• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 5:15 PM
Mkahawa wapokeza wateja mafunzo ya bure kuhusu uhifadhi wa mazingira

Mkahawa wapokeza wateja mafunzo ya bure kuhusu uhifadhi wa mazingira

NA KALUME KAZUNGU

MARA nyingi utapata wadau kutoka sekta mbalimbali wakikaribishwa na mashirika mbalimbali ya kiserikali na yale ya kibinafsi kwenye makongamano ili kupokezwa mafunzo kuhusu masuala ya mazingira na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Makongamano kama hayo huwa mara nyingi yamefadhiliwa kwa gharama ya juu ya fedha ilmradi watu wapate kuhamasishwa kuhusiana na masuala yanayofungamana na mazingira, iwe ni ya baharini, misitu, au nchi kavu.

Aidha katika Kaunti ya Lamu, kuna mkahawa mmoja ambapo wateja wanaozuru pale wamekuwa wakinufaika pakubwa na mafunzo ya bure kuhusu mazingira na elimu inayofungamana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Mkahawa huo kwa jina Kitangani Beach and Restaurant unapatikana Mokowe, eneobunge la Lamu Magharibi.

Mkahawa wa Kitangani Beach and Restaurant uko katika eneo la Mokowe, Lamu Magharibi. Wasimamizi wa mkahawa huo wana programu spesheli ya kuelimisha wateja kuhusu utunzi wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi kupitia mfumo wa moja kwa moja au mabango kwenye miti na sehemu nyingine. PICHA | KALUME KAZUNGU

Ni mkahawa ambao uko mkabala na Bahari Hindi lakini mandhari ya mkahawa wenyewe yakisheheni miti, hasa mikoko.

Upande wa Bahari Hindi, utawaona samaki wanaorukaruka wakifurahia mazingira ya baharini.

Wateja ambao wamekuwa wakizuru pale wamefurahia kupokezwa hamasisho muhimu kuhusu mazingira na mabadiliko ya tabianchi, iwe ni kupitia njia ya moja kwa moja au mabango yaliyotundikwa kila upande yenye maandishi ya kuonya au kuelimisha waja kuhusu umuhimu wa mazingira na namna ya kuyatunza.

Utapata michoro na maandhishi yakiwa yameandikwa kwenye kisiki cha mti wa mkoko yenye ujumbe kama ‘The Ocean is Where Trees/Mangroves Belong’ ama ‘Kwenye Miti/Misitu Usiku Ni Raha’.

Kisiki cha mti wa mkoko kikiwa kimeandikwa maandishi kuhusu mazingira. PICHA | KALUME KAZUNGU

Haya yote ni katika harakati za kumweka mja katika taswira ya jinsi maisha yanavyoboreka wakati mazingira ya Baharini, Misitu na mengineyo yakitunzwa ipasavyo.

Meneja wa mkahawa wa Kitangani Beach and Restaurant, Bw Fredrick Mwaganje aliambia Taifa Leo kuwa waliafikia kuanzisha mkahawa huo kama njia mojawapo ya kupiga vita uharibifu wa mazingira, japo kwa njia mbadala.

Bw Mwaganje alisema wengi wanaozuru mkahawa huo wamekuwa wakiridhishwa na mpangilio uliopo, hasa kihuduma kwani mbali na kupata mapokezi murua na mapochopocho ya kila aina, wateja haohao huondoka wakiwa wakwasi wa elimu kuhusu utunzi wa mazingira.

“Kwanza hapa huwa tunawapokea wageni na kuwatembeza kwenye uwanja wetu, wakitazama mikoko iliyozingira eneo hili. Hapo huwa wanapata fursa ya kusoma mabango tuliyotundika ambayo yote yamesheheni ujumbe wa umuhimu wa kutunza na kuhifadhi mazingira yetu,” akasema Bw Mwaganje.

Anaongeza kwamba ukumbini, pia huwa wana wahudumu ambao kila mara huwa tayari kuzungumza na wateja kuhusu masuala yanayofungamana na mazingira.

Mkahawa wa Kitangani Beach and Restaurant uko katika eneo la Mokowe, Lamu Magharibi. Wasimamizi wa mkahawa huo wana programu spesheli ya kuelimisha wateja kuhusu utunzi wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi kupitia mfumo wa moja kwa moja au mabango kwenye miti na sehemu nyingine. PICHA | KALUME KAZUNGU

“Pia tuko na kanda maalumu zenye ujumbe huo huo, ambapo wateja hutazama na kusikiliza mafundisho kuhusu mazingira na athari za mabadiliko ya tabianchi na namna ya kukabili hali hiyo huku wakisubiri kupakuliwa mapochopocho na kujituliza kwenye vibaraza vyetu,” akaeleza Bw Mwaganje.

