• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 9:50 AM
Idadi ya waliokufa kwa bomu yafika 95

Idadi ya waliokufa kwa bomu yafika 95

NA XINHUA

ISLAMABAD, PAKISTAN

IDADI ya watu waliofariki kwenye shambulio la kigaidi lililotekelezwa na mshambuliaji wa kujitoa mhanga msikitini siku ya Jumatatu katika mji mkuu wa jimbo la Kaskazini-Magharibi mwa Pakistani, Peshawar imefika 95.

Naibu Kamishna wa Peshawar, Shafiullah Khan, alisema kuwa idadi ya waliofariki iliongezeka baada ya baadhi ya waliojeruhiwa kuaga dunia.

Msikiti huo uliporomoka waumini wakiwa ndani.

Afisa huyo aliongeza kuwa watu 150 walijeruhiwa katika shambulio hilo, ambapo 67 walikuwa wakiendelea kupata matibabu katika hospitali mbalimbali.

Naibu kamishna huyo alisema huenda idadi ya waliofariki ikaongezeka zaidi kwa sababu zaidi ya watu 10 bado wako katika hali mahututi, na wengine kuzikwa chini ya vifusi.

Msemaji wa Hospitali ya Lady Reading, Muhammad Asim, alisema kwamba idadi ya waliofariki iliongezeka baada ya baadhi ya waliojeruhiwa kufariki dunia kutokana na majeraha waliopata.

“Zaidi ya watu 157 walijeruhiwa. Hii ndio maana huenda idadi hizo zikaongezeka,” akasema Asim.

“Watu zaidi ya 15 wako katika hali mahututi.”

Waliofariki ni pamoja na polisi zaidi ya watatu, raia, kiongozi wa maombi na mwanamke mmoja aliyekuwa akiishi katika nyumba moja karibu na msikiti.

Msemaji wa shirika la Rescue-1122, Bilal Faizi, alieleza kwamba wengi bado hawajatolewa chini ya vifusi.

“Kuna wengi ambao bado wamekwama chini ya vifusi. Juhudi za kuwaokoa bado zinaendelea,” akasema Faizi.

Alisema kwamba tayari wamewafikia wengi walionaswa na kuanza kuwapa msaada wa matibabu, ikiwa ni pamoja na oksijeni.

Muhammad Ijaz Khan, afisa wa polisi wa mji mkuu wa Peshawar kaskazini-magharibi mwa jimbo la Khyber Pakhtunkhwa, alisema kuwa zaidi ya watu 300 walikuwa wakisali katika eneo hilo.

“Ni jambo la kushangaza sana. Msikiti huo ulikuwa na watu zaidi ya 300. Maafisa wa polisi na raia wasio na hatia wamepoteza maisha katika shambulio hilo,” akasema Ijaz Khan.

Waziri wa Mambo ya Ndani, Rana Sanaullah Khan, alisema kuwa lengo la mshambuliaji wa kujitoa mhanga lilikuwa ni kuwaangamiza maafisa wa polisi ambao idara yao imekuwa ikipambana na ugaidi.

Nchi hiyo imetaja shambulio hilo kama hatari kwa usalama na kuongeza kuwa uchunguzi umeanzishwa ili kujua jinsi mshambuliaji huyo aliweza kuingia kisiri katika eneo lenye ulinzi mkali.

Vikosi vya usalama vilikuwa vimezingira eneo hilo na kuanzisha uchunguzi kuhusu tukio hilo.

Mshambuliaji huyo wa kujitoa mhanga alijilipua akiwa katikati ya waumini.

Inspekta mdogo wa polisi Mushtaq Khan, ambaye alijeruhiwa katika shambulio hilo, aliviambia vyombo vya habari kuwa alikuwa katika ukumbi wa pili wa kuswalia msikiti huo na alikuwa akijiandaa kuingia katika ukumbi mkuu wakati mlipuko ulitokea na kumfanya apoteze ufahamu.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililaani vikali shambulio hilo.

  • Tags

You can share this post!

Biden akataa kutuma ndege za kivita nchini Ukraine

UFUGAJI: Afurahia ufugaji kuku wa mayai licha ya visiki...

T L