• Nairobi
  • Last Updated February 29th, 2024 5:13 PM
BAHARI YA MAPENZI: Haki ya kumiliki mali kati ya wanandoa

BAHARI YA MAPENZI: Haki ya kumiliki mali kati ya wanandoa

SIZARINA HAMISI na BENSON MATHEKA

MAISHA ya ndoa huambatana na vitu ama mali ambazo wanandoa huvipata wanapokuwa pamoja.

Vitu hivi huweza kuwa ni pamoja na nyumba, mashamba, biashara ama vyote vinavyohusisha juhudi za pamoja.

Hata hivyo, mali na vitu hivi vimekuwa ni chanzo cha changamoto nyingi katika ndoa, hasa pale wanandoa wanapokuwa wameishi kwa muda na kufanikiwa kupata vitu mbalimbali.

Utata zaidi huwa unakuja pale wanapojumuishwa ndugu wa pande zote mbili na mara nyingi waathirika wakubwa ni wanawake ambao hutengwa na mchango wao kushindwa kuonekana katika upatikanaji wa mali katika familia. Tumeshuhudia matukio ambayo wanawake wanatengwa na kuporwa kila kitu pale mume anapoaga dunia ama pale inapotokea ndoa kuvunjika. Wapo waliojipata wakihangaika na watoto baada ya mume kuaga dunia na ndugu kupora mali yote za familia.

Ni nadra kupata mwanaume akiwa katika hali ya kuporwa mali ama kutupwa nje na ndugu kwani mara nyingi wao ndio huaminiwa ni chanzo cha upatikanaji wa mali ya familia. Hata hivyo, wapo wanaume ambao wamejikuta wakiishi katika mali ambayo ni urithi wa mke ama mke ameandika kwa umiliki binafsi, hali inayopelekea pia waweze kujikuta wametupwa nje ya familia inapotokea tofauti na ndoa kuvunjika ama mke kuaga dunia.

Kwa mujibu wa sheria ya umiliki mali, ardhi na urithi ya Kenya kifungu namba 60(1a), ardhi nchini Kenya itashikiliwa, kutumiwa na kusimamiwa kwa namna ambayo ni ya usawa, fanisi, yenye tija na endelevu, na kwa kufuata kanuni ya haki sawa ya kupata ardhi.

Pamoja na sheria kuwa wazi kuhusu suala la ardhi, ni muhimu pia kuwa na makubaliano ya pamoja kwa wanandoa, hasa, wakati wa ununuzi wa mali ambazo zinawahusisha wote wawili. Makubaliano hayo ni vyema yajumuishe uandikishaji wa mali ya familia na umiliki wake. Kwa maana kama ni hati ya kumiliki ardhi, ijumuishe wanandoa ambao wako pamoja kwa wakati huo halikadhalika mali mbalimbali inayohusu familia.

Jambo la msingi ni kuweka utaratibu wa kuangalia hatima ya baadaye baina ya wanandoa kwa lolote linaloweza kutokea siku za usoni. Mke na mume wanapofunga ndoa, wanaanza maisha ya pamoja ambayo huwaunganisha kimwili, kiuchumi, kifamilia na kijamii. Kwa msingi huo ndoa yenye fanaka haina budi kuweka wazi masuala yote ambayo yamewaunganisha wawili katika ndoa. Na sababu binadamu sio malaika, migongano hutokea na inapotokea ni vyema kuwa na msingi wa suluhu kuhusiana na masuala ya mali na amali ambazo zimepatikana kwa pamoja.

Mume na mke wanayo haki sawa katika yote yanayohusu familia. Hata hivyo, angalizo kuu liwe ni mali ambayo wamechuma pamoja, inapohusu mali ya urithi ama ya jamii hali inaweza kuwa tofauti, kwani yawezana mali iliyopo wanandoa wameikuta imeshachumwa na wao wamepatiwa dhamana ya kusimamia ama kuweza kuiendeleza. Hapa ni vyema waelewe mipaka inapoishia ili kama kutatokea mfarakano, ieleweke yale ambayo yanawahusu na yale ambayo hayawahusu. Ikibidi ni vyema kuweka wosia ambao unabainisha kila kilichopo na mgawanyo wake, kwani hili pia litasaidia kuzuia ama kusuluhisha sintofahamu iwapo itatokea katika ndoa.

