• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 4:43 PM
Afunguka kueleza jinsi anavyoishi baada ya kutemwa

Afunguka kueleza jinsi anavyoishi baada ya kutemwa

Na SAMMY WAWERU

PETER Irungu ni mfanyabiashara kiungani mwa jiji la Nairobi na ambaye anajishughulisha na biashara ya juakali.

Licha ya kuwa amenogesha biashara yake, ana kovu la uchungu moyoni.

Baada ya kufanya mtihani wa kitaifa kidato cha nne, KCSE mnamo 2006 Irungu alihamia jijini Nairobi kutafuta vibarua kujiendeleza kimaisha.

Kwa sababu hakuwa na kozi yoyote ile, anasema alifanya vibarua vya hapa na pale, vikiwemo kuwa shamba boi na kusafirisha mizigo.

Baadaye, kupitia akiba aliyoweka alisomea udereva.

“Sikupata kazi ya kuendesha magari, nikaishia kuweka kinyozi na ambacho kiliniinua na kunifungua macho,” Irungu anasema.

Mambo yalipoimarika, barobaro huyu anasema aliamua kuasi ukapera mwaka wa 2012. “Tulijaaliwa mtoto mmoja,” anafichua.

Kulingana na Irungu, kwa kuwa alikuwa na hamu na familia alifanya kila awezalo kuhakikisha kwamba ameiimarisha, muhimu zaidi ikiwa ni kuikidhi riziki na mahitaji mengine muhimu ya kimsingi.

Kwenye masimulizi yake, alifanya kazi kwa bidii ili kuona inaishi maisha bora.

Hata hivyo, kilichoanza kama utani mke wake kusisitiza alitamani maisha ya mashambani, kiliishia kuwa kovu la kidonda moyoni.

“Alinieleza mara kwa mara anapenda shughuli za kilimo, hivyo basi nafsi yake ingetulizwa na kuhamia mashambani,” anadokeza.

Irungu anasema hakujua ilikuwa njia ya kumtema, kwani kilele cha hatua hiyo, miaka minne baadaye, kilikuwa kuingia kwenye ndoa nyingine.

Asijue kosa alilofanya kupokezwa adhabu ya aina hiyo, Irungu anasema imesalia kuwa kidonda cha moyo.

Isitoshe, jitihada za kujaribu kushirikisha familia ya aliyekuwa mkewe kupata jawabu zimeambulia patupu.

Kulingana na Askofu Wilson Karanja, ambaye ni mshauri nasaha wa masuala ya ndoa, cha busara kwenye ndoa ni watu kuvumiliana endapo changamoto zinazojiri na kushuhudiwa zinaweza kutatuliwa au kutatulika.

Hata hivyo, Mtumishi huyu wa Mungu anahimiza haja ya machumbiano kabla ya kuingia katika ndoa, ili kusoma mwenzako nje na ndani.

“Mungu haridhishwi na talaka na maandiko yake yanashauri haja ya kutatua mizozo inapoibuka badala ya kuachana. Ndoa nyingi zinazosambaratika hasa katika jeneresheni ya kisasa, kidijitali, inachangiwa na wachumba kutojipa muda wa kutosha kujuana. Ni muhimu pia kushirikisha Mungu kwa njia ya maombi,” Askofu Karanja anahimiza.

Akitoa ushauri kwa wanaotengana pengine kwa msingi ndoa ilishuhudia vita vya kijinsia kiasi cha mwathiriwa kutovumilia, Askofu Karanja anashauri wahusika kufahamu majukumu yao katika malezi ya mtoto au watoto waliojaaliwa.

“Utengano usiwe kizingiti cha kutosaidia watoto, kila mmoja ashiriki,” anasisitiza.

Kwa mujibu wa sheria za Katiba ya Kenya, watoto walio chini ya umri wa miaka 18 wanapaswa kuishi na mama. Wanapofikisha umri huo, sheria imeeleza wazi watatoa uamuzi wa ni nani watataka kuishi naye, mama au baba.

Kulingana na Peter Irungu, anafanya kila awezalo kuhakikisha mwanawe anapata kila hitaji licha ya kuwa yuko mikononi mwa mama yake.

Akiendelea kuwa na matumaini ipo siku watarudiana kutokana na mapenzi yalivyokolea, Irungu 36 anahimizwa kutafuta ushauri nasaha ili kutuliza moyo wake.

You can share this post!

Maktaba ya kitaifa kurejelea huduma zake za kitaifa kwa umma

Arsenal na Man-United nguvu sawa ligini