• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 6:50 AM
Ukosefu wa sehemu maalum za kuuzia kuku wachosha wafanyabiashara

Ukosefu wa sehemu maalum za kuuzia kuku wachosha wafanyabiashara

Na SAMMY WAWERU

RUTH Wanjiru amekuwa katika ufugaji wa kuku halisi wa kienyeji na walioimarishwa, kwa muda wa miaka mitatu.

Aliingilia ufugaji-biashara huo 2018, baada ya kuhangaika kwa muda wa miaka mitano akitafuta kazi ya kozi aliyosomea.

Wanjiru, 36, ana Stashahada ya Masuala ya Huduma za Mikahawa na Usimamizi.

Kulingana na masimulizi, ilimgharimu mtaji wa Sh100, 000 kuingilia ufugaji wa kuku.

“Nilianza na vifaranga, na kwa jumla ya 150 ni nusu yake pekee walifanikiwa,” mfugaji huyu adokeza, akikadiria hasara.

Licha ya pigo hilo, Wanjiru anasisitiza kwamba hakukata tamaa.

Ruth Wanjiru hufuga kuku wa kienyeji eneo la Githunguri, Kaunti ya Kiambu. PICHA | SAMMY WAWERU

Mfugaji huyu anayeendeleza shughuli hiyo eneo la Githunguri, Kaunti ya Kiambu, ni kati ya waliofanikisha miradi ya kuku nchini.

Hufuga kuku maridadi wa nyama na mayai ya kienyeji, na pia huuza vifaranga.

Kwa sasa akiwa na kuku wapatao 300, Wanjiru anasema haijakuwa rahisi kuimarisha mradi wake.

Masoko Kenya kukosa kujali wafugaji wa kuku

Anataja kupenyeza soko, kama mojawapo ya changamoto kuu.

“Kumekuwa na kuku wengi na mayai kutoka nchi jirani wa bei ya chini, hivyo basi kuathiri wafugaji wa ndani kwa ndani Kenya,” analalamika.

Kulingana na Wanjiru, masoko mengi nchini hayana sehemu maalum ya wafanyabiashara na wafugaji wa kuku.

“Ukizuru masoko ya Kiambu na Nairobi, hayana eneo la kuuzia kuku,” asema, akihimiza serikali na wadauhusika katika sekta ya ufugaji kutathmini wazo hilo.

Licha ya serikali kudai imeweka mikakati kabambe kuzindua vichinjio vya kuku, wafanyabiashara na wafugaji wamejenga vizimba tamba kandokando mwa barabara.

“Maafisa wa halmashauri ya jiji hawatupi nafasi kuendeleza biashara ya kuuza kuku na kuchinja,” Wanjiru akaambia Taifa Leo wakati wa mahojiano, akilalamikia kisa ambapo alitozwa ada ya Sh100 kwa kila kuku kuwaingiza sokoni.

Changamoto nyingine, ni kuendelea kupanda kwa bei ya chakula cha mifugo.

Chakula cha kuku kuwa ghali

Lishe ya kuku ndiyo imeathirika pakubwa, chini ya kipindi cha muda wa miezi mitatu iliyopita mambo yakizidi unga.

“Watengenezaji wa chakula cha mifugo wanahoji bei ya malighafi imekuwa ghali. Lishe ya kuku imeathirika pakubwa kwa ongezeko la bei, baadhi ya wafugaji wakiacha kuwafuga,” anadokeza David Njoroge, mmiliki wa Grada Farmers Ltd, duka la kuuza malisho na bidhaa za mifugo lililoko Ruiru, Kaunti ya Kiambu.

Kulingana na mhudumu huyu, amepoteza karibu asilimia 30 ya wateja wafugaji wa kuku, waliositisha miradi yao.

Mfuko wa kilo 70 wa chakula uliokuwa ukiuzwa kati ya Sh2,200 – 2,400 sasa ni zaidi ya Sh2,700.

Kwa wafugaji kama Wanjiru waliokuwa wakijitengezea lishe kupunguza gharama, kwa sasa imekuwa vigumu kwa sababu malighafi yamekuwa ghali, ongezeko la hivi majuzi la bei ya mafuta ya petroli likichangia mfumko.

You can share this post!

Gavana ataka haki kwa mashindano ya utamaduni

JUMA NAMLOLA: Wanasiasa wa Kenya waige De Klerk katika...

T L