• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 12:03 PM
KIGODA CHA PWANI: Kingi atikisa siasa za Kilifi na Mombasa kwa kuhamia chama cha PAA

KIGODA CHA PWANI: Kingi atikisa siasa za Kilifi na Mombasa kwa kuhamia chama cha PAA

KUHAMIA kwa Naibu Gavana wa Mombasa, Dkt William Kingi hadi chama cha Pamoja African Alliance (PAA) kutoka kile cha Orange Democratic Movement (ODM) kumeibua msisimko mkubwa wa kisiasa katika kaunti za Mombasa na Kilifi.

Msisimko huo unaonekana kuegemea chama cha PAA kwani kinaonekana kuwa kinazidi kupata umaarufu kutoka chimbuko lake la Kaunti ya Kilifi na kuenea maeneo mengine ya Pwani.

Kulingana na wachanganuzi wa kisiasa, Dkt Kingi kuhamia chama cha PAA kunaonyesha mwelekeo mpya wa chama hicho. Dkt Kingi anaonekana kuwa mmoja wa wanasiasa wakuu kutoka Pwani ambao wametoka chama cha ODM na kujiunga na PAA, hivyo kukipa chama hicho (cha PAA) umaarufu kwa hatua hiyo.

Hata hivyo, wachaganuzi wa siasa wanasema kuwa mwelekeo huo mpya utakuwa wa manufaa kwa chama hicho iwapo kitajiimarisha na kukita mizizi katika eneo la Pwani kwanza kabla ya kuelekea maeneo mengine nchni.

PAA, ambacho kinahusishwa na Gavana wa Kilifi, Amason Kingi kinasemekana kuwa kimekuwa kikitafuta mwaniaji wa ugavana anayefaa katika Kaunti ya Mombasa na kuhama kwa Dkt Kingi kumeonekana kuwa hatua muhimu kwa chama hicho.

Akiongea hivi majuzi baada ya kuhamia PAA,Dkt Kingi alisema kuwa chama cha ODM kilikuwa na wawaniaji wake kilichowataka.

“Chama cha ODM hakina usawa katika uwanja wa siasa na baadhi ya wawaniaji viti kwa tikiti ya chama hicho wanachukuliwa kama raia wa daraja ya pili,” akasema Dkt Kingi.

Aliongeza kuwa alikuwa mwanachama imara wa ODM lakini alipotaka uwazi katika uchaguzi wa mchujo alipuuzwa.

“Kwa sasa ninaendelea na mikakati ya kugombea kiti cha ugavana (wa Mombasa) kwa tikiti ya chama cha PAA,” akasema Dkt Kingi. Mchanganuzi wa siasa, Prof Hassan Mwakimako anasema kuwa kujiunga kwa Dkt Kingi na PAA kutakuwa na matokeo yanayofaa chama hicho kisiasa.

“Kwa sasa huo ni mwelekeo mzuri kwa chama cha PAA kwa kuwa kitaweka utambulisho na uwepo wa jamii ya Mijikenda katika siasa za Mombasa,” alisema Prof Mwakimako.

Prof Mwakimako ambaye ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Pwani, kilichoko Kaunti ya Kilifi anaongeza kusema kuwa chama cha PAA kumkubali Dkt Kingi ni moja ya mikakati yake ya kuibua hisia za jamii ya Mijikenda za kupata mgombezi wa kiti cha ugavana, Mombasa.

Anasema kuwa Dkt Kingi kujiunga na PAA basi inaashiria kuwa jamii ya Mijikenda itapata fursa ya kukipigia chama hicho kura kwa kuwa mmoja wao anagombea ugavana Mombasa kwani kwa muda mrefu imekuwa ikipewa kiti cha naibu ya ugavana ambacho anasema kuwa hakina ushawishi wowote mkubwa.

“Ni suala ambalo liko wazi kabisa kuwa jamii ya Mijikenda ndiyo kubwa katika Kaunti ya Mombasa,kwa hivyo mmoja wao akiwania kiti cha ugavana basi chama anachotumia kitapata umaarufu,” akasema Prof Mwakimako.

