• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 2:00 PM
MARY WANGARI: Ni makosa kulazimishia Wakenya vyama vya kisiasa

MARY WANGARI: Ni makosa kulazimishia Wakenya vyama vya kisiasa

Na MARY WANGARI

WIKENDI jana, maelfu ya Wakenya walipigwa na butwaa kubaini kwamba wengi wao walikuwa wamesajiliwa kisiri katika vyama mbalimbali vya kisiasa.

Lilikuwa jambo la kukasirisha na kuchekesha kwa pamoja, raia walipogeukia mitandao ya kijamii kusimulia walivyogutuka kujipata wamekuwa wanachama wa vyama ambavyo hata hawajawahi kuvisikia.

Wengi walishangaa ni lini na vipi walijisajilisha kuwa wanachama wa vyama hivyo, ikizingatiwa kuwa baadhi yao hata hawaruhusiwi kisheri na taaluma zao kuegemea upande wowote kisiasa.

Inastaajabisha mno kwamba maafisa wa kusajili vyama vya kisiasa wanaweza kuwa na ujasiri wa kuchukua habari za siri za wananchi – kama vile majina, nambari za vitambulisho – na kuwasaijili kama wanachama wa vyama pasipo idhini yao.

Kitendo hicho kimemulika ukora wa vyama vya kisiasa nchini, kuhusu uwezekano kwamba vimekuwa vikisajili wanachama bila kibali.

Ni jambo ambalo pia limetia doa mfumo wa kisiasa nchini uchaguzi mkuu wa 2022 unapozidi kujongea.

Matukio haya yamedhihirisha bayana ukosefu wa sera thabiti za kuhakikisha kuwa, kuna uhifadhi wa data na habari za siri za watu binafsi na mashirika nchini.

Afisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa imeonyesha ukiukaji uliokithiri wa haki za wananchi kikatiba kuhusu faragha, kwa kuingilia data zao za siri bila kibali.

Inavunja moyo kuwa umma usiokuwa na hatia sasa umetwikwa kibarua kigumu cha kujaribu kujiondoa katika vyama walivyosajiliwa bila hiari yao, hasa ikiwa vyama hivyo haviambatani na falsafa na misimamo yao kisiasa.

Tukio hilo limethibitisha umuhimu wa kubuniwa kwa dharura mikakati thabiti, ya kuwezesha kutekelezwa kwa sheria kuhusu uhifadhi wa data za siri.

Tatizo kuhusu kuingiliwa kwa data ya siri limekuwa kero kuu hasa katika enzi hii ya utandawazi na dijitali.

Si ajabu kwamba idadi kubwa ya Wakenya wamekuwa wakihofia kujisajilisha au kutoa maelezo yao muhimu katika tasnia za kielektroniki, ikiwemo mifumo muhimu ya kitaifa.

Matukio kama ya wikendi iliyopita, ambayo kwa hakika yamewafanya wengi kukosa imani na mifumo inayoitisha habari za siri, huenda yakawa pigo kubwa kwa serikali inapojiandaa kuzindua awamu ya pili ya usajili wa Huduma Namba.

Wengi wameachwa wakijiuliza maswali mengi bila kupata majibu: ni kwa kiwango kipi data zao za siri zimekuwa zikiingiliwa, na akina nani, na zimekuwa zikitumika kwa njia gani?

Kulingana na Sheria ya Uhifadhi wa Data 2019, ni hatia kisheria kukusanya na kutumia data ya siri bila idhini kutoka kwa mwenye data hiyo.

Ili kuvutia tena imani ya wananchi, ni sharti Afisi ya Kamishna wa Uhifadhi wa Data ya Siri iwahakikishie Wakenya usalama wa maelezo yao ya siri.

[email protected]

You can share this post!

Covid: Uganda kuanza kuunda chanjo yake – Rais...

Joylove FC yagonga Gikambura ligi daraja la kwanza