• Nairobi
  • Last Updated April 15th, 2024 2:58 PM
Ursula von der Leyen aahidi Afrika sapoti ya Ulaya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi

Ursula von der Leyen aahidi Afrika sapoti ya Ulaya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi

HELLEN SHIKANDA Na MARY WANGARI

RAIS wa Kamisheni ya Umoja wa Ulaya (EU), Ursula von der Leyen akihutubu kwenye Kongamano Kuu la Afrika la Kuangazia Mabadiliko ya Tabianchi amesema anafurahishwa na hatua ya Kenya kuanza kutekeleza Sheria ya Kenya kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi, 2023.

Rais William Ruto alitia saini mswada wa sheria hiyo Ijumaa wiki jana.

Sheria hiyo inatia zingatio kwa masoko ya kaboni, ambayo yanatoa fursa kubwa kwa nchi za Afrika kutumia vizuri hifadhi kubwa ya rasilimali.

“Leo hii ninasikiliza yale yanayojadiliwa kwenye hili kongamano kuu, lakini pia ninatoa hakikisho kwamba Ulaya imejitolea kuwa mshirika mkuu wa Afrika tunapoelekea kwa Kongamano la Mabadiliko ya Tabianchi la COP28,” amesema Von der Leyen.

Amesema rasilimali za Afrika, ikiwemo nishati jadidifu na gesi ya haidrojeni, ni muhimu katika kuleta kwa suluhu kwa changamoto zinazoletwa na mabadiliko ya tabianchi.

Ushirikiano, amesema Von der Leyen, ni muhimu kwa sababu unailetea Afrika faida na dunia kwa ujumla.

“Bara la Afrika lina uwezo wa kuzalisha gesi jadidifu ya kutosha kutumika na mataifa ya bara hilo na hata kuiuza ng’ambo,” akasema.

Amesema kwamba ni muhimu kuweka mabadiliko kwenye mifumo ya ufadhili wa benki.

Jinsi benki za kimataifa zinavyohatarisha Afrika kwa kufadhili sekta hatari

Baadhi ya benki zinalaumiwa kwa kufadhili miradi inayotatiza harakati za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Benki hizo huchochea athari za uchafuzi wa mazingira badala ya kufadhili mikakati ya kudhibiti mabadiliko ya tabianchi, utafiti mpya umesema.

Utafiti mpya uliofanywa na shirika la kimataifa la ActionAid umefichua jinsi mashirika ya kifedha kutoka Magharibi yamekuwa yakimimina mabilioni kufadhili sekta za nishati chafu na kilimo cha viwanda, zinazochangia zaidi katika uchafuzi wa mazingira.

Taasisi kuu za kifedha zimekuwa zikitoa mabilioni kufadhili visababishi vya mabadiliko ya tabia nchi na kupuuza suluhisho za kudhibiti janga hilo, ilisema ripoti iliyotolewa na Jopokazi la Kimataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (IPCC).

Wataalam wameonya kuwa mataifa ya Afrika ambayo tayari yamelemewa na makali ya mabadiliko ya tabianchi yanazidi kushuhudia kuongezeka kwa miradi inayohusu nishati chafu na kilimo cha viwanda.

Miradi hiyo ni pamoja na uchimbaji wa madini, visima vya gesi, mabomba ya mafuta, viwanda vinavyoendeshwa kwa makaa na kilimo cha viwanda kinachohusisha mazao yanayokuzwa kwa kutumia mbolea na dawa za kuua wadudu zilizochimbwa.

Matokeo yake yamekuwa mapigano ya kung’ang’ania ardhi na maji, maafa, mazingira kuzorota, uchafuzi wa mito na maziwa na kuchochea athari za mabadiliko ya tabianchi ambazo tayari zinahangaisha wanajamii.

Benki na mashirika yanayoongoza kwa kufadhili nishati chafu na kilimobiashara katika mataifa ya Afrika ni pamoja na Barclays, HSBC, BNP Paribas, Société Générale kutoka Uropa.

Citigroup, JPMorgan, Chase na Benki ya Amerika  (kutoka Amerika) pamoja na Benki ya Viwanda na Biashara China, China CITIC Bank, Benki ya China  na  Mitsubishi UFJ Financial (kutoka Bara Asia) ni miongoni mwa mashirika ya kifedha yaliyotawa katika ripoti hiyo.

Utafiti huo unakadiria kuwa kiwango cha ufadhili uliotolewa na mashirika hayo ya kifedha barani Afrika kilifikia Sh466.6 trilioni katika muda wa miaka saba tangu Mkataba wa Paris kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi ulipoidhinishwa.

Katika kipindi hicho vilevile, ufadhili uliotolewa kwa kwa kampuni kubwa zaidi zinazojihusisha na kilimo cha viwanda barani Afrika ulifikia Sh54 trilioni.

Kwa jumla, kiasi cha fedha kilichotolewa na benki hizo kufadhili miradi ya kawi chafu na kilimo katika nchi zinazoendelea ni mara ishirini zaidi kushinda kiasi kilichotolewa na mataifa ya ulaya kufadhili nchi zilizoathiriwa zaidi na janga la uchafuzi wa mazingira.

“Idadi kubwa ya benki hizi zimeahidi katika nakala zao za kifedha kufikisha “sufuri” kiwango cha hewa sumu kufikia 2050 lakini hakuna hata moja imeweka mikakati ya dhati ya kukomesha uharibifu wa mazingira,” ilisema ripoti hiyo.

“Benki kadhaa (ikiwemo Barclays, BNP Paribas, HSBC na Citigroup) sasa zina malengo ya muda mrefu ya kukomesha ukopaji wa makaa lakini zimeendelea kufadhili baadhi ya mashirika makuu yanayoongoza kwa uchimbaji makaa na madini. Benki kuu zinafadhili mashirika yanayohusishwa na miradi tata inayohatarisha jamii na mazingira katika maeneo husika.”

Isitoshe, utafiti huo umefichua kwamba miongoni mwa benki hizo “hakuna yoyote iliyo na sera ya kuzima ufadhili wa mafuta na gesi hata ingawa hatua hii ni muhimu iwapo ufadhili wao wa kifedha utaambatana na shabaha ya kuhifadhi mazingira kwa kupunguza viwango vya joto.

Badala yake, sekta zizo hizo hizo za mafuta na gesi ndizo zilizo mstari wa mbele kupokea ufadhilui kutoka kwa benki hizo.

  • Tags

You can share this post!

Nimeolewa mke wa pili lakini mume hanidekezi hata

Tabianchi: Rais Ruto asema wakati wa vitendo ni sasa

T L