• Nairobi
  • Last Updated March 5th, 2024 12:43 PM
Alia warembo humkwepa wakidai hawakumbatii

Alia warembo humkwepa wakidai hawakumbatii

MWANGI MUIRURI NA MERCY KOSKEI

HAIKUWA mapenzi ya James Irungu mkazi wa Maragua, Kaunti ya Muranga kuzaliwa bila mkono mmoja miaka 48 iliyopita, kwani hali hii imemsababisha kukosa mke kuoa.

Irungu analalamika kuwa licha ya kuoa mara mbili amebaki bila mke, baada ya wake wake kutoweka japo muda tofauti, huku akisema kuwa angependa kuwa na mpenzi kando yake uzeeni.

“Kukua kwangu haikuwa ngumu kwani nilikuwa natumia mkono wangu wa kulia kwa kazi zangu za kila siku ikiwa ni pamoja na kuandika shuleni. Kila kitu kilikuwa shwari licha ya unyanyapaa, nilipewa jina la utani ‘goko (mkono mdogo)’ na wenzangu kutokana na hali hii,” alisema.

Kulingana na Irungu, baada ya kumaliza shule ya msingi alijiunga na shule ya Upili ya Ichagaki.

Alijizolea C- lakini hakuweza kujiunga na chuo kikuu.

“Matumaini yangu yalikuwa kujiunga na chuo kikuu na kupata ujuzi ili hapo baadaye niajiriwe au nifungue biashara yangu. Lakini hilo halikuwekezana kutokana na umaskini nyumbani na ulemavu kwa upande mwingine, nikajikuta sina popote pa kwenda,” alisema.

Irungu alisema kuwa alikuwa akitegemea mamake kwa mahitaji yake yote, lakini alianza kupatwa na aibu alivyozidi kuwa mkubwa na kuamua kuondoka nyumbani ili akabiliane na maisha.

Anasema kuwa alikopa Sh1, 000 na kufunga safari akaelekea Gikomba, Nairobi ambapo alianza kuishi na rafiki wa familia.

“Nia yangu ilikuwa kuanza kununua viatu vya mitumba na kuviuza katika maeneo ya Eastlands. Biashara ilinikubali kwa vile wengi walinunua kama tendo la uhuruma kwa sababu ya ulemavu wangu. Nilichukua ulemavu wangu kama nguvu ya biashara yangu,” alisimulia.

Mnamo wa 2004, Irungu alijitafutia mke na pia kuanzisha biashara ya ufugaji kuku na nguruwe ili kumudu familia yake.

Lakini hatua hii ikawa chanzo cha dhiki kwake kwani hakupata mke mwenye bidii na mwaminifu, kwa kile anataja kama kuanza kujihusisha na uhalifu na kujitosa kwenye biashara haramu ya uuzaji chang’aa na bangi.

Alibaini kuwa mkewe angeishia kukamatwa mara kwa mara na alipofikishwa mahakamani alilazimika kutoa faini iliyomfanya kufilisika na kuharibu biashara zake.

Irungu alikiri kuwa alianza kubugia vileo ili apunguze msongo wa mawazo.

Wanandoa hao walibarikiwa na mtoto wao wa kwanza 2005, lakini Irungu alishindwa kumudu gharama ya familia yake kutokana na ukosefu wa kazi.

“Bila ujuzi, kazi zinazopatikana kijijini ni duni. Sikuweza kuchimba, kufanya kazi katika maeneo ya ujenzi au kufanya kazi kwenye baa, hoteli au bucha. Pia sikuwa na uwezo kunyanyua vyuma au kuwa dereva.” alikumbuka.

Alisikitika kuwa mkewe alimwacha 2008, kupitia kwa ujumbe wa kejeli “nenda ujipatie mkono ambao utafanya unishike kama mwanamume halisi na pia utakaokusaidia kumudu familia yetu”.

Ujumbe huu ulimchoma moyo, japo hakukata tamaa na kutafuta mke wa pili 2012 lakini hali ya umaskini ilisababisha mfarakano kati yao na mwanamke huyo kutoroka.

Baada ya shida kuwa nyingi, Irungu alisema kuwa alijihusisha na biashara ya magendo ili kujikimu ila tishio la kufungwa jela lilimfanya aachane na tabia za kihuni.

Maisha ya Irungu yalibadilika baada ya kujiunga na chama cha watu wenye ulemavu Maragua mwaka wa 2015.

Anasema kuwa hatua hii ilimsaidia sana kwani alianza kuona dhamani katika maisha yake, hata ingawa alikuwa na ulemavu baada ya kuelezwa kuwa atajifunza ujuzi ambao hauhitaji matumizi ya mikono yote miwili.

Anasema kuwa alijifunza ukulima na kujua jinsi ya kupandikiza miche (grafting) ambapo anapata Sh30 kwa kila kipandikizi.

Kulingana naye, chama kilikuwa kimeamua kumtafutia ‘mkono bandia’ japo hali yake kiafya isingemruhusu.

Serikali ya kaunti pia imemsajili kama msambazaji bidhaa na iwapo atapata zabuni hiyo kama mtu binafsi, kampuni au kama chama cha ushirika, atajumuishwa kwa mgao wa asilimia 30 uliotengewa wenye ulemavu.

Anasema kwa sasa amejijenga uwezo kiakili kukabiliana na mapenzi, baada ya matatizo yake awlai kwenye ndoa na sasa yuko mbioni kujitosa katika maisha.

  • Tags

You can share this post!

Seneta Madzayo ajutia uamuzi wake wa kuacha kazi ya...

Mke na mume wachimba shimo ndani ya ‘bedroom’ kuficha...

T L