• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 9:50 AM
Kinaya Kenya Kwanza ikipeana ardhi ya chuo licha ya kumponda Uhuru awali

Kinaya Kenya Kwanza ikipeana ardhi ya chuo licha ya kumponda Uhuru awali

NA WANDERI KAMAU

HISIA kali zimeibuka nchini kufuatia hatua ya serikali ya Kenya Kwanza kutoa Sh741 milioni na ekari 30 za ardhi kwa Shirika la Afya Duniani (WHO), kubuni Kituo cha Kikanda cha Kushughulikia Masuala ya Dharura na Mipango Afrika (WHO-AFRO).

Ardhi hiyo itatolewa na Chuo Kikuu cha Kenyatta, kwani ndiko kituo hicho kitajengwa.

Tangazo hilo lilifuatia kikao kilichofanyika baina ya Katibu wa Wizara ya Afya, Bi Mary Muthoni, na maafisa wakuu wa WHO, Ijumaa, Septemba 29, 2023, jijini Nairobi.

“Katibu Mary Muthoni na Bw Adama Thiam, Mkuu wa Shughuli na Usimamizi wa Mipango katika  WHO-AFRO, walifanya kikao chenye manufaa na maafisa kutoka Norway, wakiongozwa na Balozi wa Afya Duniani katika Wizara ya Mashauri ya Kigeni, John-Arne Rottingen, kuendeleza mpango huo muhimu,” ikasema Wizara ya Afya kwenye taarifa.

Kinaya ni kuwa, viongozi wa Kenya Kwanza, wakiongozwa na Rais William Ruto, walikuwa miongoni wa wanasiasa waliojitokeza kumkashifu vikali Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta, alipochukua hatua kama hiyo Julai 2022.

Patashika hiyo ilimfanya Naibu Chansela wa chuo hicho, Profesa Paul Wainaina, kufutwa kazi katika hali tatanishi. Hata hivyo, alirejeshwa kazi baada ya Rais Ruto kuibuka mshindi kwenye uchaguzi mkuu mwaka uliopita.

Kwenye kampeni zao mwaka uliopita, baadhi ya viongozi wa Kenya Kwanza walitaja hatua ya Bw Kenyatta kutoa sehemu ya ardhi hiyo kwa WHO kuanzisha kituo kama hicho kuwa “njama ya familia ya (Kenyatta) kunyakuwa ardhi hiyo”.

Alisema Spika wa Bunge la Kitaifa, Moses Wetang’ula: “Bw Rais (Uhuru Kenyatta), nilikuona kwenye runinga ukiwa umekasirika sana kuhusu uongozi wa Chuo Kikuu cha Kenyatta. Sababu kuwa chuo hicho kina jina linalofanana na lile la familia yenu, hilo haliipi uhuru familia yako kuingilia shughuli za taasisi hiyo. Chuo Kikuu cha Kenyatta kimebuniwa kwa sheria iliyo kwenye Katiba. Ningetaka kumhakikishia Profesa aliyefutwa kazi (Wainaina) kwamba, baada ya Dkt Ruto kuapishwa kama Rais, tutakurudisha kazini.”

Bw Wetang’ula alitoa kauli hiyo mnamo Julai 11, kwenye mkutano wa kampeni ya Kenya Kwanza katika Kaunti ya Narok, uliohudhuriwa na Rais Ruto, wakati huo akiwa Naibu Rais.

Wakenya wameulaumu uongozi wa Kenya Kwanza, wakisema unarejea makosa waliyomlaumu Bw Kenyatta kwa kuyaendeleza.

“Huu ni unafiki wa wazi. Mbona wanarejelea ‘makosa’ waliyodai yalifanywa na Uhuru?” akashangaa Bi Florah Mwikali, kwenye mitandao ya kijamii.

  • Tags

You can share this post!

Nimesikia fununu kwamba huyu chali akilamba...

Tanzania yaishiwa na dola za Marekani miezi michache baada...

T L