• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
KIGODA CHA PWANI: Uchaguzi mkuu ulivyobadili mkondo wa siasa za Pwani

KIGODA CHA PWANI: Uchaguzi mkuu ulivyobadili mkondo wa siasa za Pwani

NA PHILIP MUYANGA

JE, wananchi wa Pwani wamefaidi kutokana na siasa za ukanda mzima mwaka huu ambao unaelekea kutamatika?

Hili ni swali ambalo watu wengi wanajiuliza ikizingatiwa kuwa huu ulikuwa ni mwaka wa siasa na viongozi wengi wapya wamechaguliwa.

Wachanganuzi wa siasa wanasema kuwa Pwani imefaidi pakubwa hususan kutokana na serikali iliyopo kwa kuwa viongozi wengi hata ambao hawakufaulu wamepewa nyadhifa serikalini.

Kwa mujibu wa mchanganuzi wa masuala ya siasa Bw Ayub Mwangi, Pwani imevuna pakubwa katika serikali ya sasa kwa kuwa viongozi wengi wamepewa nyadhifa mbalimbali.

Hata hivyo, wachanganuzi wanasema kuwa siasa za ukanda wa Pwani huenda zikabadilisha mkondo siku za usoni baada ya viongozi waliochaguliwa kupitia chama cha Orange Democratic Movement (ODM) kuonyesha nia ya kufanya kazi na Rais William Ruto.

Kwa muda mrefu sasa chama cha ODM ndicho kimekuwa kikishinda viti vingi hususan vile vya ugavana na ubunge na kufanya ukanda wa Pwani kuwa ngome yake kuu.

“Pwani imekuwa ngome ya ODM kwa muda mrefu lakini hilo huenda litabadilika,” asema Bw Mwangi.

Mchambuzi wa masuala ya siasa wa chuo kikuu kimoja hapa nchini ambaye alitaka jina lake libanwe alisema kuwa suala la umoja wa wanasiasa wa Pwani haliwezi kutekelezwa kwa kuwa hakuna kiongozi anayewashikilia Wapwani kama maeneo mengine.

“Ili kupatikana umoja wa Pwani ni sharti kuwepo kiongozi mmoja kama vile marehemu Karisa Maitha na marehemu Shariff Nassir ambao walisikika katika masuala ya ukanda mzima wa Pwani,” alisema mhadhiri huyo.

Aliongeza kuwa kwa sasa suala hilo litabaki kuwa vivywani mwa wanasiasa tu kwani pia nao hawahusishi wananchi katika kutafuta mwelekeo wa uongozi na umoja wa Wapwani.

“Itakuwa vigumu sana kwa wanasiasa kwa sasa kuwashawishi wananchi na kuwaambia kuna umuhimu wa kuwa na umoja wa Wapwani, suala hilo limepitwa na wakati kwa sasa,” alisema mhadhiri huyo.

Kwa baadhi ya wakazi wa Pwani, ile siku wanasiasa wataungana na kuwa kitu kimoja na kutoa mweleko wa maendeleo ya ukanda wa Pwani,basi wananchi wataweza kufaidi kimaendeleo.

Kwa mujibu wa mchanganuzi mwingine wa siasa Dkt Daniel Mwaringa, Pwani imefaidika sana hususan katika bunge la Afrika Mashariki.

Dkt Mwaringa asema kuwa kwa sasa Pwani imeimarika kwa kiwango kikubwa kutokana na nyadhifa zilizotolewa.

Kulingana na mchanganuzi wa siasa za Pwani Bw Abdulrahman Abdalla, wabunge na viongozi wa kaunti wanafaa wajitokeze na kuwaelezea wananchi ni miradi gani wanayonuia kuitekeleza katika kipindi chao.

Bw Abdalla asema kuwa wakati wa kampeni, viongozi walitoa ahadi chungu nzima ndiposa inafaa waanze kuzitekeleza mapema na kuonyesha ari ya kuwafanyia kazi wananchi.

“Hata iwapo ni mradi mmoja kwa mwaka, ni vizuri wabunge na viongozi wawaambie wananchi,” alisema Bw Abdalla ambaye pia alikuwa mwasiasa kupitia chama cha Kanu miaka iliyopita.

Kwa mujibu wa Bw Abdalla, kiti cha ubunge cha Uwakilishi wa Wanawake kwa sasa kinafaa kuangaziwa kwani wananchi wengi hawajui majukumu ya wadhifa huo licha ya kuwa afisi ya kisiasa kama zile nyingine.

Kwa baadhi ya wachanganuzi wa siasa, kuteuliwa kwa Bw Salim Mvurya na Bi Aisha Jumwa katika baraza la mawaziri katika serikali ya Dkt William Ruto kunamaanisha kuwa wawili hao ndio watakaopeperusha bendera ya serikali katika ukanda wa Pwani.

Kwa muda mrefu ukanda wa Pwani umekuwa na waziri mmoja pekee katika baraza la mawaziri, Bw Najib Balala, na kuteuliwa kwa wawili hao ambao pia ni wanasiasa kulizua msisimko wa jinsi siasa za ukanda wa Pwani zitakavyochukua mkondo mpya.

Swali ambalo wananchi wengi wa ukanda wa Pwani walijiuliza mwaka huu ni iwapo kuteuliwa kwa Bw Mvurya na Bi Jumwa ni kwa sababu ya kuunga mkono Dkt Ruto kuwa rais licha ya kuwa maeneo mengi ya ukanda wa Pwani ni ngome ya chama cha Orange Democratic Movement (ODM)?

Wengi walijiuliza iwapo kuteuliwa kwa Bw Mvurya na Bi Jumwa, waliokuwa gavana wa Kwale na mbuge wa Malindi mtawalia, katika baraza hilo la mawaziri kutawaweka katika nafasi ya juu ya ushawishi wa kisiasa katika siasa za ukanda wa Pwani?

Haya ni baadhi tu ya maswali ambayo yalikuwa vinywani mwa wakazi wengi wa kaunti sita za Pwani mwaka huu 2022 ikitiliwa maanani kuwa hakuna kinara au kiongozi anayesemekana kuwa na ushawishi wa kisiasa wakati huu kama ilivyokuwa nyakati za marehemu Shariff Nassir na marehemu Karisa Maitha ambao walikuwa vigogo wa siasa za Pwani.

Baadhi ya wachanganuzi wanasema kuwa kuteuliwa kwa Bw Mvurya na Bi Jumwa katika baraza la mawaziri kunatokana na hatua yao kumuunga mkono kwa dhati Dkt Ruto kuwa rais wa tano.

Wanaongeza kuwa ingawa viongozi hao hawatajihusisha na siasa moja kwa moja kutokana na majukumu yao ya uwaziri, kuteuliwa kwao kumewapa ushawishi mkubwa katika siasa za ukanda wa Pwani kwa kuwa wanatarajiwa kuwa ‘macho na masikio ya serikali’ Pwani nzima.

  • Tags

You can share this post!

SOKOMOKO: Wivu wa mapenzi huenda utamvua Nyamu useneta

Waliovamia wanahabari wamulikwa

T L