• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 6:24 PM
KIGODA CHA PWANI: Hofu wanawake wakikosa kujitegemea kisiasa Pwani

KIGODA CHA PWANI: Hofu wanawake wakikosa kujitegemea kisiasa Pwani

NA FARHIYA HUSSEIN

KILA mara chaguzi zinapozidi kukaribia, wanawake wengi nchini Kenya huwa wanajitokeza na kujitosa kwenye nyanja tofauti za kisiasa.

Huku wito unapozidi kutolewa kwa wanawake kujitokeza kuwania viti vikubwa vya kisiasa mbali na wadhifa wa Mbunge Mwakilishi wa Kike, idadi kubwa ya wanawake kutoka Pwani bado wamebaki nyuma.

Kwa wale wachache ambao wamejitosa katika siasa, imebainika wengi wangali wanategemea sana umaarufu wa vigogo wa kisiasa wa kiume ili wafanikiwe kupenya ulingoni.

Taswira ya jinsi wanawake wa Pwani wangali nyuma kujisimamia kisiasa ilionekana wiki iliyopita, wakati wanasiasa wa kiume walipojitwika jukumu la kuongoza shamrashamra za siku ya kimataifa ya wanawake katika kaunti tofauti za ukanda huo.

Katika Kaunti ya Mombasa, malumbano yaliibuka baina ya wananchi wanaoaminika kuwa wafuasi wa wanasiasa wanaotaka kuwania ugavana kaunti hiyo katika hafla ya siku ya wanawake.

Wanasiasa wanaotaka ugavana ambao walihudhuria mkutano huo ni Mbunge wa Mvita, Bw Abdulswamad Nassir, Naibu Gavana wa Mombasa, Dkt William Kingi, ambao wanawania tikiti ya Chama cha ODM.

KINGI KILIFI

Katika Kaunti ya Kilifi, hafla iliongozwa na Gavana Amason Kingi ambaye alitumia jukwaa hilo kupigia debe chama chake cha Pamoja African Alliance (PAA).

Hali haikuwa tofauti Kwale, ambapo hafla iliongozwa na kinara mwenza wa Muungano wa Kenya Kwanza, Bw Moses Wetang’ula aliyeandamana na wanasiasa wengine wanaoegemea upande wa Dkt William Ruto, wengi wakiwa ni wanaume.

Fujo zilizoshuhudiwa katika hafla ya Mombasa zilikashifiwa na viongozi na mashirika mbalimbali.

Kulingana na Bi Miraj Abdillahi, ambaye ni mwanasiasa anayelenga kuwania kiti cha Mbunge Mwakilishi wa Kike katika Kaunti ya Mombasa, ukosefu wa fedha ni mojawapo ya sababu kuu ambazo zinasababisha kikwazo kwao kujitegemea.

Kulingana naye, amewahi kujaribu kuanzisha chama cha wanawake lakini hakufua dafu.

“Pamoja na wenzangu tulijaribu kuanzisha chama cha wanawake kuleta mabadiliko lakini tuliangushwa kwa sababu mbalimbali ila sababu kuu ni kwamba, kama wanawake tungekuwa na fedha za kutosha tungejisimamia wenyewe, ila hatuna nguvu ya kumenyana na wanaume,” alisema Bi Abdillahi.

Aliongezea kuwa wengi wao, wanakimbilia nafasi cha kiti cha mwakilishi wa wanawake ili kujitengenezea jina baadaye kuwania viti vya juu kama ugavana au useneta.

“Juzi tulikuwepo katika mkutano wa wanawake wa kisiasa na mmoja wetu akaeleza kuwa alijitoa katika kinyang’anyiro cha kiti cha ugavana kwa sababu hana fedha za kutosha kwani wapinzani wake wote ni wanaume na wana fedha za kutosha kusimamia maswala yote ya kampeni. Hili ni suala ambalo linachangia pakubwa wengi wetu kufuata viongozi wa kiume,” alisema Bi Abdillahi.

Bi Abdillahi ambaye anataka kuwania kiti hicho kupitia Chama cha UDA, hata hivyo alirai wanawake wazingatie kuungana ili waache kutegemea wanasiasa wa kiume.

USHINDANI

Kando na ushindani ambao huwa wanapata kutoka kwa wanaume kisiasa, alizidi kusema kuna baadhi ya wanawake ambao hupendelewa zaidi ya wengine chamani na huishia kupewa tikiti.

Hatari iliyopo ni kuwa, wanaopendelewa huenda wakalazimika kuwa vibaraka wa kisiasa wa vigogo hao wa kiume na hivyo basi hawatatilia maanani hitaji la kuwakilisha maslahi ya wanawake.

“Tusipojipanga basi tutapangwa na hao wanaume. Wengi wetu tunaanguka na kushindwa wakati wa mchujo wa chama kwa sababu wanaosimama nyuma ya wanaume wanapewa nafasi hizo kwa haraka,” alisema Bi Abdillahi.

Bi Hamisa Zaja, ambaye pia anataka kuwania kiti cha Mbunge Mwakilishi wa Kike Mombasa, amelaumu siasa za mirengo kama sababu nyingine inayowarudisha nyuma wanawake kisiasa.

Kulingana naye, wanawake wengi hufuata misimamo ya vyama vyao bila kujali athari zao kwa ustawishaji wa maslahi ya wanawake katika jamii.

“Mwaka wa siasa wa 2013 na 2017 wanawake wengi walijitosa katika siasa mirengo. Lakini mwaka huu tumeona vyama vidogo vingi. Kama vile mimi mwaka huu nawania kupitia chama cha United Green Movement (UGM),” anasema Bi Zaja.

Kulingana naye, vigogo wa kisiasa wa kike kama vile Kiongozi wa Chama cha Narc-Kenya, Bi Martha Karua na mwenzake wa Narc-Kenya, Bi Charity Ngilu wameweza kuwa miongoni wa wanawake waliojisimamia kisiasa kwa vile wamekuwa siasani kwa muda mrefu.

Bi Zaja alisema hiyo inaashiria itachukua muda mrefu zaidi kabla Pwani ipate mwanamke anayefikia kiwango cha wawili hao kisiasa.

“Kama tungelikuwa na rasilimali basi hatungejificha nyuma ya wanasiasa wanaume. Ukiwa kwenye chama hauna sauti unafuata chama kinavyopendelea,” alisema Bi Zaja.

Uchaguzi ujao unatarajiwa kushuhudia idadi kubwa ya wanawake wakiwania kiti cha ugavana katika baadhi ya kaunti za Pwani ikiwemo Lamu, Kilifi, Kwale na Taita Taveta. Hii ni ikilinganishwa na jinsi ilivyokuwa katika chaguzi zilizopita ambapo ilionekana kama kwamba wadhifa huo ni wa madume pekee.

Kinyang’anyiro cha ugavana katika Kaunti ya Mombasa bado hakijavutia mwanamke yeyote kufikia sasa huku pia wachache wakijitokeza kutaka kuwania ubunge.

Mbunge wa Likoni Mishi Mboko akizungumza awali. PICHA | MAKTABA
  • Tags

You can share this post!

Chepng’etich atwaa taji Nagoya Marathon, avuna Sh28.5m

Jinsi pingamizi za wandani wa Rais zilivyowapa wanabodaboda...

T L