• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:09 AM
Tiba za kiasili za China tishio kwa Afrika-Ripoti

Tiba za kiasili za China tishio kwa Afrika-Ripoti

Na MASHIRIKA

BEIJING, CHINA

UPANUZI UNAOUNGWA mkono na Beijing kuhusu Dawa za Kiasili za China (TCM) katika mataifa mengi ya Afrika, unatishia kuchochea ulanguzi wa wanyamapori, ripoti mpya imeonya.

Unahatarisha vilevile hatima ya wanyamapori wanaokabiliwa na tishio la kutokomea duniani.Ukuaji wa soko la TCM ukiandamana na dhana ya Afrika kama kituo kikuu cha viungo vya TCM ni “janga kuu kwa baadhi ya wanyamapori wanaokabiliwa na hatari ya kuangamia kama vile chui, pangolini na vifaru,” ilisema ripoti iliyochapishwa jana na Shirika la Kuchunguza Masuala ya Mazingira (EIA), lenye makao yake London, Uingereza.China imekuwa ikipigia debe dawa za kiasili zilizodumu kwa zaidi ya miaka 2,500 iliyopita, pamoja na mradi wake mkuu wa Belt and Road Initiative, unaoboresha barabara, reli na miradi mingine mikuu ya miundomsingi kote Barani Afrika.

Huku idadi kubwa ya matibabu ikitokana na mimea, mahitaji kutoka kwenye sekta hiyo, yamelaumiwa kwa kushinikiza wanyamapori ikiwemo pangolini na vifaru kuelekea kutokomea. “Hatimaye, ukuaji usiodhibitiwa wa TCM ni tishio kuu kwa mazingira asilia yanayopatikana katika mataifa mengi Afrika, yote haya kwa ajili ya kupata faida ya muda mfupi,”“Matumizi yoyote ya viumbe wanaokabiliwa na hatari katika TCM huenda yakachochea mahitaji zaidi, kuchochea uhalifu kuhusu wanyamapori na mwishowe kusababisha matumizi mabaya kukithiri,” alisema mwanaharakati wa wanyamapori, EIA, Ceres Kam kupitia taarifa.

Ripoti hiyo inayofahamika kama Tiba Hatari: Jinsi upigiaji debe wa baadhi ya dawa za kiasili za China -Afrika unavyozua hatari kuu kwa wanyamapori wanaokabiliwa na tishio.Inahoji kuwa bidhaa za TCM zimeenezwa mno Afrika huku kampuni na kliniki za TCM zikianzishwa kote barani nayo Beijing ikizidisha kampeni za kuzipigia debe kuambatana na janga la COVID-19.

Kulingana na ripoti hiyo, baadhi ya wauzaji wananuia kuanzisha mchakato kamili wa bidhaa hizo kuanzia zinapotoka hadi mauzo.Imehimiza uangalizi wa makini zaidi na hatua kutoka kwa serikali ili kuzuia TCM dhidi ya kutumia wanyama walio hatarini katika bidhaa zake.

Japo China imeahidi kukomesha matumizi ya viumbe adimu katika tiba za kiasili, bado kunao wanaotoa dawa hizo kama tiba ya kuamsha hamu ya ngono au kutibu maradhi kuanzia saratani hadi matatizo ya ngozi.

Mwelekeo kuhusu marufuku dhidi ya matumizi ya pembe za kifaru na viungo vya simbamarara ilitangazwa 1993 na kisha kuondolewa ghafla 2018 kabla ya serikali kugeuza mkondo, ungali una utata.“Tunaelewa kuwa tiba za kiasili ni muhimu kwa tamaduni nyingi na zinachangia nafasi muhimu katika huduma ya afya Afrika na kwingineko,” alisema Kam.

“Wasiwasi wetu mkuu ni kwamba upanuzi kama huo wa TCM kwa kiwango kikubwa Afrika, jinsi inavyofanyika chini ya mpango wa China’s Belt and Road Initiative, utakuwa na athari hasi za kuongeza upesi mahitaji ya matibabu yanayosheheni wanyamapori na hivyo basi, kusababisha viumbe zaidi kuhatarishwa au kutoweka,” aliongeza.

Huku janga la COVID-19 likiendelea, huduma ya afya ikiwemo kuimarisha uhusiano kati ya TCM na tiba za Kiafrika, huenda ikawa suala kuu katika Kongamano lijalo kuhusu Ushirikiano kati ya China-Afrika (FOCAC), lililopangiwa kuanza Senegal mwishoni mwa mwezi huu.

You can share this post!

Sagasaga Kenya, UG zikifufua uhasama mechi ya kufuzu Kombe...

Maeneo 8 ya kuamua rais mpya katika 2022

T L