• Nairobi
  • Last Updated February 26th, 2024 11:20 AM
Jinsi mraibu wa unywaji pombe anavyoweza kujinasua

Jinsi mraibu wa unywaji pombe anavyoweza kujinasua

NA MARGARET MAINA

[email protected]

KUACHA ulevi ni lengo ambalo si rahisi kwa mraibu kuliafikia.

Mraibu anahitaji kujitolea, kujitia moyo, na hata ikiwezekana atafute usaidizi wa kitaalam.

Hatua ya kwanza muhimu katika kushinda ulevi ni kujikubali kwamba una tatizo na pombe. Yaani unafahamu fika kwamba pombe imekuwa tatizo maishani mwako na kwamba unahitaji usaidizi ili kuacha. Kujua huku kunakupa dira kamili na kukupa ufahamu kwamba unafaa kufuata mkondo tofauti maishani.

Baadhi ya viashiria kwamba mtu ni mraibu wa pombe

  • kulewa chakari
  • mtazamo mkali au hamu ya kunywa pombe iliyopitiliza
  • kukosa kutekeleza majukumu kama matokeo ya unywaji pombe
  • kuwa na athari zisizofaa kutokana na unywaji pombe, kama vile matatizo na watu wengine, changamoto za kifedha, au masuala ya kisheria
  • kuendelea kunywa pombe licha ya kufahamu kuwa inaathiri vibaya maisha yako

Ikiwa una mojawapo ya dalili hizi, basi huu ni wakati mwafaka wa kutafuta msaada.

Kumbuka kwamba kukubali tatizo kunaonyesha nguvu na ujasiri badala ya udhaifu. Inachukua ujasiri kukubali unahitaji msaada na kuanza mchakato wa kushinda uraibu.

Kuzungumza na mtaalamu, mshiriki wa kikundi cha usaidizi kama vile Alcoholics Anonymous, rafiki anayeaminika au mwanafamilia kunaweza kuwa na manufaa ikiwa unatatizika kukiri kwamba una tatizo la unywaji pombe. Watu hawa wanaweza kukusaidia na kukuelekeza unapopitia mchakato huu wenye changamoto. Ili kuacha ulevi, ni vyema kutafuta usaidizi ambapo utapewa programu ya matibabu ya kitaalamu, ambayo inaweza kutoa mazingira yaliyopangwa na yenye kutia moyo.

Anzisha mfumo wa usaidizi: Tangamana na watu wa kukuinua, wa kukushauri, na watu wanaofahamu mapambano yako. Huu ni mmojawapo wa mikakati bora zaidi ya kukusaidia kuacha ulevi. Huyu anaweza kuwa rafiki, jamaa, mtaalamu, au mtu kutoka kwa kikundi cha usaidizi.

Tunza hali yako ya kimwili na kiakili: Kuacha ulevi kunahitaji kujitunza vizuri. Huenda hilo likahusisha kutafuta njia zinazofaa za kukabiliana na mfadhaiko, kupata usingizi wa kutosha, kula mlo kamili, na kufanya mazoezi.

Ikiwa unaona kwamba unatatizika kuacha unywaji pombe, ni muhimu kutafuta usaidizi zaidi. Hii inaweza kujumuisha kugundua njia mpya au mbadala za matibabu, kujiunga na mtandao tofauti wa usaidizi, au kuomba usaidizi kutoka kwa mtaalamu.

Kumbuka kwamba kuacha ulevi ni vigumu hivyo ni mchakato unaohitaji uweke jitihada na utie bidii.

  • Tags

You can share this post!

Je, kuna chakula cha kukusaidia usizeeke haraka?

TAHARIRI: Idara za serikali ziwe zinatenga malipo kabla ya...

T L