Katika Mkahawa wa Kitangani, wateja pia hupata fursa ya kuingia ufukweni na hata kutembezwa kwa mashua baharini kutazama kila aina ya samaki na hata kuvua samaki hao ili wafurahie kitoweo freshi.

Ni kutokana na upekee wa hoteli hiyo ambapo hivi karibuni imeibuka kupendwa, hasa na mashirika yanayohifadhi mazingira, ikiwemo lile la Huduma za Misitu nchini (KFS), ambapo makongamano mengi ya kujadili masuala ya mazingira yamekuwa yakifanyika mkahawani hapo.

Mwenyekiti wa Wakataji na Watunzaji Mikoko, Kaunti ya Lamu, Abdulrahman Aboud ni miongoni mwa wateja kindakindaki wa mkahawa wa Kitangani Beach and Restaurant.

Katika mahojiano na Taifa Leo, Bw Aboud aliwasifu waanzilishi wa mkahawa huo, akisema juhudi zao zimesaidia pakubwa katika kuwapokeza wananchi, wageni na watalii hamasa na elimu kuhusu utunzi wa mazingira na masuala mengine mengi yanayotekelezwa kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

Bw Aboud aliwasihi wawekezaji zaidi kuja Lamu na kuanzisha miradi kama hiyo ili kusaidia kutunza mazingira nchini.

“Nafurahia kila nikizuru hapa Kitangani Beach and Restaurant. Huu mkahawa umewekwa mahali pazuri ambapo awali palikuwa pakishuhudia uharibifu mkubwa wa mikoko na uchafuzi wa bahari. Tangu hoteli hii kuanzishwa twaona visa vya uharibifu wa mazingira vimepungua,” akasema Bw Aboud.

Afisa huyo aidha aliisihi serikali ya kaunti na ile ya kitaifa kusaidia vijana walioanzisha mkahawa wa Kitangani Beach and Restaurant kuepuka kuhangaishwa na mabwanyenye ambao wamekuwa wakinyemelea eneo hilo kulinyakua.

“Najua kuna baadhi ya mabwanyenye ambao tayari wako mbioni kupiga vita hawa vijana wetu walioanzisha mkahawa wa Kitangani Beach and Restaurant. Wanataka ardhi wainyakue. Serikali ya kaunti na ile ya kitaifa zisaidie hawa vijana wasipokonywe hii ardhi. Wanatekeleza wajibu muhimu na lazima waheshimiwe,” akasema Bw Aboud.

Mbali na mkahawa wa Kitangani Beach and Restaurant kutekeleza jukumu hilo la kufunza wateja umuhimu wa kuhifadhi mazingira na kuepuka uchafuzi na uharibifu, hali hiyo hiyo pia imekuwa ikiendelezwa eneo la Mkokoni, Lamu Mashariki, ambapo makundi ya akina mama pia yamekuwa yakitunza mazingira kupitia njia mbadala.

Sehemu mojawapo ya mkahawa wa Kitangani Beach and Restaurant iliyokaribiana na Bahari Hindi. PICHA | KALUME KAZUNGU

Miongoni mwa njia hizo ni kutenga siku maalumu ya kuenda ufukweni na ndani ya bahari kuokota taka, hasa zile za plastiki, kuzikusanya mahali pamoja ili kuepuka athari za uchafu huo kumezwa na samaki ambao huishia kufariki.

Isitoshe, akina mama hao hao pia wamekuwa wakijenga vibanda na vibaraza vya kupunga hewa kwenye fuo wakitumia chupa za plastiki na taka nyingine ilmradi wanaotembelea maeneo hayo wajipatie mafunzo kuhusu athari za uchafuzi wa mazingira na kukabiliana na mfumko wa mabadiliko ya tabia nchi.

Katika eneo la Shella, kisiwani Lamu, wanaharakati wa mazingira na wadau wa utalii pia wamekuwa wakitumia njia mbadala kutunza mazingira ya Bahari Hindi, ikiwemo kuweka mifuko maalumu ya kuhifadhia taka za plastiki na nyinginezo kwa wageni, watalii na wenyeji wanaozuru fukwe hizo kujivinjari.

Mabango yanayotundikwa kwenye fuo nyingi za Bahari Hindi, Kaunti ya Lamu pia yamekuwa yakitumika kupitisha jumbe hizo.

  • Tags

You can share this post!

UDA yasubiri kuvuna kutokana na ‘vita vya panzi’ ndani...

SHINA LA UHAI: Hofu maambukizi ya TB yakiongezeka miongoni...

T L