• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 6:07 PM
Mvutano kuhusu mswada tata wa vyama kukita katika seneti

Mvutano kuhusu mswada tata wa vyama kukita katika seneti

Na CHARLES WASONGA

WANDANI wa Naibu Rais William Ruto na kiongozi wa ODM Raila Odinga katika seneti wanatarajiwa kukabiliana tena wakati wa mjadala kuhusu mswada wa marekebisho ya sheria za vyama vya kisiasa Jumanne.

Mswada huo ambao ulipitishwa katika bunge la kitaifa wiki jana, utawasilishwa rasmi katika seneti wakati wa kikao maalum kilichoitishwa na Spika wa bunge hilo Ken Lusaka.

Mswada huo ambao unalenga kugeuza vuguvugu la Azimio la Umoja kuwa chama cha kisiasa, ulipitishwa katika kikao kilichosheheni fujo katika bunge la kitaifa wakati wabunge wanaoegemea kambi ya Dkt Ruto waliupinga vikali.

Hata hivyo, jumla ya hoja 30 za kuufanyia marekebisho mswada huo zilizowasilishwa na wabunge hao wa mrengo wa ‘Tangatanga’ ziliangushwa na wabunge wa kambi ya handisheki, ambao ni wandani wa Rais Uhuru Kenyatta na Bw Odinga.

Wandani wa Dkt Ruto wanadai mswada huo unalenga kumsaidia Bw Odinga kushinda urais katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022.

Bw Odinga analenga kugeuza Azimio la Umoja kuwa muungano mkubwa ambao utashirikisha chama tawala Jubilee na vyama vingine vyenye maoni sawa na vinavyoongoza azma yake ya kuingia Ikulu.

Kulingana na ratiba ya shughuli iliyoandaliwa na Kamati ya Kuratibu Shughuli za Seneti, maseneta wamepewa muda wa hadi Januari 27 kukamilisha mjadala kuhusu mswada huo; katika hatua zote.

“Mnamo Jumanne mswada huo utasomwa kwa mara ya kwanza ukumbini. Baada ya hapo umma na wadau mbalimbali wataalikwa kutoa maoni au mapendekezo kuhusiana na mapendekezo mbalimbali katika mswada huo,” Kiranja wa Wachache Mutula Kilonzo Junior akasema.

Shughuli ya kukusanya maoni na mapendekezo ya umma kuhusu mswada huo itaendeshwa na Kamati ya Seneti kuhusu Haki, Masuala ya Sheria na Haki za Kibinadamu inayoongozwa na Seneta wa Nyamira Okong’o Omogeni.

Kisha mnamo Januari 25, kamati hiyo itawasilisha ripoti yake katika kikao cha bunge lote la seneti ili ijadiliwe na kupigiwa kura.

Wanachama wa kamati hiyo wanajumuisha mawakili na wanasheria wenye uzoefu mkubwa nchini.

Wao ni Kiongozi wa Wachache James Orengo, Mwanasheria Mkuu wa zamani Amos Wako, Mutula Junior, Seneta wa Murang’a Irungu Kang’ata na mwenyekiti Bw Omogeni mwenyewe.

Wanachama wengine ni Seneta wa Nairobi Johnson Sakaja, Fatuma Dullo (Isiolo) na Seneta Maalum Naomi Waqo.

Kamati hiyo inaweza kupendekeza marekebisho zaidi kwa mswada huo au wanachama wake wapendekeze kuwa upitishwe jinsi ulivyo.

Baadaye maseneta wote watapewa muda wa siku mbili kujadili mswada huo mnamo Januari 26 na Januari 27 ambapo inatarajiwa kuwa maseneta wandani wa Dkt Ruto watapendekeza mapendekezo kadha ya mabadiliko.

Inatarajiwa kuwa kikao cha kujadili mswada huo katika kamati ya bunge lote kitaibua cheche na joto kali jinsi ilivyofanyika katika bunge la kitaifa wiki moja iliyopita.

“Binafsi nitawasilisha hoja ya kuondoa sehemu zote za mswada huo ambazo zina mapendekezo yanayokiuka Katiba. Kwa mfano, ninapinga sehemu ya tano inayopendekeza kubuniwa kwa chama cha muungano,” Seneta wa Nandi Samson Cherargei aliambia Taifa Leo.

Bw Cherargei hata hivyo, alisema kuwa anatarajia kuwa mswada huo utajadiliwa katika mazingira ya utulivu bila vurugu zilizoshuhudiwa katika Bunge la Kitaifa.

“Sisi hatuwezi kupigana kama watoto jinsi wale wengine walivyofanya. Tutatofautiana kwa uungwana na heshima,” akasema seneta huyo ambaye ni mwandani wa Dkt Ruto.

Naye Spika Lusaka alisema anatarajia kuwa maseneta watajadili mswada huo kwa ukomavu na heshima kuu pasina kuzomeana au kupigana.

You can share this post!

PAUKWA: Getore afumaniwa akichoma makaa

MWALIMU WA WIKI: Anatumia nyimbo kufunzia darasani

T L