[email protected]

KUMEKUWA na mizozo mingi wanandoa wakilalamika kuwa waume au wake zao wanawakandamiza kwa kuwanyima haki zao.

Katika kisa kimoja, mwanamke ninayemfahamu vyema alimshtaki mumewe, baba ya watoto wake watatu kwa kumnyang’anya ploti aliyodai alichangia kuinunua.

Mwanamke huyo alisisitiza kuwa jina lake linafaa kuwa kwenye cheti cha kumiliki ploti hiyo kwa kuwa pesa alizochanga kununua ni jasho lake. Alimpa presha mumewe hadi akakubali takwa lake ili amani idumu katika boma lao.

Mwanamke ninamyetaja hapa huenda akawa mmoja wa wale wanaofahamu haki zao za kumiliki mali wakiwa katika ndoa ila nahisi alizitumia vibaya. Hakufaa kumpa presha mumewe kwa kuwa hatua hiyo ilimsawiri kama mtu mwenye tamaa na imani ya mumewe kwake ilipungua. Hatua yake pia ilionyesha hamwamini mumewe ambaye wamekuwa kwenye ndoa kwa miaka 24.

Kuna wanaume wanaoamini kuwa wake zao hawafai kumiliki mali ya binafsi, imani ambayo imepitwa na wakati. Hakuna kinachozuia mwanamke anayejitafutia mapato kwa bidii na jasho lake kununua gari, mashamba, manyumba na hata kujiwekea akiba.

Kuna wanandoa wanaoshirikiana kutafuta mali, unapata mke na mume wanachanga kufanikisha mradi wa kuwaletea mapato na kuwafaa siku zijazo. Japo hakuna sheria inayoamrisha iwe hivi, ndivyo inavyopaswa kuwa pale mapenzi yanaponawiri.

Lakini kwa sababu ya tandabelua la kuvunjika kwa ndoa siku hizi, utakuta mume na mke kila mmoja anaamua kumiliki mali yake binafsi. Hii inakinga mtu iwapo janga la talaka litamwangukia apigwe teke mikono mitupu.

Hata hivyo, hofu hii imelindwa katika sheria ya ndoa ya Kenya inayopatia wanandoa haki ya kugawana mali waliyopata katika muda ambao wamekuwa mtu na mke. Hapa wanaodandia ndoa na watu kwa sababu ya mali yao hawana bahati.

Mali ambayo mke au mume ana haki ya kudai ni iliyopatikana kuanzia tarehe ya kuhalalisha ndoa hadi inapovunjwa rasmi na korti na cheti cha talaka kutolewa. Hii inampatia mtu haki ya kumiliki mali ambayo mkewe au mumewe alipata katika kipindi cha ndoa yao.

Nafikiri hii inakinga pande zote kwa sababu katika ndoa, mume na mke huwa wanapatiana haki zao za mapenzi hadi tendo la ndoa. Ikiwa basi unadai haki ya tendo la ndoa kutoka kwa mume au mke wako na anakupatia bila masharti hadi unaridhika, kwa nini asidai mali yako mnapovunja uhusiano wenu?

Wanandoa wanaotambua na kuheshimu haki za kimsingi za kila mmoja huwa wanaishi kwa amani bila bughudha na mivutano. Mivutano kama mume kukataa kutunza watoto wake akiwa na uwezo wa kufanya hivyo na kutumia mali yake kulewa au kwa vimada ni upumbavu usiofaa kusamehewa.

Mwanamume hafai kukumbushwa haki yake kwa watoto wake ambao aliwazaa katika mazingira ya upendo na burudani na mkewe hata wakitofautiana. Kutengana kwa mume na mke hakufuti haki kwamba wao ni wazazi wa watoto wao.

Mizozo ikizuka kuhusu ukiukaji wa haki katika ndoa, inapaswa kushughulikiwa kwa misingi iliyofafanuliwa kisheria, kidini na kitamaduni na uamuzi kuheshimiwa na kila upande. Kitu kimoja ni wazi, palipo na upendo wa dhati na heshima, mume na mke hawawezi kunyimana haki.

[email protected]

You can share this post!

FATAKI: Penzi likiingia mdudu usikonde dada, jipe shughuli!

MAPISHI KIKWETU: Wali mwekundu na maharagwe ya maziwa

T L