• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 9:50 AM
Elimu ilivyochangia katika ustawi wa nchi tangu 1963

Elimu ilivyochangia katika ustawi wa nchi tangu 1963

NA DAVID ADUDA

KENYA ilipopata uhuru mwaka wa 1963, serikali ililenga kupambana na mambo matatu yakiwemo umaskini, ujinga na maradhi.

Hayo mambo matatu yalikuwa ajenda kuu ya serikali. Mpango wa kwanza wa maendeleo wa taifa, 1964 hadi 1970, ulieleza kwa uwazi mikakati ya kukabiliana na changamoto hizo na kuipa kipaumbele elimu kama nyenzo ya mageuzi ya kijamii, kiuchumi na kisiasa.

Baada ya uhuru, nchi ilikuwa ikijikwamua kutoka kwa minyororo ya utawala wa wakoloni ambapo utajiri ulikuwa umeidhinishwa na watu kujilimbikizia mali bila kujali mwananchi wa kawaida. Kutokana na ubinafsi na ubabe, serikali iliunda dhana mpya ya kuwaokoa wananchi.

Dhana ya kwanza kabisa ilikuwa kuhakikisha kuwa watu wamepata elimu msingi ili kuleta mabadiliko ambayo ingewapa Waafrika ujuzi muhimu na namna ya kuinua uchumi.

Kwa hiyo, serikali ilibuni tume ya elimu mwaka wa 1964 chini ya uenyekiti wa Profesa Simeon Ominde na kuitwika jukumu la kuunda ramani ya mfumo wa elimu nchini na sera za wahudumu.

Chini ya utawala wa kikoloni, elimu ilitenganishwa ambapo Wazungu na Waeshia walisoma shule za kifahari zilizokuwa na maarifa, ujuzi na uwezo wa kuwaongoza kwenye taaluma zenye faida kubwa na vyeo vya juu katika utumishi wa umma.

Waafrika, kwa upande mwingine, walichukuliwa kupitia mafunzo ya msingi kwa kuzingatia kile kilichojulikana kama Three Rs- ambayo inajumuisha kusoma, kuandika na kuhesabu.

Masomo hayo yalilenga kuwawezesha Waafrika kupata kibarua.

Tume ya Profesa Ominde ilikuwa na malengo saba mapana, miongoni mwao ikiwa ni kukuza umoja wa kitaifa, kuhamasisha jamii na kukuza mila na maadili ya Kiafrika.

Kadhalika, tume hiyo ilitoa mapendekezo mbalimbali ambayo yalipitishwa na serikali.

Ilitoa mapendekezo ya kimsingi kama vile kupendekeza mfumo wa elimu bila mapendeleao na kukomesha ubaguzi wa rangi.

Kwa hivyo, Tume ya Ominde ilipendekeza mfumo wa elimu wa 7-4-2-3 ambao ulitumika nchi kwa karibu miongo miwili, ambayo ilibadilishwa kuwa wa 8-4-4 mnamo 1985.

Pia ilipendekeza kuanzishwa kwa mwajiri mmoja ili kuwaleta walimu wote pamoja chini ya utawala mmoja tofauti na ilivyokuwa katika utawala wa kikoloni ambapo walimu waliajiriwa na mashirika mbalimbali yakiwemo makanisa na mamlaka za mitaa.

Aidha, Tume ilipendekeza utoaji wa elimu ya msingi bila malipo, ambayo baadaye ilianzishwa mwaka 1974, ikijumuisha Darasa la Kwanza hadi la Nne. Kutokana na mapendekezo hayo, serikali ilianza mpango mkubwa wa upanuzi wa shule na mafunzo ya walimu ili kukidhi mahitaji ya wanafunzi.

Ushahidi wa ukuaji ulidhihirika kutokana na upanuzi wa shule katika muongo wa kwanza wa uhuru. Kuanzia 1963, shule za msingi zilikuwa na jumla ya wanafunzi 891,553 waliosajiliwa lakini hii ilipanda kwa kasi hadi 1,428,000 mwaka 1970 na kuongezeka maradufu hadi 2,881,000 mwaka 1975.

