• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 8:55 PM
Tahadhari uchaguzi Nigeria ukianza leo Jumamosi

Tahadhari uchaguzi Nigeria ukianza leo Jumamosi

NA AFP

ABUJA, NIGERIA

SERIKALI ya Nigeria imeamuru kufungwa kwa mipaka yake yote ya ardhini huku ikidhibiti safari za magari kufanikisha usafirishaji wa vifaa vya kupigia kura, uchaguzi mkuu ukianza leo Jumamosi.

Nazo nchi kadha za kigeni zimewataka viongozi nchini Nigeria kuhakikisha uchaguzi huo unaendeshwa kwa njia ya haki na katika mazingira ya amani.

Jumla ya raia 93 milioni wanashiriki uchaguzi huo ambao kwa mara ya kwanza, tangu kutamatika kwa uongozi wa kijeshi 1999, utashuhudia ushindani mkali kati ya wagombeaji urais watatu.

“Ni muhimu kwa uthabiti na kunawiri kwa demokrasia nchini Nigeria ikiwa uchaguzi huo utaendeshwa na kukamilishwa katika mazingira salama,” ikasema taarifa ya pamoja kutoka kwa balozi za Amerika, Uingereza, Australia, Japan, Canada na Norway.

“Tunahimiza wadau wote kuchukua hatua za kupunguza taharuki na kuepuka machafuko yoyote,” ikaongeza.

Wao ni; Bola Tinubu wa chama tawala cha All Progressive Congress (APC), Atiku Abubakar wa chama kikuu cha upinzani People’s Democratic Party (PDP) NA Peter Obi wa Chama cha Leba (LP) wanaopania kumrithi Rais Mohammadu Buhari.

Na kwa mara ya kwanza, mgombeaji asiyedhaminiwa na mojawapo ya vyama vikuu vya kisiasa anapigiwa upatu kushinda katika kinyang’anyiro cha urais.

Mgombeaji huyo ni Bw Obi, 61, ambaye mwaka jana alihama kutoka chama tawala cha PDP hadi chama cha LP.

Katika matokeo ya kura tano za maoni ambazo zimetolewa tangu mwaka jana, Obi ameibuka mwenye umaarufu mkubwa zaidi.

Mgombeaji huyo wa urais ametumia mitandao ya kijamii kusaka kura kutoka haswa kwa vijana ambao wamevunjika moyo na kuchoshwa na mtindo wa zamani ambapo wanasiasa wazee ndio huwania urais.

Bw Tunubu na Bw Abubakar wako katika umri wa miaka 70.

Lakini wachanganuzi wanahoji ikiwa matokeo ya kura ya maoni yanayoonyesha Obi akiongoza yanaakisi ukweli. Wanasema kuwa mgombeaji huyo, hana rasilimali na ushawishi mkubwa wa kisiasa, ukilinganishwa na ule wa wagombeaji Tinubu na Abubakar.

Hata hivyo, yeyote ambaye wapigakura watamchagua kurithi Rais Buhari, atakuwa na kibarua kigumu cha kukabiliana na changamoto nyingi ambazo zimekumba serikali ya sasa.

Hizi ni pamoja na ujangili na mashambulio ya kigaidi ambayo sasa yanashuhudiwa katika sehemu nyingi za Nigeria, haswa kaskazini mwa Nigeria.

Pia nchi hiyo inakumbwa na kero la ufisadi, ambalo linadumaza uwekezaji na kuwatajirisha wachache wenye mamlaka, kupanda kwa mfumko wa bei za bidhaa na uhaba wa pesa kufuatia makosa yaliyotokea baada ya kuzinduliwa kwa sarafu mpya mwaka 2022.

Wagombeaji wote wakuu wametoa ahadi za kupambana na matatizo hayo.

Kufuatia hofu kwamba matokeo ya ushindani wa karibu yanaweza kupingwa na kusababisha fujo, wagombeaji wote wa urais walitia saini makubaliano ya kudumisha amani.

Katika makubaliano hayo yaliyotiwa saini Jumatano, kila mmoja aliahidi kuelekea mahakamani ikiwa hataridhishwa na matokeo yatakayotangazwa.

“Hii ndio nchi ya pekee tuliyonayo na sharti tufanye kila tuwezalo kuhakikisha kuwa ni salama, imeungana na ni tulivu. Fujo na mapigano hayafai kutokea baada ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi wa urais,” Buhari akasema wakati wa kutiwa saini makubaliano hayo jijini Abuja.

Wapigakura pia watachagua wabunge wapya watakaohudumu kwa miaka mitano ijayo.

“Huu ndio uchaguzi wenye ushindani mkubwa zaidi kuwahi kufanyika katika taifa hili,” alisema Profesa Abiodum Adeniyi wa Chuo Kikuu cha Baze, jijini Abuja.

  • Tags

You can share this post!

Wito mradi wa gesi wa Taifa uwafaidi wakazi wa Pwani

Vihiga Queens, Nakuru City Queens kitaeleweka ligini KWPL...

T L