• Nairobi
  • Last Updated February 25th, 2024 10:30 AM
Maina Njenga ni mradi wa Gachagua kuzima umaarufu wa Kenyatta?

Maina Njenga ni mradi wa Gachagua kuzima umaarufu wa Kenyatta?

NA MWANGI MUIRURI

HUENDA ikawa harakati za aliyekuwa kinara wa kundi haramu la Mungiki katika Mlima Kenya ambapo anatesa, akisema analenga kuwa msemaji wa kisiasa eneo hilo ni njama ya serikali ya kumzima aliyekuwa Rais wa Nne Bw Uhuru Kenyatta.

Tangu astaafu, Bw Kenyatta amekuwa akirushia serikali ya William Ruto cheche za shutuma akishikilia kwamba yeye ni mwanachama wa Azimio la Umoja ambapo kinara wake ni Raila Odinga.

Aidha, wafuasi wa Kenyatta Mlima Kenya wamekuwa wakisisitiza kwamba yeye ndiye bado msemaji wa watu wa eneo hilo na hatapisha mwingine hivi karibuni bila ya kuwahusisha wenyeji katika kuamua ni nani atarithi mikoba hiyo.

Kwa upande mwingine, wafuasi wa serikali ya Kenya Kwanza katika Mlima Kenya wamekuwa wakisema kwamba Naibu wa Rais Rigathi Gachagua ndiye kinara wa siasa za eneo hilo kupitia wadhifa wake unaomweka kidedea kimamlaka.

“Hapo ndipo siasa zinaingia sasa ambapo katika kuzima ushawishi wa Bw Kenyatta huenda Bw Gachagua amemshinikiza Maina Njenga kuendeleza harakati za ukaidi kwa jina la Azimio Mlima Kenya. Kwa kuwa Njenga huchukuliwa kwa tahadhari kuu na wenyeji, hali hiyo inaishia kumfanya Bw Kenyatta kuonekana mwenye nia mbaya kwa kusalia Azimio,” asema mchanganuzi wa siasa za eneo hilo, Prof Ngugi Njoroge.

Bw Njoroge anaongeza kuwa harakati za Bw Njenga za kusaka makuu ya kisiasa eneo hilo yamekuwa yakichanganya wengi kwa kuwa nusu anaonekana akiridhiana na serikali na nusu nyingine akikwama ndani ya Azimio.

“Mimi sina shida na mtu yeyote. Awe ni Bw Gachagua, Kenyatta…Nani mwingine katikia siasa za Mlima Kenya…mimi niko kule kwingine kuchunga masilahi yetu ya hapa mlimani na hata ikibidi, mimi nitaingia katika siasa za Mlima Kenya kuungana na wengine wote ili tuwe kitu kimoja,” akasema Bw Njenga katika mazishi ya Bi Muthoni Kirima mnamo Septemba 22, 2023, Kaunti ya Nyeri.

Afisa mmoja wa ngazi ya juu katika eneo la Kati amedokezea Taifa Leo Dijitali kwamba “tumeambiwa tusimtatize Bw Njenga akiandaa mikutano yake ya kisiasa eneo hili…Tumeambiwa kwamba yeye anafanyia serikali kazi na hana hatari yoyote”.

Katika hali hiyo, Bw Njenga tayari ameandaa mikutano mikubwa ya kisiasa katika Kaunti za Murang’a na Nyeri na ameratibiwa kuandaa mingine katika Nyandarua, Kirinyaga, Embu, Nairobi, Nakuru, Meru, Tharaka Nithi, Kiambu na Laikipia.

Licha ya kuwa amekuwa akijaribu kuwa mbunge na seneta katika Kaunti ya Laikipia na kuangukia pua kwa kiwango kikuu, ubabe anaousaka Mlima Kenya unasemwa na wengi kuwa siasa iliyopangwa.

“Bw Njenga sio maarufu Mlima Kenya…Ukihusishwa na mrengo wa Bw Njenga katika siasa za eneo hilo, utaanguka kura. Kuna mwanasiasa mashuhuri wa Kaunti ndogo ya Kigumo ambaye amekuwa akihusishwa na siasa za Mungiki na amekuwa akianguka kura licha ya kuonekana akiwa maarufu na anayeweza kubadilisha maisha ya wenyeji,” akasema mwenyekiti wa muungano wa wanataaluma chipukizi ndani ya siasa katika eneo la Kati Bw Jason Mburu.

Katika hali hiyo, kuendelea kuwika kwa Bw Njenga katika eneo hilo huku akisambaza ari yake ya kuwa kinara wa siasa za eneo hilo kunatafsiriwa na wanaoelewa siasa za Mlima Kenya kuwa njama ya kumpiga kisiasa Bw Kenyatta na pia Bw Odinga.

“Bw Njenga akikutaja hadharani kama mshirika wake wa kisiasa, sahau kura za Mlima Kenya. Kundi lake la Mungiki wakati lilikuwa hai na ushawishi liliishia kujipa nembo ya ukatili na usambaratikaji wa uchumi na huonekana kama ugaidi wa kukemewa,” akasema Mbunge wa Naivasha Bi Jane Kihara.

Wachanganuzi wanasema kwamba mkutano na waandishi wa habari wa hivi majuzi uliowaleta pamoja wanawake wa Kenya Kwanza bungeni kukemea harakati za Bw Njenga, ni njama tu ya kisiasa ya kuwakumbusha wenyeji kwamba wote walio na asili ya Mungiki ni hatari.

“Ilikuwa tu mbinu ya kisiasa ya kumkubalia Bw Njenga aendelee kuwika nyanjani kwa niaba ya Azimio huku nao walio na ufuasi kwa Bw Gachagua na serikali ya Kenya Kwanza wakipiga siasa za kuwakumbusha wenyeji kwamba Njenga na washirika wake bado sio wa kuaminika na huenda warejeshe kundi la Mungiki katika jamii za eneo hilo,” akasema Prof Njoroge.

 

[email protected]

 

  • Tags

You can share this post!

Serikali kutambua rasmi vazi la uponyaji la Mijikenda...

Sababu ya mibuyu kuhusishwa na mashetani

T L