Kadhalika, katika ngazi ya shule za sekondari, idadi ya wanafunzi ilipanda kutoka 30,000 mwaka wa 1963 hadi 126,900 mwaka wa 1970 na baadaye kuongezeka maradufu hadi 217,400.

Katika ngazi ya chuo kikuu, idadi ya wanafunzi iliongezeka kutoka 370 mwaka 1963 hadi 2,300 mwaka 1970/71 na 5,140 mwaka wa 1975 hadi 1976. Hakika, hii iliweka mwelekeo wa upanuzi mkubwa wa nchi katika viwango vyote vilivyoendelea hadi sasa.

Kupanuka kwa shule na kuongezeka kwa idadi ya watu waliopata masomo ulionyesha maendeleo ya uchumi wa nchi. Kati ya 1963 na 1972, Kenya ilirekodi ukuaji wa wastani wa uchumi wa asilimia 6.6 kila mwaka, jambo ambalo lilienziwa na serikali.

Hali nzuri za kiuchumi ni kichocheo cha maendeleo ya elimu. Wale waliosoma walipata ajira, jambo ambalo liliwafanya wengi kuenzi elimu.

Hata hivyo, mambo yalibadilika 1973 na baadaye 1979 ambao bei za bidhaa zilipanda kwa asilimia kubwa na kufanya uchumu kuanza kuzorota.

Hii iliilazimisha serikali kujipanga upya ili kuimarisha uchumi wa nchi. Kuzorota kwa uchumi wa nchi kuliathiri sana sekta kama vile elimu na biashara. Elimu na huduma nyingine za kijamii zilitwikwa mzigo mkubwa hasa kutokana na changamoto zilizoibuka za utandawazi na mabadiliko ya kisiasa. Hii ililazimisha serikali kufikiria upya namna ya kuendelea kutoa elimu kwa wananchi.

Ili kukabiliana na hali hiyo, serikali iliunda Kamati ya Kitaifa ya Malengo na Sera za Elimu mwaka wa 1975, iliyoongozwa na Peter Gachathi, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu wakati huo.

Jukumu lake kubwa lilikuwa ni kupitia upya malengo ya kitaifa ya elimu na sera na kuyaoanisha na hali halisi inayojitokeza wakati huo na pia kuishauri serikali kuhusu mfumo bora wa elimu.

Kamati ilihitimisha na kukabidhi ripoti yake Oktoba 1976. Bw Gachathi alipendekeza mfumo wa elimu ubadilishwe ili kuwaruhusu wanafunzi kusoma miaka tisa katika shule za msingi na shule za upili miaka minne.

Mnamo 2012, serikali ilibuni jopokazi jingine ambalo liliongozwa na Profesa Douglas Odhiambo, aliyekuwa naibu chansela wa Chuo Kikuu cha Moi, ili kutoa ushauri kuhusu mpango mpya wa elimu.

Jopokazi hilo lilipendekeza mfumo mpya wa elimu ambao ulisisitiza umahiri badala ya kupata maarifa tu. Pendekezo hilo lilizalisha mtaala wa CBC uliotekelezwa 2017.

CBC imejikita katika nguzo saba, ambazo ni, mawasiliano na ushirikiano, kujitegemea, kufikiri kwa kina na kutatua matatizo, ubunifu, uraia, ujuzi wa kidijitali na uwezo wa kujisimamia kama mwananfuzni.

Kikundi cha kwanza kusoma chini ya mtaala wa CBC ni wanafunzi waliojiunga na Sekondari ya Msingi (JSS) mwaka huu 2023.

  • Tags

You can share this post!

Viongozi wahimizwa kupiga jeki wanamichezo

Askari aangushiwa kichapo kwa madai ya wizi wa ng’ombe  

T L