• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 6:07 PM
ZARAA: Uzito na utamu wa matikitimaji anayokuza umempatia soko imara

ZARAA: Uzito na utamu wa matikitimaji anayokuza umempatia soko imara

NA PETER CHANGTOEK

WILSON Baya amekuwa akishughulikia ukuzaji wa mitikiti kwa muda wa miaka saba sasa.

Alianza kwa kulitumia shamba ekari moja, lakini kwa wakati huu, hulitumia shamba la ekari saba.

Mkulima huyo anasema kuwa, kuna mambo kadha wa kadha, ambayo amekuwa akiyatekeleza au kuzingatia, ambayo yamemwezesha kupata hela nyingi kutoka kwa mmea huo.

Baya, anayekiendesha kilimo hicho katika eneo la Garashi, Masindeni, Kaunti ya Kilifi, huzitumia mbolea asilia, mathalan; samadi ya ng’ombe, jambo ambalo limemwezesha kuchuma matikitimaji yaliyo na uzani wa juu, ambapo huyachuma matunda yenye uzani wa hadi kilo 12.

“Wakati wa kwanza nilianza kwa ekari moja, nikafaulu na sasa ninakuza kwa ekari saba,” asema mkulima huyo.

Anafichua kuwa, alipokuwa akijitosa katika ukuzaji wa mitikiti kwa mara ya kwanza, aliutumia mtaji wa Sh70,000.

Baya, ambaye hulitumia shamba la familia yake, anadokeza kuwa alizinunua mbegu kutoka kwa duka la pembejeo za kilimo la Coast Farmers, mjini Malindi.

“Wakati tulipokuwa tukianza, kilo moja ilikuwa ikiuzwa kwa Sh4,600,” adokeza, akiongeza kuwa alipanda mbegu nusu kilo.

Anafichua kuwa, alianza kwa kukuza mitikiti aina ya Maridadi. Hata hivyo, kwa wakati huu, yeye hukuza aina mbili — Maridadi na Sukari F1.

Mkulima huyo anasema kwamba, aina hizo za mitikiti anazokuza huchukua muda wa siku 78 baada ya kupandwa ili izae matunda yawe tayari kuchumwa.

Amechimba kisima shambani, ambacho hukitumia kuyatoa maji anayoyatumia kunyunyizia kwa mimea yake.

“Ninatumia pampu kunyunyizia maji,” aongeza Baya.

Kwa mujibu wa Baya ni kwamba, anaweza kutumia Sh100,000 kuyazalisha matikitimaji kwa shamba ekari moja. Fedha hizo ni za kulitayarisha shamba, kuzinunua mbegu, mbolea, dawa na nguvukazi.

Anasema kuwa, kwa shamba ekari moja, ana uwezo wa kubaki na Sh500,000, baada ya kuondoa gharama ya uzalishaji.

Kwa wakati huu, huuza kilo moja ya tikitimaji kwa Sh40. Anaongeza kuwa, tikitimaji linaweza kuwa na kilo 7 hadi kilo 9.

“Tikitimaji kubwa zaidi kwa shamba langu huwa na kilo 12,” afichua Baya, akiongeza kuwa, siri ya kuyazalisha matunda yenye uzani kubwa zaidi ni kuzitumia mbolea asilia na aina ya D.A.P.

Kabla hajazipanda mbegu, yeye huliandaa shamba vizuri kwa kutumia trekta. Baada ya kulima, hutengeneza mitaro kwa kuacha nafasi ya mita mbili kutoka kwa mtaro mmoja hadi kwa mwingine.

Kisha, humwaga mbolea asilia katika mitaro hiyo kabla hajazipanda mbegu.

Hata hivyo, kuna changamoto kadhaa ambazo amezipitia katika uzalishaji wa matikitimaji, mathalan; magonjwa na wadudu waharibifu, hususan wale wanaotoboa matunda.

Ili kuzuia wadudu kutoboa matikitimaji, mkulima huyo anasema ananuia kutumia mifuko fulani, ambapo atayaweka matunda ndani. Ili kuzuia baadhi ya magonjwa, yeye hupanda mahindi baada ya kuchuma matikitimaji.

Changamoto nyingine ambayo mkulima huyo amepitia ni kutumia petroli nyingi kuendesha mtambo wa kusukuma maji shambani, hasa wakati wa kiangazi.

Mkulima huyo ana wafanyakazi watatu, anaosema aliwaajiri kwa kuzingatia sheria za leba, na wawili ambao huwalipa kila wiki.

“Soko liko hapa Malindi, pale Gongoni. Magarini pia kuna soko,” asema mkulima huyo, akiongeza kuwa, huwapata wateja wengine pia, kutoka Mtwapa na Kongowea, ambao huenda shambani kwake kuyanunua matikitimaji.

Baya anadokeza kuwa, katika siku za usoni, Mungu akimjaalia, ana mipango ya kutengeneza juisi ya matikitimaji na kuuza.

You can share this post!

Uhuru akuza wanasiasa kizazi kipya Mlimani

Kithi apuuza madai alihusika na ufisadi

T L