• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 12:30 PM
JUNGU KUU: Muthama asuka njama mpya dhidi ya Kalonzo

JUNGU KUU: Muthama asuka njama mpya dhidi ya Kalonzo

NA BENSON MATHEKA

VITA vya ubabe kati ya Kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka na Mwenyekiti wa chama cha United Democratic Alliance (UDA) Johnson Muthama vimefufuka tena huku kila mmoja akiwania kuwa msemaji wa jamii ya Wakamba.

Muthama, ambaye alikuwa mshirika wa Bw Musyoka kabla ya kuhama Wiper na kujiunga na UDA cha Rais William Ruto, ameanza mikakati ya kuzima umaarufu wa makamu rais huyo wa zamani.

Bw Musyoka ambaye ni mwanasiasa wa kwanza kuwahi kushikilia wadhifa mkubwa serikali amekuwa akipigwa vita na wapinzani wake, wengi wakiwa washirika wake wa zamani waliojitenga naye wakimlaumu kwa kutotilia maanani maslahi ya jamii.

Kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu, kulikuwa na juhudi za kumpokonya Bw Musyoka wadhifa wa msemaji wa jamii zilizoendeshwa na Bw Muthama, aliyekuwa gavana wa Machakos Dkt Alfred Mutua ambaye kwa sasa ni waziri wa Mashauri ya Kigeni na aliyekuwa gavana wa Makueni Kivutha Kibwana miongoni mwa wengine.

Licha ya kampeni kali dhidi yake, chama cha Wiper kilishinda viti vingi vya ubunge, magavana, maseneta, wawakilishi wa kike na madiwani wengi katika kaunti tatu za ukambani za Kitui, Machakos na Makueni.

Lakini, akionekana kupata nguvu baada ya chama chake cha UDA kuingia mamlakani, Bw Muthama ambaye alibwagwa na Wavinya Ndeti wa chama cha Wiper katika uchaguzi wa ugavana kaunti ya Machakos, ameanza kampeni mpya ya kuyeyusha umaarufu wa Bw Musyoka eneo la Ukambani.

Jumapili iliyopita, Bw Muthama aliandaa mkutano wa viongozi wa vyama tanzu vya muungano tawala wa Kenya Kwanza kuweka mikakati ya kuzima Bw Musyoka na chama chake cha Wiper katika eneo hilo.

Viongozi hao walimtaja Bw Muthama kama mweledi wa kisiasa ambaye uongozi wake wa hekima uliwezesha jamii kuingia katika serikali baada ya kuwa kwenye baridi kwa muongo mmoja chini ya unahodha wa Bw Musyoka.

Licha ya kupata kura 250,000 kutoka eneo la Ukambani, Rais Ruto ameteua mawaziri wawili kutoka jamii ya Wakamba na amependekeza wanne kwa wadhifa wa katibu wa wizara.

Mbali na Dkt Mutua anayetoka kaunti ya Machakos, Waziri wa Utalii Bi Peninah Malonza anatoka kaunti ya Kitui.

Kulingana na Profesa Kivutha Kibwana, ambaye alihudhuria mkutano wa Jumapili iliyopita ulioitishwa na Bw Muthama, wakati umefika kwa jamii kumvua Bw Musyoka wadhifa wa msemaji na kumvika joho hilo Bw Muthama.

“Iwapo wewe ni kiongozi na haufaulu kusaidia jamii yako, basi unafaa kupisha mtu mwingine,” alisema akimaanisha kushindwa kwa Bw Musyoka kuongoza jamii kuingia serikalini tangu 2013.

Duru zinasema Bw Muthama na washirika wake wanalenga kuzima ushawishi wa wabunge wa Wiper kwa kuhakikisha hawatumii shughuli, mipango na miradi ya Kenya Kwanza kumpigia debe Bw Musyoka.

Hata hivyo, wachanganuzi wa siasa eneo la Ukambani wanasema itakuwa mlima kwao kuyeyusha umaarufu wa Bw Musyoka.

“Kwamba Bw Musyoka ana idadi kubwa ya viongozi waliochaguliwa ni kuonyesha watu wanamtambua kama msemaji wao na haitakuwa rahisi kubomoa himaya ya umaarufu ambao amejenga,” alisema Bw Meshack Loki, mdadisi wa siasa.

Anasema kwamba wengi waliohudhuria mkutano wa Bw Muthama ni viongozi walioshindwa kwenye uchaguzi mkuu uliopita.

You can share this post!

JUKWAA WAZI: Gachagua, Mutua walumbana kuhusu...

JAMVI LA SIASA: Sasa ni maisha ya baridi kwa...

T L