• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
MALEZI KIDIJITALI: Mwongoze kwa vitendo kutumia mitandao

MALEZI KIDIJITALI: Mwongoze kwa vitendo kutumia mitandao

Watoto huwa wanaiga jinsi wazazi wanavyotumia vifaabebe.

Wataalamu wanasema kuwa tajriba ya watoto mtandaoni huwa inategemea vitu vingi ikiwemo marafiki na watu maarufu, apu ibuka na mitindo ya teknolojia na mambo mengine yanayowavutia.

Hata hivyo, haya yote yanaweza kukosa kuwa na athari hasi kwao iwapo mzazi atakuwa mfano bora wa kuigwa.

“Ule ushawishi mkubwa ambao unaathiri mtoto katika matumizi ya vifaabebe unatoka nyumbani; na ni mzazi wake,” wanasema wataalamu wa malezi katika makala yaliyochapishwa kwenye tovuti ya teknolojia ya Vodafone.

“Ni kawaida ya watoto wadogo kuiga tabia za watu wazima katika maisha yao, kwa hivyo ni muhimu kuwa mfano bora zaidi kuanzia mwanzo,” wanaeleza wataalamu hao.

Wanasema kwamba mzazi akiwa mateka wa vipindi vya runinga, itakuwa vigumu kumweleza mtoto wake kwamba ni makosa kufanya hivyo.

“Ikiwa wewe ni mtu wa kuzama kwa simu kuwasiliana na marafiki kwenye mitandao ya kijamii hadi unakosa muda wa kumwelekeza mtoto wako, itakuwa vigumu kumweleza asizame kwenye vifaabebe. Hivyo basi, onyesha mtoto wako kwa vitendo na atakua akikuiga,” wanaeleza wataalamu hao.

Kulingana na mtaalamu wa malezi Jephinada Aluoch, mzazi anafaa kuwa msitari wa mbele kutimiza masharti au kanuni anazoweka kwa watoto wake.

“Ukipiga marufuku matumizi ya vifaa vya dijitali wakati wa chajio au kabla ya kwenda kulala, unapaswa kuwa mfano ambao wanao watafuata,” asema Aluoch.

Anasema ili watoto waweze kufahamu kuwa kuna hatari ya kuchapisha baadhi ya vitu kwenye mtandao, mzazi anaweza kuwaomba ruhusa kabla ya kuchapisha picha yao au ya familia kwenye kurasa za mitandao ya kijamii.

Ili kuhakikisha kuwa watoto hawazami kwenye hatari zinazoibuka mtandaoni, wataalamu wanapendekeza wazazi wasiwabanie wanayofanya mtandaoni.

“Onyesha mtoto kwamba unatumia mtandao kufanya kazi, kuwasiliana au kujua yanayojiri na atakua akijua manufaa chanya ya mtandao,” aeleza Aluoch.

You can share this post!

FATAKI: Vipodozi haviongezi wala kupunguza werevu wako,...

BAHARI YA MAPENZI: Kukabili mtazamo hasi dhidi ya wanawake

T L