• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 12:09 PM
Google taabani kwa kupendelea teknolojia yake katika matangazo ya mitandaoni

Google taabani kwa kupendelea teknolojia yake katika matangazo ya mitandaoni

Na MARY WANGARI

KAMPUNI ya Google huenda ikafanyiwa uchunguzi wa kina zaidi na Umoja wa Uropa (EU) kuhusu teknolojia yake ya matangazo ya bidhaa.

Haya yamejiri karibu miaka miwili tu baada ya wasimamizi hao kufunga shughuli za uchunguzi uliodumu kwa karibu mwongo mmoja.

Kulingana na taarifa iliyotolewa Jumanne, Juni 22, Tume ya Uropa ilisema kwamba uchunguzi wake utatathmini iwapo shirika hilo maarufu la mtandao hukiuka sheria za ushindani kwa kupendelea teknolojia yake binafsi kushinda zile za washindani wake.

Uchunguzi huo vilevile utakagua iwapo Google huwazuia kwa njia isiyo ya haki washindani wake kupata data ya watumiaji mtandao huo na kutathmini mabadiliko kuhusu faragha ambayo yatatupilia mbali baadhi ya mbinu zinazotumiwa na watangazaji bidhaa kupata data.

“Tuna wasiwasi kuwa Google imefanya kuwa vigumu kwa huduma za kutangaza bidhaa mitandaoni kushindana,”

“Huduma za matangazo ya bidhaa mitandaoni ni muhimu mno kwa Google na wachapishaji hupata hela kutokana na huduma zao kimtandao,” Bosi wa EU Margrethe Vestager, alisema.

Hii ni mara ya kwanza kwa EU kuchunguza moja kwa moja kituo kikuu cha matangazo kimtandao ambapo Google huhesabu moja kwa moja na kutoa nafasi na bei kwa watangazaji na wachapishaji mtumiaji mtandao huo anapobonyeza ukurasa huo mtandaoni.

Uchunguzi wa awali wa EU ilizingatia matangazo kuhusu ununuzi, simu na kandarasi za matangazo.

Kupitia taarifa iliyotumwa kwa baruameme, Google ilisema “itaendelea kushirikiana na Tume ya Uropa kujibu maswali yao na kuthibitisha manufaa ya bidhaa zetu kwa biashara na wateja wa Uropa.

“Maelfu ya biashara za raia wa Uropa hutumia bidhaa zetu za matangazo kuwafikia wateja wapya na kufadhili tovuti zao kila siku. Huwa wanazichagua kwa sababu ni bora na zenye ushindani,” ilisema.

Matumizi ya matangazo kidijitali yalikuwa karibu Sh2.6bilioni mnamo 2019.

EU hutoza faini kuambatana na thamani ya mauzo ambayo ni asilimia 10 ya mapato ya kila mwaka.

Google imewahi kutozwa faini ya zaidi ya 970bilioni na EU.

You can share this post!

Kocha Tusker FC asherehekea kuzima Kariobangi Sharks

Wanaume wa Kenya wajikwaa dhidi ya Nigeria voliboli ya...