• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 6:55 PM
Mwamko mpya wanawake Pwani wakilenga ugavana

Mwamko mpya wanawake Pwani wakilenga ugavana

Na PHILIP MUYANGA

KUONGEZEKA kwa idadi ya wanawake katika kinyang’anyiro cha ugavana eneo la Pwani kunaonyesha mabadiliko makubwa ya kisiasa yaashiriayo mwelekeo mpya kuwa wanawake wa ukanda wa Pwani wanazinduka kisiasa.

Hapo awali ilikuwa ni nadra sana kuwapata wanawake wa Pwani wamejitosa katika siasa na hali hii ilibadilika miaka michache iliyopita.

Mwaka wa 2013 na 2017, kulikuwa na mwanamke mmoja pekee aliyejitokeza na kugombania ugavana katika ukanda mzima wa Pwani.

Bi Jacinta Mwatela ndiye aliyekuwa mgombeaji pekee mwanamke aliyegombania kiti cha ugavana ukanda wa Pwani katika chaguzi hizo mbili.

Bi Mwatela ambaye kwa wakati mmoja alikuwa naibu gavana wa Banki Kuu ya Kenya aliwania kiti cha ugavana Kaunti ya Taita Taveta.

WANAWAKE WATANO

Kwa sasa wimbi la mabadiliko limetanda na idadi ya wanawake ambao wamejitosa ulingoni kuwania ugavana imeongezeka hadi watano.

Wanawake waliojitokeza kuwania ugavana wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka ujao ni pamoja na Bi Umra Omar (Lamu), Bi Aisha Jumwa (Kilifi), Bi Fatuma Achani (Kwale), Bi Patience Nyange na Bi Rachel Mwakazi (Taita Taveta).

Kulingana na wachanganuzi wa maswala ya siasa, iwapo wanawake hao watashinda au mmoja kati yao atashinda, basi ushindi huo utakuwa ni badiliko kubwa la kisiasa ikilinganishwa ya kuwa kabla ya katiba ya sasa, idadi ya wanawake waliokuwa kwa siasa eneo nzima la pwani ilikuwa ndogo sana.

“Ushindi wa mwanamke mmoja katika kiti cha ugavana kaunti mojawapo ya pwani utabadilisha mkondo wa siasa za akina mama kwani utachangia kuongezeka kwa idadi ya wawaniaji wa kiti hicho chaguzi nyingine zijazo,” alisema afisa mmoja mwanamke wa shirika moja la kiserikali aliyetaka jina lake libanwe.

Bi Omar anayewania kiti cha ugavana Lamu anasema kuwa ugatuzi umewawezesha wanawake wengi kujitokeza kuwania viti vya ugavana katika ukanda wa Pwani.

Aliongeza kuwa hatua ya uthibitisho (affirmative action) pia imesababisha ongezeko la wanawake kuwania nyadhifa za kisiasa jambo ambalo litaimarisha usawa hususan katika nyanja ya siasa.

“Hapo awali kulikuwa na baadhi ya wanasiasa kwa mfano waliokuwa si wenyeji wa Lamu na wanagombea viti huku,kwa sasa sababu ya ugatuzi jambo hilo haliwezi kufanyika,” alisema Bi Omar.

Aliongeza kusema kuwa idadi ya wanawake kuwania ugavana kuongezeka pia imesabishwa na mabadiliko ya kizazi (generation) kipya ambacho kinaangazia sera.

Bi Omar anatarajia kupigania ugavana wa Lamu na tiketi ya chama cha United Democratic Alliance (UDA) kinachohusishwa na naibu rais William Ruto.

Mwanasiasa huyo aliwahimiza wanawake wenzake kujibidiisha katika siasa na kutokubali kuambiwa ya kuwa hawawezi kuongoza.

NYADHIFA

Mchanganuzi wa maswala ya siasa Bi Naomi Cidi alisema kuwa wakati ni sasa kwa wanawake kutwaa nyadhifa za uongozi zikiwemo zile za ugavana.

“Mwaka ujao sisi kama wanawake tutawaunga mkono wanawake wenzetu wanaowania viti vya ugavana na vinginevyo vya kisiasa hapa pwani na nje ya pwani,” alisema Bi Cidi.

Aliongeza kusema kuwa swala la kuwa mwanamke ni adui ya mwanamke mwenzake halitakuwepo wakati wa uchaguzi ujao na kwamba wanawake watasaidiana kutwaa nyadhifa za siasa.

Bi Cidi aliongeza kusema kuwa ingawa thuluthi tatu ya kijinsia inayohitajika kikatiba haikupitishwa katika bunge la kitaifa, wanawake wengi hawataogopa kujitosa katika uongozi.

Mshauri wa uuzaji wa maswala ya siasa (political marketing consultant) Bw Bozo Jenje alisema kuwa kujitokeza kwa idadi kubwa ya wanawake wanaowania ugavana inahusishwa sana na ugatuzi vile ulivyodhamiriwa na katiba.

JINSIA

Aliongeza kusema kuwa kuangaziwa sana kwa maswala ya usawa wa jinsia pia kumechangia pakubwa kuongezeka kwa idadi ya wanawake wanaogombania ugavana katika ukanda wa pwani.

“Wanawake wengi wameenda kwa warsha nyingi za kuwaelimisha kuhusiana na maswala ya usawa wa jinsia ambazo zimewaongezea maarifa ya uongozi na kuwapa mwelekeo unaohitajika wa maswala mbalimbali yakiwemo siasa na wanasiasa,” alisema Bw Bozo.

Bw Bozo aliongeza kusema kuwa kuogozeka kwa idadi kubwa ya wanawake wanaogombania nyadhifa za ugavana pia ni kwa sababu ya wanawake kutaka kujiimarisha kiuchumi,kisiasa na usimamizi wa raslimali za umma.

Kaunti ya Mombasa na ile ya Tana River ndizo kwa sasa hazina muwaniaje yeyote mwanamke ambaye anagombania ugavana.

Mbunge wa Likoni Mishi Mboko ambaye alikuwa ameazimia kupigiania ugavana wa Mombasa alijiondoa kwa kinyang’anyiro na kusema kuwa angetaka kuhifadhi kiti chake cha ubunge.

“Nitagombania ubunge katika eneobunge la Likoni, ukiwa unaimani ya kuwa nimefanya kazi nzuri na kwamba nikihifadhi kiti changu basi nitafurahi,” alisema Bi Mboko wakati akijiondoa kwa kinyang’anyiro cha ugavana.

Aliwaomba wananchi msaada wao akisema kuwa hawezi kuelekea na safari hiyo ya kuhifadhi kiti chake cha ubunge bila wao.

Magavana wanaong’atuka uongozini baada ya kuhitimisha awamu zao mbili ni Bw Hassan Joho, Salim Mvurya na Amason Kingi wa Mombasa, Kwale na Kilifi mtawalia.

Magavana Granton Samboja, Dhadho Godhana na Fahim Twaha wa Taita Taveta, Tana River na Lamu mtawalia wanatarajiwa kupigania kuhifadhi viti hivyo wanavyoshikilia sasa.

You can share this post!

Wapinzani wa Ruto hawatambomoa mashinani kirahisi

Yanayomsubiri Ruto akifurushwa Jubilee

T L