• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 6:07 PM
TAHARIRI: Ushirikiano unahitajika mno katika elimu 2022

TAHARIRI: Ushirikiano unahitajika mno katika elimu 2022

Na MHARIRI

KALENDA ya Elimu mwaka huu wa 2022 ina shughuli nyingi ambazo zitahitaji mchango wa pamoja wa wadau wote.

Ni mwaka ambao mitihani minne itafanywa, mihula ikiwa mifupi na hivyo kuwatwika walimu na wazazi mzigo mzito zaidi.

Hili ni jukumu linalohitaji ushirikiano wa karibu sana wa serikali kama mdau mkuu katika sekta ya elimu. Waziri wa elimu ametoa maagizo kwa walimu wakuu wasiwafukuze wanafunzi ambao wazazi wao watashindwa kulipa karo.

Pia, ameonya walimu wakuu dhidi ya kuwatoza wazazi ada zaidi ya karo iliyowekwa na wizara ya elimu. Huu ni mwelekeo mzuri ambao utasaidia iwapo wizara itahakikisha umetekelezwa. Hii ni kwa sababu mara nyingi wizara haifuatilii maagizo inayotoa na kuwaacha wazazi wakiteseka katika mikono ya wakuu wakaidi.

Ukiwa mwaka ambao mtaala mpya wa elimu unaozingatia umilisi na uwezo wa mwanafunzi unaingia awamu muhimu ya gredi ya sita, serikali inafaa kufuatilia kuhakikisha kuwa kila kitu kinaenda sawa.

Elimu ni sekta muhimu kwa nchi ambayo haiwezi kuachiwa upande mmoja kuifanikisha, na hivyo basi, wadau wote wanafaa kushikana mikono kwa kuwa inaweka msingi wa hali ya baadaye ya nchi. Ushirikiano huu, utahakikisha uwepo wa usawa.

Walimu wasiwalemee wazazi, nao wazazi wawasaidie walimu kushughulikia wanafunzi na kwa kufanya hivi, visiki vinavyotatiza usawa katika elimu vitaondolewa.

Ushirikiano wa wadau katika elimu utafanikisha mtaala, kupalilia nidhamu katika wanafunzi na kuepuka visa vya utovu wa nidhamu vinavyosababisha hasara katika shule hasa za sekondari nchini.

You can share this post!

MIKIMBIO YA SIASA: OKA ni mnara mpya wa Babeli uchaguzi...

Malawi kutegemea idadi kubwa ya wanasoka wa ligi yao ya...

T L