Mhadhiri huyo anaongeza kusema kuwa ni wajibu wa PAA kujiimarisha baada ya kusimamisha mgombeaji ugavana Mombasa ili kuweza kufikia maeneo mengine ya Pwani ikizingatiwa kuwa kwa sasa ni chama kinachochukuliwa kama cha Kilifi.

Mshauri wa masuala ya kisiasa, Bw Bozo Jenje anasema kuwa hatua ya Dkt Kingi kujiunga na PAA na kuwania kiti cha ugavana haiwezi kusemakana kuwa chama hicho ni maarufu.

Bw Jenje anasema kuwa iwapo kungekuwa na wanasiasa wengi wanaotoka vyama vingine na kujiunga na PAA basi ingesemekana kuwa chama hicho kitakuwa maarufu au umaarufu wake umeongezeka.

Anaongeza kuwa kwa kujiunga na PAA,Dkt Kingi alionekana kufungiwa nafasi katika chama alichokuwa ndani yake na ilibidi kutafuta nafasi ya kuwa katika sajili ya tume ya uchaguzi (IEBC) ya wanaowania ugavana Mombasa Agosti 9.

“Vyama vikubwa nchini kutoa tikiti kwa wawaniaji wengine ni kwa sababu ya maslahi yao kwani kuna watu wamewekeza katika vyama hivyo,” akasema Bw Jenje.

Hali hiyo, aliongeza kusema kuwa, ndiyo inayofanya wanachama wengine wanaotaka kuwania viti tofauti kuhama vyama ili kuhakikisha wako katika debe.

Bw Mwakera Mndwamrombo ambaye pia ni mchanganuzi wa siasa anasema kuwa umaarufu wa PAA katika ngazi za kitaifa unatokana na kuwa ni mojawapo ya vyama vilivyo katika muungano wa Azimio la Umoja One Kenya.

Hivyo basi, hatua ya Naibu Gavana wa Mombasa, Dkt Kingi kupata tikiti ya PAA imemweka katika mizani sawa na wagombeaji wengine kutoka muungano huo .

Bw Mdwamrombo anasema kuwa kupitia wanachama kuhama vyama vingine, PAA imefaidika kwa kupata Dkt Kingi ambaye alikuwa anataka tikiti ya chama cha ODM.

“PAA imepeperusha mbawa zake katika kaunti sita za Pwani kutoka ugavana hadi viti vya MCA,kwa hivyo ni chama kinachotafutwa na wanasiasa wengi Pwani.”

Katika mkutano mmoja wa PAA uliofanyika mwaka jana,aliyekuwa mbunge wa Malindi, Bw Lucas Maitha alisema kuwa chama hicho kitasimamisha wawaniaji viti katika nyadhifa zote isipokuwa urais peke yake.

“Lazima tuingie katika uchaguzi ujao kama Wapwani tukiwa katika chama kimoja,” akanukuliwa Bw Maitha wakati wa mkutano huo.

Aliongeza kusema kuwa vyama vingine vinamilikiwa na watu kwa sababu yao ya kisiasa na ndiposa Pwani inafaa kusimama imara na chama cha PAA.

Bw Maitha alisema kuwa vyama walivyokuwa navyo awali havijawatumikia Wapwani ipasavyo ndiposa kuna umuhimu wa chama cha PAA ambacho kitaangazia masuala ya Wapwani.

Wakati huo alisema kuwa PAA itashirikiana na vyama au mirengo ya kisiasa ambayo itakuwa tayari kutimiza malengo ya Wapwani. Kwa sasa,chama cha PAA kinashirikiana na kile cha Jubilee na pia kinaunga mkono mgombea wa urais kwa tikiti ya Azimio la Umoja One Kenya Alliance, Bw Raila Odinga.

You can share this post!

Real Madrid wapepeta Getafe na kufungua pengo la alama 12...

WALIOBOBEA: Parpai aliangusha mbabe, akawa waziri miezi 7 tu

T L