• Nairobi
  • Last Updated May 16th, 2024 6:44 AM
Korti yaagiza mwekezaji kutoka Rwanda arudishiwe Sh400m

Korti yaagiza mwekezaji kutoka Rwanda arudishiwe Sh400m

NA RICHARD MUNGUTI

NAIROBI, KENYA

RAIA wa Rwanda Desire Muhinyuza atasherehekea Mwaka Mpya 2024 akiwa na amani na utulivu moyoni, baada ya Serikali ya Kenya kuamuru arudishiwe Dola 2.6 milioni (sawa na Sh400 milioni) zilizokuwa zimetwaliwa na Polisi kufuatia mzozo wa umiliki wa kampuni ya biashara ya kimtandao kati yake na mfanyabiashara wa humu nchini Bw Kirimi Koome.

Hatua hii ya serikali ni muhimu katika kuimarisha imani ya wawekezaji wanaotoroka nchini mara baada ya kulaghaiwa na baadhi ya Wakenya.

Akiamuru Bw Muhinyuza akabidhiwe kitita hicho, hakimu mwandamizi katika mahakama ya Milimani, Nairobi Bi Dolphina Alego alisema Mahakama Kuu mnamo Desemba 27, 2023, ilimtambua mwekezaji huyo kuwa ndiye mwenye kampuni ya Stay Online Limited (SOL) aliyokuwa amenyang’anywa na Bw Koome kwa njia ya ujanja na ufisadi.

Bi Alego alisema Jaji Alfred Mabeya, ambaye ni mkuu wa kitengo cha biashara katika Mahakama Kuu, alimtambua Bw Muhinyuza kuwa ndiye mmiliki wa SOL, aliyokuwa amelaghaiwa na Bw Koome mnamo Aprili 14, 2023.

Jaji Mabeya alisema katika uamuzi huo wa kihistoria kwamba Bw Koome alitumia ukora na ulaghai kujisingizia na kujitambua kuwa mmiliki wa SOL ilhali alikuwa ameteuliwa na Bw Muhinyuza aiandikishe kwa niaba yake.

“Bw Koome aliteuliwa na Bw Muhinyuza aandikishe SOL, Kenya kwa niaba yake, lakini akajisingizia kuwa yake na kupotosha idara ya usajili wa kampuni katika afisi ya Mwanasheria Mkuu,” Bi Alego alisema.

Punde tu baada ya kuandikisha SOL, Kenya wafanyabiashara kutoka Canada, Estonia, Zambia, Tanzania, Uganda, na Kenya waliwekeza zaidi ya Dola 2.6 milioni (Sh400 milioni) katika biashara hiyo ya jukwa la mtandaoni.

Kuona kwamba amepokonywa kampuni ya SOL, Bw Muhinyuza alilalamika kwa polisi kwamba ametapeliwa kampuni na pesa na Bw Koome ndipo, idara ya uchunguzi wa jinai (DCI) ikafika kortini na kupata agizo la kutwaa pesa hizo sizipotee.

Na wakati huo huo Bw Muhinyuza akalalamikia idara ya usajili wa kampuni katika afisi ya mwanasheria mkuu kwamba Bw Koome alificha ukweli kuhusu umiliki wa SOL.

Pia Bw Muhinyuza kupitia mawakili Danstan Omari, Shadrack Wambui, Sophie Nekesa, Ronald Momanyi na Aranga Omaiyo alimshtaki Bw Koome katika mahakama kuu akiomba ashurutishwe arudishe kampuni na pesa za wateja walioekeza katika SOL, Kenya.

Baada ya kutathmini ushahidi uliowasilishwa na Bw Omari, Jaji Mabeya alifikia uamuzi kwamba SOL ni yake Bw Muhinyuza.

Alisema mwekezaji huyo aliekeza USD ($)129,000 katika SOL na Bw Koome “hakutoa hata senti moja kufanikisha biashara na usajili wake.”

Jaji huyo alimwagiza Bw Koome anayeshtakiwa mbele hakimu mkazi Bw Ben Mark Ekhubi kwa kula njama za kumlaghai Bw Muhinyuza kiasi cha Dola 2.6 milioni na wizi wa Dola 100,000 arudishe pesa hizo.

Ijumaa ,viongozi wa mashtaka Bi Dorcus Rugut na James Gachoka walisema ijapokuwa Bw Koome anadai pesa hizo ni zake “hana mamlaka yoyote juu ya pesa hizo.”

Bi Rugut alisema Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Renson Igonga ameamuru polisi wamrudishie Bw Muhinyuza kiasi hicho Dola 2.6 milioni.

Bi Alego alisema serikali imeagiza pesa hizo zirudishwe kwa mwekezaji huyo aendelee na biashara na kubuni ajira kwa wakenya.

Kabla ya polisi kuagizwa kurudisha pesa hizo Bw Koome alipinga ombi hilo akisema “apewe muda wa wiki mbili atafute wakili awasilishe ombi la kuzuia kutwaliwa kwa pesa hizo na Muhinyuza.”

Bw Koome alisema : “nimewatimua kazini mawakili Cliff Ombeta, Jackson Omwanza na hivyo nahitaji muda wa kumtafuta wakili mwingine kwa vile sielewi ombi hili la DPP na madhara yake katika kesi hii inayonikabili.”

Mahakama iliombwa na wakili Danstan Omari isitilie maanani ombi la Bw Koome kwa vile “pesa anazodai sio zake.”

Bi Rugut alisema DPP hapingi pesa hizo zilizokuwa zimezuiliwa kama ushahidi katika kesi inayomkabili Bw Koome.

Bi Rugut alisema Desemba 27, 2023, Bw Koome hajakata rufaa kupinga uamuzi wa kumng’oa katika kampuni ya SOL na agizo la kulipa fidia na kurudishia Muhinyuza Dola 100,000 alizomdanganya zilikuwa za kulipia kodi biashara ya SOL lakini “akazitia kibindoni.”

Bi Alego alielezwa kesi inayomkabili Bw Koome ni kwamba alikula njama za kumlaghai Bw Muhinyuza kiasi Dola 2.6 milioni na wizi wa Dola 100,000.

Mahakama ilikubalia ombi la DPP na kuagiza pesa hizo arudishiwe Muhinyuza.

Sasa Bw Koome atapambana na hali yake na kesi ya ufisadi inayomkabili.

Kesi inayomkabili Bw Koome itaanza kusikilizwa Februari 9, 2023.

Alikana mashtaka manne ya ufisadi na wizi na yuko nje kwa dhamana ya pesa taslimu Sh500,000

  • Tags

You can share this post!

Kero ya rundo la taka sokoni Mamboleo

Mwanafunzi aliyeangaziwa na ‘Taifa Leo’ apata...

T L