• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 3:12 PM
KIKOLEZO: Grammys zimebaki stori tu!

KIKOLEZO: Grammys zimebaki stori tu!

Na SINDA MATIKO

MAKALA ya 2022 ya utoaji tuzo stahiki za muziki duniani, Grammys yaliyoratibiwa kufanyika mwishoni mwa mwezi huu, yameahirishwa kutokana na ongezeko la virusi vya Covid-19.

Kama ilivyo Oscars kwenye tasnia ya filamu, ndivyo ilivyo Grammys katika ulimwengu wa muziki.

Mpaka sasa yameandaliwa makala 63. Lakini kama tu zilivyo Oscars, tuzo za Grammys hazijawahi kukosa skendo. Mojawapo ya skendo hizo ni uwepo wa mastaa wakubwa waliofanikiwa kupata uteuzi wa kutosha kwenye uwaniaji wa tuzo hizo, ila hawajawahi kushinda hata moja.

Baadhi ya mastaa hao walishafifia ila kunao bado wanatisha lakini Grammys wamebaki kuzisikia tu.

Leo tunaichambua sampuli hii ya mastaa wanaozidi kupepea kwenye gemu lakini kwenye Grammys ni kiza tupu!

SNOOP DOGG

Teuzi: 16

Rapa huyu mkongwe kashinda tuzo zote zilizopo kwenye muziki wa Hip-hop isipokuwa Grammys.

Licha ya kutawala gemu toka enzi za Notorius B.I.G na Tupac Shakur, jamaa bado yupo akiendelea kuachia muziki mzuri.

Anajiamini vya kutosha na ndio sababu mwaka juzi alipochukua tuzo ya Hall of Fame, aliamua kujishukuru kwa juhudi na bidii zake kwenye mafanikio yake.

Rapa Snoop Dogg. PICHA | MAKTABA

Utakuwa unaikumbuka ile kauli yake iliyotrendi.. .’I wanna thank me for believing in me…’

Kwenye tuzo za mwaka 2021, alipata uteuzi mmoja katika kipengele cha albamu bora ya Reggae. Hakuwahi kitu. Uteuzi wake wa kwanza wa Grammys ulikuwa 1993, bado anasubiri.

NICKI MINAJ

Teuzi: 10

Rapa Minaj amedumu kwenye gemu kwa zaidi ya miaka 10 sasa. Nyingi za kazi zake zimeishia kuwa hiti. Toka alipoanza muziki, hajawahi kusita kuachia madini ya maana.

Harakati zake hizo zimempelekea kuteuliwa mara kumi kuwania tuzo za Grammys katika vipengele tofauti. Uteuzi wake wa kwanza ulikuwa 2011 kupitia albamu zake ya Pink Friday na The Pink Print.

Hata hivyo msupa mpaka leo bado anasubiri kuiwahi tuzo yake ya kwanza wakati mastaa wa levo kama yake kama vile Beyonce wakiwa na zaidi ya Grammys 20.

KATY PERRY

Teuzi: 13

Perry kaachia hiti za kutosha katika kipindi cha zaidi ya miaka 10. Ana hiti tisa zilizokamata nambari moja kwenye chati za Billboard. Juzi kati tu, aliachia mzigo mwingine When I’m Gone ambao tayari umepata mapokezi mazuri ukiwa na zaidi ya ‘views’ milioni mbili.

Licha ya kazi zake kuvutia utazamaji wa mabilioni, bado hajawahi kuangukia tuzo ya Grammys toka alipopata uteuzi wake wa kwanza 2009 kupitia ngoma yake ya I Kissed a Girl.

Septemba 2021 alipoulizwa mtazamo wake kuhusu hili, alitupa dongo.

“Kusema kweli, haijalishi, ninachojali mimi ni data muziki wangu umeweza kufanikisha. Data hizo hazidanganyi na nimeridhika katika hilo, mengine sijisumbui,” akajibu.

SIA

Teuzi: 9

Nyota huyu kutoka Australia alijitengenezea ushabiki na umaarufu mkubwa sio kutokana tu na muziki wake mnene ambao bado anaendelea kuachia, lakini pia kwa staili yake ya kuficha uso wake.

Ukitizama nyingi video zake, utagundua kuwa haonekani na kama akionekana, anakuwa kaficha uso.

Sia amefanya kazi na wasanii wote wakubwa unaowafikiria.

Pia ameachia albamu tisa nzito toka alipoanza muziki 1990 akiwa mwanachama wa bendi moja kabla ya kujitenga na kuenda solo.

Baadhi ya mashabiki wake wanahisi Grammys ina mapendeleo sababu muziki wake ni mnene usio pingika au kukatalika.

BUSTA RHYMES

Teuzi: 12

Kuna nyakati jamaa alikuwa anasumbua sana na michano yake ya kasi. Rhymes amejisifia mara kadhaa kuwa hamna rapa mwenye uwezo wa kuchana kwa kasi kama yeye.

Ingawaje miaka ya sasa hajaonyesha kufanya muziki kwa fujo kama zamani, bado yupo sana kwenye gemu.

Aliteuliwa mara ya kwanza kuwania tuzo za Grammys 1996. Uteuzi wake wa mwisho aliupata 2011 kwenye vipengele vya Best Rap Perfomance na Best Rap Song.

Tuzo zote kwenye vipengele hivyo alipita navyo Kanye West.

BLAKE SHELTON

Teuzi: 8

Ndiye aliyekutungia hiti ya God’s Country. Nguli huyu wa muziki wa Country, bado anaendelea kufanya vizuri tu katika fani yake.Umaarufu na ushabiki wake upo pale pale.

Mume huyu wa staa Gwen Stefani, kateuliwa mara nane lakini zote zimemtokea puani. Uteuzi wake wa mwisho ulikuwa kwenye makala ya 62 ambayo wengi waliamini angeshinda kipengele cha Best Country Solo Perfomance kupitia hiti yake God’s Country. Tuzo hiyo ikamponyoka na kumwendea Willie Nelson.

You can share this post!

Menengai Oilers yafanya mabadiliko 9 ikivizia Homeboyz

Mainstream Academy balaa taji la Dago Super Cup

T L