• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 1:16 PM
Sagasaga Kenya, UG zikifufua uhasama mechi ya kufuzu Kombe la Dunia

Sagasaga Kenya, UG zikifufua uhasama mechi ya kufuzu Kombe la Dunia

Na CECIL ODONGO

KENYA na Uganda leo zitafufua uhasama wa tangu jadi katika soka, zitakapokabiliana katika mechi ya kufuzu Kombe la Dunia 2022 jijini Kampala.

Mechi hiyo ya Kundi E ambayo inatarajiwa kusisimua mno, itasakatiwa uwanja wa St Mary’s Kitende kuanzia saa 10 jioni.Serikali ya Rais Yoweri Museveni imekubali kuruhusu zaidi ya nusu ya mashabiki katika uga huo wenye uwezo wa kusitiri watu 25,000.

Viongozi wa Kundi E, Mali, nao watakuwa uga wa Nyamirambo jijini Kigali kupepetana na Amavubi Stars ya Rwanda, kuanzia saa moja jioni. Mali inaongoza kundi hilo kwa alama 10, Uganda (nane), Kenya (mbili) huku Rwanda ikiwa na alama moja.

Huku Kenya ikiwa haina nafasi ya kuelekea Qatar, Uganda na Mali zinapigania kumaliza nambari moja kundini kwani ni timu moja pekee inafuzu kujiunga na viongozi wa makundi mengine tisa katika hatua ya muondoano.

Mechi za muondoano zitasakatwa mwaka ujao ambapo mataifa matano yatafuzu kuwakilisha bara Afrika katika Kombe la Dunia, litakaloandaliwa Qatar kuanzia Novemba 21 – Desemba 18.Hapo jana, kikosi cha wachezaji 25 wa Harambee Stars kiliondoka nchini na kufika salama salmini Uganda, kisha wakafanya mazoezi katika uga wa St Mary’s Kitende baadaye jioni.

Timu hiyo inayonolewa na kocha Engin Firat wa Uturuki, iliandamana na watu wengine 15 ambao wanajumuisha wanachama wa benchi ya kiufundi pamoja maafisa wa Shirikisho la Soka Nchini (FKF).

Tayari mechi hiyo imezingirwa na hisia kali, mkufunzi wa Uganda Cranes Milutin ‘Micho’ Sredojevic akisisitiza kuwa, vijana wake hawana jingine ila kupigana wapate ushindi.Kenya ilishinda Uganda mara ya mwisho ugenini 2-1 katika mechi ya kirafiki mnamo Mei 26, 1996.

Tangu wakati huo Stars imeenda sare mara tano na kupoteza mara nne nyumbani kwa majirani hao.“Mechi hii ina umuhimu mkubwa kwetu kwa sababu Kenya ndio kizingiti katika kufuzu kwa raundi ya mwisho. Lazima tushinde ili hata Mali wakishinda au kujikwaa, kihesabu bado tuwe na nafasi katika mechi yetu ya mwisho,” akasema raia huyo wa Serbia.

Uganda inatarajiwa kupepetana na Mali ugenini mnamo Jumapili, huku Kenya ikiwa mwenyeji wa Rwanda siku iyo hiyo kutamatisha mechi za Kundi E.Hata hivyo, mkufunzi wa Stars Firat naye amekariri kuwa Kenya lazima ishinde mechi zake mbili zilizosalia dhidi ya Uganda na Rwanda.

Firat jana alishangaza kwa kutaja washambuliaji wawili pekee kikosini, suala ambalo lilionekana kuwakera mashabiki wa timu ya taifa. Nahodha Michael Olunga na mvamizi wa zamani wa Tusker ambaye alichezea Stars mara ya mwisho mnamo 2012, Ismael Dunga, ndio wanatarajiwa kuongoza safu ya kuvurumisha matulinga dhidi ya Uganda.

Awali katika dhifa ya chakula cha jioni katika mkahawa moja jijini Nairobi Jumanne usiku, Rais wa FKF Nick Mwendwa alilalamika kuwa serikali imetelekeza timu hiyo na haijawapa ufadhili wowote.“Tiketi ambayo Olunga alitumia kusafiri hadi Nairobi haijalipiwa.

Tumeomba ufadhili kutoka kwa serikali na hata tulituma barua wiki haijajibiwa. Tumezungumza na watoaji huduma ambao wamekubali kutoa huduma zao kwa mkopo,” akasema Mwendwa.

You can share this post!

Waziri ataka afya ya akili ipewe uzito unaostahili

Tiba za kiasili za China tishio kwa Afrika-Ripoti

T L