• Nairobi
  • Last Updated April 17th, 2024 6:55 PM
MUME KIGONGO: Makapera hatarini kuugua moyo, wanasema wataalamu

MUME KIGONGO: Makapera hatarini kuugua moyo, wanasema wataalamu

NA LEONARD ONYANGO

MWANAUME anayeishi maisha ya ukapera baada ya kutalikiana na mkewe au kuachwa na wapenzi yuko katika hatari kubwa ya kusumbuliwa na magonjwa hatari kama vile maradhi ya moyo.

Wataalamu wanasema kuwa wanaume huathirika zaidi kiafya uhusiano wa kimapenzi na mwanamke unapofikia tamati ikilinganishwa na wanawake.

Afya hudorora zaidi iwapo ataachwa na wanawake zaidi ya wawili, kwa mujibu wa watafiti.

Utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Copenhagen nchini Denmark, na ripoti yake kuchapishwa katika jarida la Journal of Epidemiology and Community Health hivi majuzi, ulibaini kuwa wanaume wanaokaa kwa muda mrefu bila kuwa na wapenzi kufuatia kuvunjika kwa mahusiano ya awali, pia wanakuwa katika hatari ya kupatwa na msongo wa akili, kusahau mambo kwa urahisi (dementia) na kudorora kwa kingamwili (immunity).

Utafiti huo ulifanywa miongoni mwa watu 4,835 ndani ya miaka 26, ulibaini kuwa wanawake hawaathiriki kiafya wanapokaa pekee yao kwa muda mrefu baada ya kuachwa au talaka.

Utafiti huu unajiri huku visa vya vijana kujitoa uhai au kuuana kutokana na mizozo ya uhusiano wa kimapenzi vikiongezeka nchini.

Wataalamu wanasema kuwa ndoa, haswa miongoni mwa vijana zimekuwa zikivunjika baada ya muda mfupi kwa sababu wahusika wanakimbilia kuoana bila kuchumbiana au kupata ushauri nasaha.

Baadhi ya wanandoa kwa mujibu wa wataalamu, wanapendelea kunyamaziana wanapokosana badala ya kuzungumzia tatizo lililopo na kuelewana.

Mitandao ya kijamii pia imelaumiwa kwa kuchochea wanandoa kuwa na ‘mipango ya kando’ hivyo kutia ndoa au uhusiano wa kimapenzi hatarini.

You can share this post!

Harakati za utoaji chanjo ya HPV nchini zasuasua

Ushirikiano wa Mudavadi, Ruto waibua tumbojoto huku...

T L