• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 6:50 AM
Owalo awataka wabunge kubadilisha sheria na sera za sekta ya ICT ili kuzima shughuli haramu

Owalo awataka wabunge kubadilisha sheria na sera za sekta ya ICT ili kuzima shughuli haramu

NA CHARLES WASONGA

WAZIRI wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) na Uchumi wa Kidijitali Eliud Owalo amesema kampuni ya Worldcoin ilifaulu kuendesha shughuli zake ‘haramu’ nchini kutokana na mapungufu ya kisera na kisheria yaliyopo nchini.

Bw Owalo mnamo Jumatatu, Septemba 9, 2023, aliiambia kamati ya muda ya Bunge inayochunguza shughuli za kampuni ya asili ya Amerika kwamba shughuli zake za ukusanyaji data ziligunduliwa mwaka mmoja baada ya kampuni hiyo kuanza kuwasajili Wakenya.

“Ni jambo lililotushangaza kuwa japo Worldcoin ilianza kukusanya data kutoka kwa umma nchini Kenya mnamo Mei 2021, Afisa ya Kamishna wa Kulinda Data (ODPC) iligundua shughuli hizo mnamo Aprili 2022. Asasi nyingine za serikali ziliweza kufahamu kwamba Wordcoin imekuwa ikisajili Wakenya baadaye mwishoni mwa mwezi Julai 2023. Hii ni baada ya Wakenya kujitokeza kwa wingi katika ukumbi wa KICC ili data zao zichukuliwe,” Bw Owalo akaambia Kamati hiyo ya muda inayoongozwa na Mbunge wa Narok Magharibi Gabriel Tongoyo.

Waziri wa ICT na Uchumi wa Kidijitali Eliud Owalo alipofika mbele ya Kamati ya Muda ya Bunge inayochunguza sakata ya Worldcoin katika County Hall, Nairobi mnamo Septemba 11, 2023. PICHA | CHARLES WASONGA

Waziri alisema hana habari ikiwa uchunguzi wowote ulifanywa kabla ya kampuni washirika wa Worldcoin – Tools For Humanity (ya Amerika) na Tools For Humanity (ya Ujerumani) – kupewa leseni ya ODPC ili ziendeshe shughuli za ukusanyaji data kutoka kwa Wakenya.

“Sheria ya Kulinda Data ya 2019 imepungukiwa katika suala hili la kufanyika kwa uchunguzi wa kina kabla ya kampuni za data kusajiliwa nchini. Ipo haja kwa nyie kama wabunge kuifanyia marekebisho sheria hii na kanuni nyingine husika ili kuziba mianya iliyopo,” Bw Owalo akasema.

“Aidha, sheria zote zilizoko katika sekta ya teknolojia ya habari na mawasiliano na uchumi wa kidijitali kwa ujumla zinahitaji kufanyiwa marekebisho ili ziandamane na teknolojia mpya zinazoibuka kama vile teknolojia ya kuiga akili ya mwanadamu (Artificial Intelligence-AI) na sarafu za kidijitali kama vile cryptocurrency,” waziri akaongeza.

Bw Owalo alisema ni kutokana na hitaji hilo la mabadiliko kufanywa katika sera na sheria za sekta hiyo ambapo ameteua jopokazi la wataalamu 42 ambao watafanya uchunguzi na kisha kupendekeza mabadiliko kama hayo.

  • Tags

You can share this post!

Mume wangu na meidi wanatumiana SMS za siri

Wakimbizi wanavyofaulu kuvuna donge jijini licha ya...

T L