• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 7:50 AM
Maelfu walazimika kuondoka katika makazi yao kufuatia mlipuko wa volkeno DRC

Maelfu walazimika kuondoka katika makazi yao kufuatia mlipuko wa volkeno DRC

Na MASHIRIKA

GOMA, DRC

SERIKALI katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) Jumapili imewahimiza wakazi katika eneo la Goma mashariki kuhama baada ya volkeno katika eneo hilo kulipuka.

Moto kutoka Mlima wa Volkeno wa Nyiragongo ulienea katika uwanja wa ndege wa Goma mapema Jumamosi, Mei 23.

Maelfu ya wakazi waliobeba magodoro na virago vingine walitoroka mji huo wa mpakani wakikimbia kuelekea mpaka wa Rwanda.

Moto huo uliacha kusambaa baada ya kufika viungani mwa Goma kulingana na ripoti eneo hilo.

Mlipuko wa mwisho wa Volkeno ya Nyiragongo ulitokea mnamo 2002 ambapo watu 250 waliuawa na wengine 120,000 kuachwa bila makao.

Mlima huo ni miongoni mwa volkeno zinazolipuka mara nyingi ziadi na unachukuliwa kama mojawapo wa milima hatari zaidi.

“Mpango wa kuhamisha watu kutoka mji wa Goma umeanzishwa ambapo Serikali tayari inajadili kuhusu mikakati ya dharura itakayochukuliwa kwa sasa,” Waziri wa Mawasiliano aliandika kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter.

Shughuli hiyo ilianzishwa baada ya mkutano wa dharura jijini Kinshasa kama alivyosema.

Afisi ya Rais nchini humo ilisema Rais Felix Tshisekedi alikatiza ziara yake bara Uropa na kurejea DRC.

Gavana wa kijeshi anayesimamia eneo la Kivu Kaskazini ambalo ni jiji kuu la Goma, alithibitisha kuhusu mlipuko huo wa volkeno uliotokea saa moja usiku.

Jenerali Constant Ndima aliwahimiza wakazi wa Goma, mji wenye watu milioni mbili kwenye Mlima wa Nyiragongo, sehemu ya kusini na ufuo wa kaskazini wa Ziwa Kivu, kuwa na utulivu.

Mapema siku iliyotangulia, wakazi waliripoti kuhusu harufu kali ya sulphur mitaani katika mji wa mashariki na miale myekundu iliyoenea katika anga na kufunika mji huo.

Ingawa hivyo, baadhi ya wakazi waliokuwa wametafuta mahala salama wameonekana Jumapili wakirudi katika “eneo hatari” hata kabla ya tamko lolote kutoka kwa serikali.

Tafsiri: MARY WANGARI

You can share this post!

Shughuli ya utoaji chanjo ya polio yazinduliwa Kiambu

Virusi vya corona vinavyohangaisha India vilizuka kitambo...