• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 6:55 PM
Raila aanza mikutano na Wakenya Marekani

Raila aanza mikutano na Wakenya Marekani

NA WINNIE ONYANDO

KINARA wa ODM, Raila Odinga jana Jumapili alianza rasmi mkutano wake na Wakenya wanaoishi Marekani baada ya kuwasili katika nchi hiyo Ijumaa.

Ziara yake itakayodumu kwa wiki moja, itahusisha msururu wa mikutano ambapo Bw Odinga amepangiwa kukutana na maafisa wa serikali ya Marekani.

Pia anatarajiwa kushauriana na maafisa wa vitengo vya kushirikisha serikali ya Marekani mbalimbali kati ya leo na Jumanne.

Baada ya hapo, Bw Odinga atakutana na kitengo cha kutunga sheria nchini Marekani na baadaye kukutana na viongozi wakuu wa Seneti na Bunge huko Capitol Hill.

Kadhalika, anatarajiwa kuzungumza na viongozi katika taasisi muhimu za jijini Washington, DC.

Taasisi hizo ni pamoja na Baraza la Atlantic na Kituo cha Maendeleo ya Ulimwengu.

Katika mkutano wa Jumapili, Bw Odinga aliwafahamisha raia hao wa Kenya kuhusu hali ya nchi, maandalizi ya uchaguzi wa Agosti 9 na mipango yake ya baada ya uchaguzi.

Katika mazungumzo yake na shirika la Amerika, Bw Odinga atatambua na kuthamini mashirika ya Marekani ambayo yameanzishwa nchini Kenya na kuhimiza wadau wa kundi hilo kukabiliana na changamoto ya kuwekeza nchini Kenya.

Atawaeleza kuhusu nafasi zilizopo nchini na Afrika, na kutoa wito wa ushirikiano katika vita dhidi ya ufisadi.

“Bw Odinga pia atawaeleza wawekezaji hao kuhusu maandalizi ya uchaguzi na kueleza mipango yake ya baada ya uchaguzi ya kuifanya nchi iwe mahali ambapo mtu anaweza kuwekeza bila uoga,” ripoti ikasoma.

Bw Odinga pia anatarajiwa kuwafahamisha maafisa wakuu wa serikali ya Marekani kuhusu maandalizi ya uchaguzi na mipango ya baada ya uchaguzi wa Kenya.

Atatoa wito wa ushirikiano ili kuvutia biashara na uwekezaji nchini na juhudi za pamoja za kupambana na ufisadi.

Baadhi ya viongozi walioandamana na Bw Odinga ni magavana James Ongwae (Kisii) na Wycliffe Oparanya (Kakamega), Martha Karua, aliyekuwa mbunge wa Aldai, Sally Kosgey, seneta wa Homa Bay, Moses Kajwang, mbunge wa Kathiani, Robert Mbui, Peter Kaluma, John Mbadi, Esther Passaris, Suleiman Shabhal, Makau Mutua miongoni mwa wengine.

  • Tags

You can share this post!

Zelensky amkashifu Guterres kwa ziara nchini Urusi kwanza

UhuRuto walivyofuta mafanikio ya Kibaki

T L