• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 8:55 PM
Harakati za utoaji chanjo ya HPV nchini zasuasua

Harakati za utoaji chanjo ya HPV nchini zasuasua

Na PAULINE ONGAJI

NI takriban miaka mitatu tangu serikali ya Kenya ilipozindua rasmi utoaji chanjo dhidi ya Human Papillomavirus (HPV), virusi vinavyosababisha kansa ya lango la uzazi.

Mpango huu ulipozinduliwa mwaka wa 2019, wasichana wenye umri wa miaka kumi nchini kote walitarajiwa kupokea dozi mbili za chanjo hii kila baada ya miezi sita, katika mradi uliohusisha ushirikiano kati ya Wizara ya Afya, Muungano wa kimataifa wa dawa za chanjo na utoaji chanjo (Global Alliance for Vaccines and Immunization-Gavi) , UNICEF na Shirika la Afya Duniani -WHO.

Kulingana na wataalam, baada ya uchunguzi wa muda mrefu ilithibitishwa kwamba chanjo hii ilikuwa na uwezo mkubwa kukinga dhidi ya virusi hivi.

“Kwa kawaida chanjo hii huchochea mfumo wa kingamwili ili uzalishe mizindiko inayopiga vita virusi halisi endapo kutatokea maambukizi,” aeleza Prof Mansoor Saleh, Mwenyekiti wa idara ya maradhi ya damu na onkolojia katika Aga Khan University Hospital.

Lakini licha ya haya, tangu kuzinduliwa kwake, chanjo hii imekumbana na pingamizi kali. Kwa mfano, kuna baadhi ya wataalam wanaohoji kwamba asilimia 90 ya maambukizi yote ya HPV hujitatua na mara nyingi virusi hivi huangamizwa na mfumo wa kingamwili, kumaanisha kwamba hakuna haja ya kupokea chanjo.

Prof Mansoor asema ni kweli kwamba HPV yaweza kujitatua, lakini ikiwa haitafanyika hivyo, yaweza sababisha matatizo ya kiafya.

“Hakuna jinsi ya kutabiri ni watu gani walio na virusi vya HPV watakaokumbwa na kansa au matatizo mengine ya kiafya na ndiposa tunasisitiza umuhimu wa kupimwa kila wakati na kupokea chanjo dhidi ya HPV,” aeleza Prof Mansoor.

Mbali na pingamizi hizi, miezi michache baada ya uzinduzi, janga la Covid 19 likachipuka. Licha ya kuwa bado haijabainika ni vipi maradhi haya yalivyoathiri utoaji wa chanjo ya HPV, ukweli ni kwamba sekta nyingi za afya zilipuuzwa, huku asilimia kubwa ya rasilimali zikielekezewa vita dhidi ya corona.

Aidha, tangu uzinduzi wa chanjo nchini, serikali imekuwa ikigaharimia chanjo hii kwa wasichana wa umri wa miaka kumi. Swali ni je, itakuwaje kwa wale ambao wamepitisha umri huu katika kipindi hiki cha janga la corona?

Katika vituo binafsi vya kiafya, chanjo hii inatolewa kwa kati ya Sh3, 000 na Sh5, 000. Je, ni wangapi walio tayari kutoa pesa hizi ili mabinti zao wapokee chanjo hii?

Je, huenda hii ikaathiri vita dhidi ya kansa ya lango la uzazi? Tayari kuna wasiwasi kuhusu kiwango cha upokeaji chanjo hii.

Katika mkutano wa Zoom ulioandaliwa mapema mwezi huu ili kutathmini maafikio katika vita dhidi ya kansa hii, ilibainika kwamba Kenya ingali nyuma katika jitihada za kutoa chanjo dhidi ya HPV. Kwa mfano, wakati wa uzinduzi, shabaha ilikuwa kufikia asilimia 75 ya wasichana, ilhali kufikia sasa ni asilimia 36 pekee ambao wamechanjwa.

Mwanafunzi wa umri wa miaka 10 katika shule ya msingi ya Ossen, Kaunti ya Baringo akipokea chanjo ya HPV pindi baada ya mpango wa utoaji chanjo hiyo kuzinduliwa 2019. PICHA | FLORAH KOECH

Je, huenda hii ikawa na matokeo duni katika vita dhidi ya virusi hivi na matatizo ya kiafya vinavyosababisha?

Kulingana na Dkt Mansoor kuna baadhi ya matatizo ya kiafya yanayotokana na virusi vya HPV kama vile vidutu vya sehemu nyeti (genital warts), na aina mbalimbali za kansa kama vile ya tupu ya nyuma, uume, uke, na sehemu ya nyuma ya koo (oropharyngeal).

“Miongoni mwa zaidi ya aina 100 za virusi vya HPV, angalau 14, husababisha kansa, na aina mbili (16 na18) zinasababisha asilimia 70% ya visa vya kansa,” asema.

Kansa ya lango la uzazi miongoni mwa wanawake ndilo tatizo ambalo limethibitishwa kukithiri sana kutokana na virusi hivi.

Kwa mujibu wa WHO, asilimia 99.7 ya kansa zote za lango la uzazi husababishwa na maambukizi ya HPV. Hapa nchini, HPV inaongoza kwa kusababisha kansa ya lango la uzazi miongoni mwa wanawake kati ya miaka 15 na 44.

Kwa wale ambao huenda hawaelewi taswira kamili ya kansa hii, maradhi haya yanaongoza kwa kusababisha vifo vinavyotokana na kansa nchini Kenya, huku takriban visa 5,250 vipya vikiripotiwa kila mwaka.

Ukanda wa Afrika Mashariki ndio umebeba mzigo mkubwa zaidi wa kansa hii ulimwenguni. Duniani, wanawake 311,365 hufariki kila mwaka kutokana na ugonjwa huu.

Kansa hii ikitambulika katika awamu ya kwanza (Stage 1), uwezekano wa kuishi baada ya kutibiwa ni asilimia 90, na yakitambulika katika awamu ya tatu (stage 3), uwezekano wa mgonjwa kuishi na baada ya matibabu ni asilimia 50 pekee.

Isitoshe, matibabu yaweza gharimu kati ya Sh 300,000 na Sh500, 000.

Ili kuangamiza kansa ya lango la uzazi, WHO linapendekeza asilimia 90 ya wasichana chini ya umri wa miaka 15 wachanjwe kufikia mwaka wa 2030.

Kulingana na Prof Mansoor, takriban visa vyote vya kansa hii vyaweza zuiwa kupitia chanjo na hivyo kuokoa maisha ya takriban wanawake 3,000 nchini kila mwaka.

“Chanjo salama na thabiti dhidi ya virusi vya HPV yaweza zuia kwa asilimia 90 visa vya kansa ya lango la uzazi,” aongeza.

You can share this post!

Mvuvi afariki Lamu mawimbi makali yakiendelea kuyumbisha...

MUME KIGONGO: Makapera hatarini kuugua moyo, wanasema...

T L