• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 6:07 PM
FATAKI: Vipodozi haviongezi wala kupunguza werevu wako, ubongo ni ule ule!

FATAKI: Vipodozi haviongezi wala kupunguza werevu wako, ubongo ni ule ule!

NA PAULINE ONGAJI

HIVI majuzi nilikumbana na mjadala wa kusisimua uliokuwa ukiendelea baina ya wanaume wawili.

Wawili hawa walikuwa wakimzungumzia mkubwa wao kazini ambaye ni mwanamke.

“Ameniita kwenye dawati lake ambapo nilimpata kama amevua barakoa yake, ambapo tulipokuwa tukizungumza nilishangaa kuona vazi hili lilikuwa limechafuka kwa vipodozi,” akasema.

Kulingana nao, lilikuwa jambo la kusikitisha kwa mwanamke mwenye elimu na taaluma ya juu kama huyo mkubwa wao, kujipaka vipodozi.

“Kwa nini mwanamke mwerevu hivyo anatumia mapambo? Anapata wapi muda? Vipodozi ni vya mabinti wapumbavu wasiojielewa na wasio na akili ya kufanya chochote, ndiposa wanatumia muda wao mwingi kujipodoa ili kunasa macho ya wanaume,” wakaongeza.

Kumekuwa na dhana potovu kwamba urembo na mwonekano wa kupendeza, haviwezi kamwe kuambatanishwa na werevu na ustadi kitaaluma.

Eti ikiwa wewe ni mwanamke msomi na mwenye taaluma ya juu, basi hupaswi kujipodoa, ilhali ikiwa unapendelea kujipodoa, basi kichwa chako kimejaa uji.

Huo ni uwongo mtupu! Nani aliyesema kwamba werevu na utaalam kwa mwanamke haupaswi kuambatanishwa na urembo au kujipodoa?

Nani aliyesema kwamba werevu kamwe hauwezi ‘ambatanishwa na urembo?

Hii inanikumbusha maisha ya shule ya upili ambapo wasichana waliodhaniwa kuwa werevu, walikuwa wakinyoa nywele na hawakuchukua muda wao kujipodoa, ilhali wale waliokuwa wakichukua muda wao kujipamba tokea kichwani hadi miguuni, walionekana kuwa wapumbavu kimasomo.

Ni suala ambalo wakati mmoja liliibua kikundi cha baadhi ya walimu waliokuwa wakihoji kwamba msichana akiwa na nywele ndefu hawezi makinika kimasomo.

Nusura kikundi hiki kifaulu katika kuishawishi bodi ya shule ipige marufuku nywele ndefu miongoni mwa wasichana.

Wasichana na wanawake ulimwenguni kote wanapaswa kujua kwamba kujipodoa na kurembekea hakukupunguzii wala kukuongezea chochote akilini, sawa na jinsi usahili haukuongezei wala kukupunguzia akili.

Ikiwa wewe ni mwerevu, hata ujipodoe au la, akili ni ile ile na ikiwa u mpumbavu, hata ujimwagie vipodozi, hali itasalia ile ile.Kwa ufupi, usahili au vipodozi haviongezi wala kupunguza werevu. Ubongo ni ule ule!

You can share this post!

HUKU USWAHILINI: Corona imeanika mikataba feki ya mapenzi...

MALEZI KIDIJITALI: Mwongoze kwa vitendo kutumia mitandao

T L