• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 6:07 PM
Wahamiaji 19 wafa maji wakielekea Italia

Wahamiaji 19 wafa maji wakielekea Italia

NA MASHIRIKA

TUNIS, TUNISIA

WAHAMIAJI 19 kutoka mataifa kadhaa ya Afrika Jumamosi walifariki katika Pwani ya Tunisia, baada ya mashua waliyokuwa wakisafiria kuzama walipokuwa wakijaribu kuvuka Bahari ya Mediterranean kuelekea nchini Italia.

Kulingana na shirika moja la kutetea haki za binadamu, ajali hiyo ilifanyika baada ya mashua hiyo kuzidiwa na nguvu ya mawimbi ya bahari.

Kwa siku nne zilizopita, mashua tano zimezama katika mji wa kusini wa Sfax, hali ambayo imesababisha vifo vya watu tisa huku 67 wakiwa hawajulikani waliko.
Hali hiyo imechangiwa na ongezeko la mashua ambazo zimekuwa zikielekea nchini Italia.

Walinzi katika pwani hiyo waliwaokoa watu watano baada ya mashua yao kuzama katika pwani ya Mahdia, kulingana na Romadan ben Omar, ambaye ni afisa mkuu katika shirika la Forum for Social and Economic Rights (FTDES).

Idara za serikali ya Tunisia hazikutoa maelezo mara moja.

Mlinzi mmoja alisema kuwa wamesimamisha zaidi ya mashua 80 zilizokuwa zikielekea Italia katika muda wa siku nne zilizopita. Alisema kuwa kando na mashua hizo, wanawazuilia wahamiaji zaidi ya 3,000.

Pwani hiyo imeibukia kuwa eneo maarufu linalotumiwa na wahamiaji kuelekea Ulaya. Wengi wao wamekuwa wakitoroka hali za umaskini na vita vinavyoendelea katika mataifa ya Afrika na eneo la Mashariki ya kati. Wengi wao wamekuwa wakielekea Ulaya kutafuta maisha bora katika mataifa ya Ulaya.

Kisa hicho kinajiri huku vikosi vya Tunisia vikiendesha operesheni kali dhidi ya wahamiaji kutoka Afrika.

Kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa (UN), zaidi ya wahamiaji 12,000 walioingia Italia mwaka huu walitumia bandari za Tunisia. Hii ni ikilinganishwa na wahamiaji 1,300 katika wakati kama huo mwaka 2022.

  • Tags

You can share this post!

Sayari 5 kuonekana angani Jumanne jioni

Raila ahutubia waandamanaji Kawangware

T L