kutumia mitishamba.

“Corona ilipofika hapa, nilizungumza naye na akaniarifu kwamba alitumia mitishamba yake kwa watu 30, na wote walipona,” alisema.

Takwimu za hivi punde kutoka wizara ya afya nchini humo zinaonyesha kuwa kufikia Juni 19, maambukizi ya corona Uganda yalipanda hadi watu 70,176.

Serikali ilisema watu 42 walifariki ndani ya saa 24. Kwa Museveni, “suluhu ya mwisho ya virusi hivi vya corona ni watu wetu kupata chanjo.”

You can share this post!

Serikali yaonya wimbi la tatu la corona lanukia nchini...

MARY WANGARI: Ni makosa kulazimishia Wakenya vyama vya...