• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 9:55 AM
Karen Nyamu: Ruto ndiye ameumia zaidi na kupanda kwa bei ya mafuta na anapambana kurekebisha hali

Karen Nyamu: Ruto ndiye ameumia zaidi na kupanda kwa bei ya mafuta na anapambana kurekebisha hali

NA WANGU KANURI

SENETA maalum Karen Nyamu amemtetea Rais William Ruto baada ya kukiuka ahadi yake ya kushukisha bei ya mafuta.

Kwenye ujumbe wake Bi Nyamu, Rais Ruto ndiye anaumia zaidi na kupanda kwa bei ya mafuta na ‘anapambana’ sana kurekebisha hali hiyo.

Akiandika kwenye ukurasa wake wa X, Seneta Nyamu aliandika, “Bei ya mafuta imefikia kilele maeneo tofauti ya dunia. Najua hali hii si nzuri haswa kwa sababu itaathiri gharama ya maisha na pia ni ishara mbaya ya uchumi. Lakini hakuna mtu ameumizwa sana na hali hii kama rais wetu ambaye anafanya kila awezalo kutuondoa katika hali hii.”

Wiki jana, Mamlaka ya Kusimamia Sekta ya Kawi na Petroli (EPRA) ilitangaza nyongeza ya bei ya mafuta huku petroli ikipanda kwa Sh16.9 kwa lita, dizeli kwa Sh21.31 na mafuta taa yakipaa kwa Sh33.22 kwa lita.

Bei hii mpya ilipandisha petroli kuwa Sh211.64 kwa lita jijini Nairobi huku dizeli ikiuzwa kwa Sh200.9 kwa lita na mafuta taa kwa Sh202.6 kwa lita kuanzia Septemba 15 usiku wa manane kama ilivyotangazwa Septemba 14.

Nyongeza hii imewafanya madereva kuongeza nauli kwa waabiri wao huku vuta nikuvute ikisheheni kati ya serikali na upinzani. Licha ya Rais Ruto kuahidi kupunguza gharama ya maisha na bei ya mafuta, mrengo wa upinzani ukimsuta kwa kuwadanganya Wakenya.

Isitoshe, Wakenya wenyewe waliwakashifu viongozi wa Kenya Kwanza ambao hawakutumia tasfida katika matamshi yao kuhusu ongezeko la bei ya mafuta huku wakimvutia Naibu Rais Rigathi Gachagua.

Bw Gachagua aliwaonya dhidi ya ‘kutania’ hali za Wakenya ilhali wao ndio waajiri wao hata ingawa hakuwataja majina. Hali kadhalika, madereva mjini Namanga waliendesha magari yao kwenye vituo vya mafuta vya taifa jirani la Tanzania huku bei ghali za bidhaa hiyo zikishika kasi kote nchini.

Upelelezi wa Taifa Dijitali ulifichua kuwa lita moja ya petroli inauzwa kwa Sh184.18 huku dizeli ikiuzwa kwa Sh186.76. Hivyo basi, Wakenya waendeshaji magari  wataokoa jumla ya Sh27.46 kwa kila lita moja ya petroli na Sh14.23 kwa dizeli.

  • Tags

You can share this post!

Penzi la mubaba tamu nashindwa kumuacha

Kimya kirefu cha Uhuru chazua maswali

T L