• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 5:03 AM
JAMVI LA SIASA: Sasa ni maisha ya baridi kwa ‘mayatima’ wa Uhuru

JAMVI LA SIASA: Sasa ni maisha ya baridi kwa ‘mayatima’ wa Uhuru

NA WANDERI KAMAU

WANASIASA na maafisa wakuu serikalini waliokuwa na ukaribu na Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta, sasa wameanza rasmi maisha mapya kwenye baridi ya kisiasa, baada ya Rais William Ruto kufanya teuzi muhimu za watu watakaomsaidia kuendesha serikali yake.

Tayari, Rais Ruto amemaliza taratibu zote za kisheria kuteua Baraza la Mawaziri, wasimamizi wa Ikulu na makatibu wa wizara.

Katika utawala wa Bw Kenyatta, baadhi ya maafisa walioibukia kuwa wenye ushawishi mkubwa ni aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiang’i, Katibu wa Wizara Karanja Kibicho, mawaziri Peter Munya (Kilimo), Joe Mucheru (Habari, Mawasiliano na Teknolojia), Msimamizi wa Ikulu Kinuthia Mbugua, Naibu Mwenyekiti wa Jubilee David Murathe, Mkuu wa Utumishi wa Umma Joseph Kinyua kati ya wengine.

Hata hivyo, maafisa hao wanatarajiwa kuanza maisha mapya, baada ya Rais Ruto kuanza kubuni “jeshi lake” litakalomsaidia kuendesha serikali yake.

Baadhi ya watu wanaotajwa kuwa na usemi mkubwa katika utawala mpya ni Msaidizi wa Kibinafsi wa Dkt Ruto Farouk Kibet, Mkuu wa Utumishi wa Umma Felix Koskei, Msimamizi Mkuu wa Ikulu Katoo Ole Metito, mawaziri Kithure Kindiki (Usalama wa Ndani), Aden Duale (Ulinzi), Alice Wahome (Maji) na Kipchumba Murkomen (Barabara na Uchukuzi).

Wengine ni Katibu wa Wizara ya Ndani, Dkt Raymond Omollo.Katika Bunge la Kitaifa na Seneti, Rais Ruto pia amebuni makundi ya wabunge watakaokuwa kama “macho na masikio” yake.

‘Majeshi’ hayo pia yanajumuisha Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Kimani Ichung’wa na mwenzake katika Seneti, Aaron Cheruiyot.

Kulingana na wadadisi wa siasa, itawalazimu ‘mayatima’ wa Bw Kenyatta kuanza kubuni mikakati mipya ili kuingiliana na utawala mpya.

“Kwa washirika wa Bw Kenyatta ambao walikuwa wanasiasa, itawalazimu kubuni njia mpya za kujifufua kisiasa au kubuni urafiki na utawala wa sasa,” akasema Bw Oscar Plato, ambaye ni mchanganuzi wa siasa.

Wakati wa utawala wa Bw Kenyatta, Dkt Matiang’i na Bw Kibicho waliibukia kuwa maafisa wa serikali wenye nguvu zaidi na walioaminiwa sana na rais.

Kwa mfano, Dkt Matiang’i alikwezwa na kuwa Msimamizi Mkuu wa Mawaziri, huku Dkt Kibicho akisimamia na kuendesha masuala muhimu ya usalama.

Wakiwa wasomi, inaelezwa wawili hao wanapanga kurejea katika vyuo vikuu kama wahadhiri.

Kabla ya kuteuliwa kama waziri na Bw Kenyatta mnamo 2013, Dkt Matiang’i alikuwa akihudumu kama mhadhiri wa Fasihi katika Chuo Kikuu cha Nairobi.

Naye Dkt Kibicho alikuwa mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Egerton kabla ya kuteuliwa na Rais Mstaafu (marehemu) Mwai Kibaki kama Katibu katika Wizara ya Mashauri ya Kigeni.

Kwenye mahojiano, Bw Munya alisema “hajafahamu mwelekeo atakaochukua” kwani kuna masuala mengi anayoweza kujihusisha nayo.

“Kitaaluma, mimi ni wakili. Nina kampuni yangu ya uwakili. Pia, mimi ni mkulima na mfanyabiashara. Bado sijafanya uamuzi kuhusu njia nitakayofuata,” akasema Bw Munya.

Ijapokuwa washirika wengi wa Bw Kenyatta hawajajitokeza kutangaza rasmi mielekeo yao ya kisiasa na kitaaluma, baadhi wamenukuliwa wakimlaumu kichinichini kwa “kuwashinikiza kufanya maamuzi mabaya ya kisiasa.”

“Ingawa ninamshukuru Bw Kenyatta kwa kunipa nafasi kuhudumu kama waziri, ninahisi alinikosea kwa kunirai kutowania ugavana katika kaunti ninakotoka,” akasema waziri mmoja aliyehudumu katika serikali iliyopita.

Wadadisi wanasema kwa kubuni “jeshi” lake jipya, lengo la Rais Ruto ni kuhakikisha watamsaidia kwa mikakati yote ya kiutawala na kisiasa ielekeapo 2027.

  • Tags

You can share this post!

JUNGU KUU: Muthama asuka njama mpya dhidi ya Kalonzo

TAHARIRI: Upinzani umsukume Rais Ruto kuwajibika

T L