• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 8:55 PM
Wapinzani wa Ruto hawatambomoa mashinani kirahisi

Wapinzani wa Ruto hawatambomoa mashinani kirahisi

Na BENSON MATHEKA

WAPINZANI wa Naibu Rais William Ruto kwenye uchaguzi mkuu wa 2022 wana kibarua kingumu kubomoa mtandao aliojenga kote nchini na ambao umempata umaarufu mkubwa hasa viongoni mwa vijana.

Dkt Ruto amepenya katika kila eneo nchini kupitia kampeni yake ya kuinua vijana kiuchumi ambayo amekuwa akiendeleza tangu 2018 alipotofautiana na Rais Kenyatta kufuatia handisheki yake na Bw Odinga.

Ingawa wapinzani wake akiwemo Bw Odinga, vinara wa One Kenya Alliance na washirika wao wamekuwa wakimfananisha na mwanariadha anayekimbia peke yake, wadadisi wa siasa wanasema kwamba huenda ikawa vigumu kwao kubomoa umaarufu ambao amejijengea kupitia kampeni zake za kujisawiri kama mwokozi wa walalahoi.

“ Kuna uwezekano mkubwa kwamba washindani wake wataungana dhidi yake. Japo wakiungana wanaweza kumpa ushindani mkali katika safari ya kumrithi Rais Kenyatta, watakuwa na kibarua cha kung’oa mizizi ambayo amekita kote nchini miongoni mwa vijana,” asema mdadisi wa siasa George Wainaina.

“Ni kweli alianza mbio zake na mapema na kujijengea umaarufu hasa miongoni mwa vijana ambao ndio wengi wasio na ajira. Anaweza kuwa anawahadaa kama wanavyofanya wanasiasa lakini umaarufu wake sio wa kupuuzwa,” akafafanua.

Ripoti ambazo hazikuweza kuthibitishwa zilisema kwamba Rais Kenyatta aliwafichulia vinara wa OKA katika mkutano wa kuwapatanisha na Bw Odinga kwamba utafiti wa shirika la ujasusi la Kenya ulionyesha wanaweza kumshinda Dkt Ruto wakiungana nyuma ya waziri mkuu huyo wa zamani.

Kulingana na Wainaina, hata wakiungana itabidi wabuni mfumo madhubuti wa kampeni sio tu kubomboa himaya ya Dkt Ruto ya hasla, bali kwa kuonyesha wapigakura mfumo badala wa kuimarisha maisha yao.

“Awali walijaribu kulemaza kampeni ya hasla wakimlaumu Dkt Ruto kwa kuchochea vita vya matabaka nchini lakini hawakufaulu kisha wakanyamaza huku akiendelea kuiimarisha na leo imekuwa kama wimbo katika vijiji vyote kote nchini. Hiki sio kitu cha kupuuzwa,” aeleza Wainaina.

Wadadisi wanasema kwamba mbinu ambazo Dkt Ruto na washirika wake wamekuwa wakitumia zinalandana na mahitaji ya wapigakura masikini ambao wamelemewa na gharama ya maisha tofauti na za wapinzani wake wanaotumia maneno makavu bila vitendo.

“Kwa kufanya hivi, amefaulu kupenyeza umaarufu wake katika ngome za wapinzani wake. Anaonekana kuwa na mpango mzuri wa kampeni, ana nguvu na huwa amepanga hotuba zake vyema. Hatapatapi anapowasilisha ujumbe wake na pia amejisawiri kama kiongozi mkarimu kuliko wapinzani wake. Hii, kwa wakati huu, imemfanya kipenzi cha wapigakura wengi wakiwemo vijana na wanawake ambao amekuwa akilenga,” asema mchanganuzi wa siasa Deborah Akinyi.

Dkt Ruto pia amepenya katika makanisa ambako amekuwa akichanga pesa kwa wingi na kuendeleza kampeni yake.

Kwa sasa hakuna mgombea urais anayeweza kufananishwa naye akiwa amefanya mikutano zaidi ya 300 ya kisiasa ndani ya mwaka mmoja 135 ikiwa ndani ya mwezi mmoja.

“Anawapatia wapinzani wake wakati mngumu sana. Anajua hivyo na ndio sababu amekuwa akiwakejeli kila wakati akiwataka kuteua mgombea urais wa kupambana naye,” asema Akinyi.

Muungano

Hata hivyo, Akinyi anasema kinachoweza kutikisa umaarufu wa Dkt Ruto ni kuungana kwa vigogo wa kisiasa wa vyama tofauti na kuzidisha kasi ya kampeni za pamoja.

“Inasemwa kuwa siasa za Kenya ni telezi na Dkt Ruto hafai kujigamba kana kwamba ashaingia ikulu. Mawimbi yanaweza kuvuma ilivyofanyika 2001 na umaarufu anaofurahia ufutwe ndani ya miezi mitatu,” asema.

Akinyi anasema kwamba kufikia sasa, Dkt Ruto hana mpinzani.

“Atakuwa na wakati rahisi sana iwapo vinara wa OKA hawataungana na Bw Odinga. Atakuwa na mteremko zaidi iwapo vinara wa OKA hawataafikiana kuteua mgombeaji urais wa pamoja kwenye uchaguzi mkuu ujao. Ataweza kuwa na mteremko zaidi vinara wa OKA wakiungana naye au Rais Kenyatta akimuunga mkono. Hata hivyo itakuwa kibarua kwake wakiungana na Bw Odinga kwa baraka za Rais Kenyatta,” aeleza.

You can share this post!

Vyama vidogo kumeza wale watakaobwagwa katika kura za mchujo

Mwamko mpya wanawake Pwani wakilenga ugavana

T L