• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 7:05 PM
Zelensky amkashifu Guterres kwa ziara nchini Urusi kwanza

Zelensky amkashifu Guterres kwa ziara nchini Urusi kwanza

NA MASHIRIKA

KYIV, UKRAINE

RAIS Volodymyr Zelensky wa Ukraine, Jumamosi alikashifu vikali hatua ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Antonio Guterres, kuzuru Urusi kabla ya kuitembelea nchi yake.

Guterres anatarajiwa kukutana na Rais Vladimir Putin wa Urusi hapo kesho, kwenye juhudi za kujaribu kutatua mapigano yanayoendelea kati ya nchi hiyo na Ukraine.

“Ni makosa sana kwa (Guterres) kuzuru Urusi kabla ya kuitembelea Ukraine,” akasema Zelensky, kwenye kikao na wanahabari jijini Kyiv.

Alieleza kuwa jijini Kyiv pekee, vikosi vya Urusi vimewaua zaidi ya watu 1,000.

Baada ya kukutana na Putin kesho, Guterres amepangiwa kukutana na Rais Zelensky Alhamisi.

Katibu huyo pia amepangiwa kukutana na wafanyakazi wa UN kujadili kuhusu mikakati ya kuimarisha njia za kutoa misaada kwa waathiriwa wa mapigano hayo.

Tangu Guterres kuilaumu Urusi dhidi ya kukiuka kanuni za UN kwa kuyatuma majeshi yake Ukraine, Putin amekuwa akikwepa mazungumzo yoyote na katibu huyo.

Hata hivyo, amekuwa akizungumza mara kwa mara na Zelensky kuhusu athari za vita hivyo.

Jumanne wiki iliyopita, Guterres aliikashifu tena Urusi kwa kuendeleza mashambulio yake mashariki mwa Ukraine, akiziomba nchi hizo mbili kusitisha mapigano hayo angaa kwa siku nne kama heshima kwa Sikukuu ya Pasaka.

Zelensky anashikilia kuwa hatima ya vita hivyo italingana na mwelekeo atakaochukua Putin baada ya kikao hicho.

You can share this post!

NMS kukumbatia teknolojia katika huduma za uegeshaji

Raila aanza mikutano na Wakenya Marekani

T L