• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 7:05 PM
Asimulia alivyonusurika kifo kwenye ajali mbaya ya barabara kwa tundu la sindano wenzake wakiaga  

Asimulia alivyonusurika kifo kwenye ajali mbaya ya barabara kwa tundu la sindano wenzake wakiaga  

NA MERCY KOSKEI

JUNI 1, 2013 Simon Mwangi aliabiri matatu na wenzake saa kumi na mbili za jioni kurejea Naivasha, baada ya kuhudhuria warsha mjini Nakuru.

Safari yao ilianza vizuri huku dereva akihimiza kila mtu kufunga mkanda wa usalama na hata abiria mmoja akajitolea kuombea safari hiyo.

Hata hivyo, walipofika Kikopey, katika barabara kuu ya Nakuru-Nairobi, matatu waliyokuwa wakisafiria ilihusika katika ajali mbaya baada ya kugongana na trela.

Akikumbuka ajali hiyo iliyogharimu maisha ya marafiki zake wawili, Mwangi anasema kuwa trela hiyo iliyokuwa ikielekea Nakuru ilipoteza mwelekeo baada ya breki zake kufeli na kugongana na matatu.

Anakumbuka masaibu hayo ya miaka kumi iliyopita wakati wa siku ya kuwakumbuka waathiriwa wa ajali ya barabarani, iliyofanyika katika shamba la Delamere Kaunti Ndogo ya Naivasha, Bw Mwangi anasema matatu yao ilibingiria mara saba.

Katika hafla hiyo ya ukumbusho, Mwangi alisema waliokolewa na wasamaria wema waliowakimbiza katika Hospitali ya St. Mary’s Gilgil.

Hospitalini alielezwa na madakatari kuwa alivunjika fupa la kiuno (Hip fracture).

Baada ya miezi kadhaa ya kutibiwa bila kupata nafuu, alifanyiwa upasuaji na fupa hilo likatolewa.

Bw Mwangi alisema kuwa kwa sasa anatumia fupa bandia.

“Licha ya kwamba nimesimama hapa, nilihusika kwa ajali na ni bahati nilirusurika kifo. Kinachouma moyo zaidi ni kupoteza marafiki zangu. Bosi wangu aligharamia matibabu na hata kusaidia familia yangu wakati huo,” alikumbuka.

Bw Mwangi alikuwa miongoni mwa manusura wa ajali hiyo waliokusanyika kwa minajili ya sherehe hiyo.

Kulingana na ripoti ya Mamlaka ya Usalama Barabarani ya (NTSA), imefichua kuwa kufikia Oktoba 2, 2023 imeandikisha vifo 330 vilivyotokana na ajali za barabarani ikilinganishwa na mwaka wa 2022 ambapo vifo 361 viliandikishwa.

Kulingana na ripoti hiyo, kulikuwa na upungufu wa asilimia 8.59 ya vifo.

Mwaka 2023, jumla ya majeraha mabaya 730 yalirekodiwa huku majeruhi kidogo ikiwa 499.

Mwaka 2022 waliojeruhiwa vibaya walikuwa 903 na majeraha kidogo 647.

Mwaka jana, 2022 jumla ya ajali 3, 936 zilirekodiwa kufikia Oktoba ikilinganishwa na mwaka huu ambapo hadi sasa ajali 3,609 zimeandikshwa.

Kaunti za Nairobi na Nakuru ndizo zilizoongoza kwa kusajili vifo 39 na 35 mtawalia.

Maandamano ya amani ya kuwakumbuka waathiriwa wa ajali ya barabarani iliyofanyika Dalamere Kaunti Ndogo ya Naivasha 2013. PICHA|MERCY KOSKEI

Kaunti za Elgeyo Marakwet, Garissa, Lamu, Mandera, Nandi, Taita Taveta na Tana River ziliandikisha kisa kimoja cha maafa ya ajali barabarani.

Kaunti zinazoongoza kwa vifo vya wapita njia mwaka huu, 2023, ni Kaunti ya Nairobi ikiwa na zaidi ya watu 21, Kiambu vifo 17 na Nakuru vifo 12.

Katika ripoti hiyo ya NTSA, Kaunti ya Nakuru inaongoza kwa vifo vya madereva idadi ikisimamia 6 kupoteza maisha yao ikifuatiwa na Kaunti ya Kiambu 3 na Makueni ikiandikisha vifo 3.

Ilibaini kuwa ajali mbaya za trafiki hutokea kati ya saa kumi na moja jioni na saa tatu usiku, kilele kikiwa saa mbili usiku.

Kulingana na Mkurugenzi Mkuu wa NTSA Bw George Njao, watazindua kampeni Desemba 2023 kwa muda wa siku sitini, inayolenga kutoa ufahamu kuhusu usalama barabarani kabla ya msimu wa Krismasi.

Alitoa wito kwa madereva kujiepusha kuvuka mito au barabara zilizofurika ili kukwepa maaafa, hasa kipindi hiki maeneo mengi ya nchi yanaendelea kushuhudia El-Neno.

“Tunashuhudia mvua kubwa nchini, ukiwa dereva tunakusihi uwajibikie maisha ya watu unaosafirisha, sote tuwe makini,” akashauri afisa huyo.

  • Tags

You can share this post!

Wauzaji mafuta Busia walaumu shughuli za unyonyaji mafuta...

Wahuni waliokuwa wakikeketa wasichana Pokot Magharibi...

T L