• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
MWALIMU WA WIKI: Anatumia nyimbo kufunzia darasani

MWALIMU WA WIKI: Anatumia nyimbo kufunzia darasani

Na CHRIS ADUNGO

KUSOMA kwingi, kufanya utafiti wa kina na kuwauliza wajuao ni mazoea ambayo humjenga mwalimu kitaaluma.

Haya ni kwa mujibu wa Bw David Njoroge Kagiri ambaye sasa anafundisha Kiswahili na somo la Dini katika Shule ya Msingi ya Anestar Prestige, Kaunti ya Nakuru.

“Mwalimu bora huelekeza wanafunzi kwa utaratibu ufaao huku akiwahimiza mara kwa mara katika safari yao ya elimu. Huwa karibu na wanafunzi wake na hutia azma ya kufahamu changamoto wanazozipitia wakiwa shuleni na nyumbani,” anasema.

Kinachomtofuatisha Njoroge na walimu wengine ni upekee na wepesi wake wa kutunga nyimbo rahisi zinazowezesha wanafunzi kukumbuka hoja muhimu katika takriban kila mada – si aina za maneno, si ushairi, si msamiati!

“Nyimbo hizi hufanya wanafunzi kuelewa mambo haraka, huwapa hamu ya kujifunza vitu vipya na hawafanya kutosahau wanachofundishwa. Pia ni mbinu inayowapa baadhi yao jukwaa la kutambua vipaji vyao,” anaeleza.

Njoroge alizaliwa 1993 katika eneo la Molo, Kaunti ya Nakuru na akalelewa katika kijiji la Mirangine, Kaunti ya Nyandarua. Ndiye wa nne kuzaliwa katika familia ya watoto wanane wa Bw William Kagiri na Bi Salome Wanjiku.

Alisomea katika shule za msingi za Kamuyu na Matunda, Nyandarua (1997-2009) kabla ya kujiunga na Shule ya Upili ya Moi NDEFFO (kwa sasa Heroes High School), Nakuru kati ya 2010 na 2013. Ilikuwa hadi Januari 2022 alipojiunga na Chuo cha Mafunzo ya Ualimu cha St Mary’s Nakuru.

Alianza kufundisha wanafunzi wa shule za msingi kutoka Nyandarua yeye mwenyewe akiwa mwanafunzi wa kidato cha tatu. Vipindi vya masomo ya ziada alivyokuwa akiviendesha nyumbani kwao vilimpa jukwaa la kuzima kiu ya ualimu na vikamwamshia ari ya kuthamini na kuchapukia Kiswahili.

Baada ya kukamilisha KCSE, alifundisha katika Shule ya Msingi ya Janet Academy (2014-15) kabla ya kuhamia Chema Academy (2016-17) kuwa mwalimu wa Kiswahili na mwelekezi wa michezo. Shule hizi zinapatikana Nyandarua.

Alihudumu katika Shule ya Msingi ya Vision Preparatory, eneo la Subukia, Nakuru (2017-18) kabla ya kurejea Chema Academy (2019) kisha kuajiriwa na Anestar Prestige mnamo Januari 2021. Yeye kwa sasa ndiye mlezi wa Chama cha Uanahabari shuleni humo.

Zaidi ya kuwa mhubiri katika Kanisa la AIPCA Nakuru, Njoroge ambaye ni mpenzi kindakindaki wa gazeti la ‘Taifa Leo’, pia ni mtunzi mahiri wa mitihani ya Kiswahili. Tajriba pevu na uzoefu mpana anaojivunia katika ulingo huo umemwezesha kuzuru shule nyingi za humu nchini kwa nia ya kuhamasisha walimu na kuelekeza wanafunzi kuhusu mbinu faafu na mwafaka zaidi za kujiandaa kwa mitihani ya KCPE.

Amewahi kutuzwa na kampuni ya Nation Media Group (NMG) baada ya kuibuka mwelekezi bora wa wanafunzi wake kwenye mikumbo mbalimbali ya ‘Shindano la Uandishi wa Insha’ katika gazeti hili.

Miongoni mwa mikota wa lugha wanaozidi kumchochea Njoroge kitaaluma na kumpigia mhuri wa kuwa mwalimu arifu na mwandishi stadi wa Kiswahili ni Guru Ustadh Wallah Bin Wallah, Bw Ernest Macharia (Makueni) na Bw Kabuchwa Bin Kabuchwa wa Shule ya Msingi ya Rift Valley Prestige katika eneo la Njoro, Nakuru.

Azma yake ya kuwa mwalimu ilipaliliwa na mwalimu Kung’u wa Shule ya Msingi ya Matunda na Bw Kiai aliyempokeza malezi bora zaidi ya kiakedemia na kukikuza kipaji chake cha uandishi wa kazi bunilizi katika Shule ya Msingi ya Kamuyu.

Kwa imani kwamba mfuko mmoja haujazi meza, Njoroge pia ni mkulima na mfugaji katika eneo la Nyandarua. Kubwa zaidi katika maazimio yake ni kuwa mwandishi mahiri wa vitabu vitakavyobadilisha sura ya ujifunzaji na ufundishaji wa uandishi wa Insha katika shule za msingi nchini Kenya.

Kwa pamoja na mkewe Bi Beth Waithera, wamejaliwa watoto wawili – Angel Wanjiku na Angelina Muthoni. Bi Waithera kwa sasa ni mwalimu wa Kiingereza na Hisabati katika Shule ya Msingi ya Bagaria, Njoro.

You can share this post!

Mvutano kuhusu mswada tata wa vyama kukita katika seneti

Beki Axel Tuanzebe ajiunga na Napoli ya Italia kwa mkopo

T L