• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 1:13 PM
Ronaldo abeba Man-United dhidi ya Tottenham ligini

Ronaldo abeba Man-United dhidi ya Tottenham ligini

Na MASHIRIKA

CRISTIANO Ronaldo, 37, alifungia Manchester United mabao matatu katika mchuano mmoja kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 14 mnamo Jumamosi na kuchochea waajiri wake hao kupepeta Tottenham Hotspur 3-2 katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) ugani Old Trafford.

Ronaldo ambaye ni raia wa Ureno aliwaweka Man-United kifua mbele mara mbili kabla ya kushirikiana na Alex Telles na kufungia mabingwa hao mara 20 wa EPL bao la ushindi katika dakika ya 81. Bao hilo lilikuwa lake la 807 kitaaluma.

Tottenham wanaotiwa makali na kocha Antonio Conte walijibu mapigo ya Ronaldo mara mbili kupitia penalti ya Harry Kane katika dakika ya 35 na bao la beki Harry Maguire aliyejifunga kunako dakika ya 72.

Hata hivyo, ni Ronaldo ndiye aliibuka shujaa wa gozi hilo baada ya kufungia Man-United mabao matatu katika mechi moja kwa mara ya kwanza tangu Januari 2008 alipoongoza kikosi hicho kusajili ushindi wa 6-0 dhidi ya Newcastle United ligini.

Ushindi wa Man-United sasa unaweka hai matumaini yao ya kukamilisha kampeni za EPL msimu huu ndani ya mduara wa nne-bora huku wakilenga pia kuwazamisha Atletico Madrid katika Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo Machi 15, 2022 ugani Old Trafford.

Kufikia sasa, Man-United wanakamata nafasi ya nne kwenye msimamo wa jedwali la EPL kwa alama 50, sita nyuma ya nambari tatu Chelsea ambao wana mechi mbili zaidi za kutandaza ili kufikia idadi ya michuano 29 ambayo tayari imepigwa na Man-United ligini. Arsenal wanashikilia nafasi ya tano jedwalini kwa pointi 48 kutokana na mechi 25 pekee.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Majeshi ya Putin sasa yabisha Kyiv

Brentford wazidisha masaibu ya Burnley katika EPL

T L