• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 7:05 PM
LSK yawinda mawakili 21 bandia

LSK yawinda mawakili 21 bandia

NA MWANGI MUIRURI
BARAZA la Mawakili Nchini (LSK) tawi la Murang’a limezindua msako dhidi ya wanaotoa huduma za uwakili bila idhini, likisema linakisia kuna matapeli 21.

Kwa mujibu wa mwenyekiti wa LSK katika Kaunti hiyo, Alex Ndegwa, matapeli wa uwakili Murang’a wamepaka tope baraza hilo.

“Tukishirikiana na vitengo vya kiusalama tutawasakama wote wanaohusika na tuwafikishe mahakamani na kuwafungulia mashtaka ya kutapeli wakitumia taaluma ya uanasheria,” Bw Ndegwa akasema.

Ndegwa alisema kwamba tayari oparesheni kuwawinda imeanza, ambapo Desemba 1, 2023 Bi Alice Wanjiru Gitahi alifikishwa katika mahakama ya Kenol akikabiliwa na mashtaka kuhudumu kama wakili kinyume na sheria, tangu 2016.

Bi Gitahi alikana mashtaka hayo mbele ya hakimu Jakinda Renna na akaachiliwa kwa bodi ya Sh150, 000 pesa taslimu au mdhamini wa Sh300, 000.

Wakili Simon Wambugu aliyewakilisha LSK katika kesi hiyo baadaye aliambia waandishi wa habari kwamba ikiwa mawakili bandia hawataandamwa, mkondo wa haki utaingiwa na dosari kuu kiasi cha kuzua hasara katika safu zote za kimaisha.

“Huduma za kisheria ni nyeti sana na gharama ya kuingizwa ukora ni ghali mno. Unaweza ukawazia yatakayokupata ikiwa utanunua mali ukitumia uelekezi wa wakili bandia au uwekwe kwa mkataba wowote ule na mwanataaluma feki wa kisheria…Iwapo hali hiyo itagunduliwa, hasara itakayokupata si kidogo,” akasema.

Bw Wambugu alisema kwamba kuna mawakili wengine ambao wamehitimu, lakini wameajiri wasio na taaluma ya uwakili.

“Waajiriwa hao nao baada ya kuzoea kuona jinsi mikakati ya uanasheria huandaliwa, wanajitoa wakiwa na masomo yao yasiyoambatana na uwakili na kuweka maduka yao ya kuchuuza uwakili bandia,” akasema.

Katika hali hiyo, alisema Kaunti imejawa na matukio ya kufedhehesha ambapo mawakili hao feki wameingiza wengi katika dili za utapeli, wengine wakitoweka na fedha za wateja huku pia kukiwa na tetesi za wanaotetewa mahakamani wakiachwa kwa mataa baada ya matapeli hao kuhepa kujitokeza kwa kesi ili wasitambulike ni bandia.

Bw Ndegwa alisema harakati hizo za kuwafurusha mawakili bandia zitaendelea “na tukifuata sheria tutashirikiana na vitengo vingine vya kiusalama ili kutekeleza misako dhidi ya wote ambao wamefungua biashara za kuchuuza huduma za uwakili kinyume na sheria”.

Bw Ndegwa alisema harakati hizo zinaendeshwa kitaifa “kwa kuwa ikiwa tutakubalia matapeli kuteka nyara taaluma ya uanasheria, kutakuwa na hasara kubwa kwa watu na pia uchumi wa nchi”.

Aliwataka wote ambao wanatoa huduma za uwakili Murang’a na kwingineko nchini wajiandae kujitambulisha kwa mujibu wa mikakati iliyowekwa ya vigezo vya mawakili.

“Tunajua ili uwe wakili nchini Kenya kuna vigezo vya kuhitimu, kusajiliwa na pia kuwa katika orodha ya LSK inayotolewa kila mwaka,” akasema, akiongeza kuwa “ikiwa unajua hujahitimu, funga tu hiyo biashara yako ya utapeli kabla unaswe na ujipate mahakamani”.

 

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

KEBS: Mafuta yaliyosemekana kuwa hatari ni salama

Silvanus Osoro alaumu serikali ya Kenyatta kwa masaibu ya...

T L