• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 1:13 PM
Maoni mseto kuhusu sare mpya za polisi baadhi wakitaka mifuko iondolewe

Maoni mseto kuhusu sare mpya za polisi baadhi wakitaka mifuko iondolewe

NA SAMMY WAWERU

PINDI tu baada ya Idara ya Huduma ya Polisi Nchini (NPS) kuzindua aina mpya ya sare za maafisa wake, Wakenya walielekeza hisia zao mitandaoni kutoa maoni.

Uzinduzi huo ulifanyika mnamo Jumanne, Agosti 29, 2023 katika Kaunti ya Nairobi, NPS ikihimiza wananchi kutoa mapendekezo yao kuhusu sare hizo.

Vikao vingine vitaandaliwa maeneo tofauti nchini.

Wakiwa wamevalia mashati (wanaume) na blauzi (wanawake) ya samawati na suruali ndefu ya samati iliyoshika, picha za askari waliotumika zilisambaa mitandaoni na kuvutia mseto wa maoni.

Baadhi ya wachangiaji mitandaoni walizua ucheshi, wakitaka sare za polisi zisiwekwe mifuko.

@Otieno Makagutu, OFMCap alipendekeza katika Twitter mifuko yote itolewe kisha washonewe muundo wowote ule, kauli iliyopigwa jeki na Boniface Mwangi.

“Tunapendekeza sare zisizo na madoido wala mifuko. Hawatakuwa (akimaanisha askari) na jukwaa kuendeleza uitishaji hongo,” @Boniface Mwangi akaelezea, akionekana kurejelea polisi kukashifiwa kuhusu rushwa katika utendakazi wao.

Naye MR RIGHT, alizua ucheshi akishangaa ni kwa nini mifuko ya sare hizo mpya ilikuwa kubwa.

Maoni sawa na hayo yalitolewa Facebook na wananchi.

“Mifuko yote itolewe…Hakuna cha hongo,” Santos Garvey Jr aliandika.

Waindava Junior alichangia, “Watoe mifuko kwa hizo sare.”

Septemba 2023, chini ya utawala wa Rais Uhuru Kenyatta (ambaye kwa sasa ni mstaafu), NPS ilizindua sare nyingine – Ya samawati, japo rangi hiyo ilikosolewa na wengi.

Dkt Fred Matiang’i, ndiye aliongoza shughuli hiyo wakati akihudumu kama Waziri wa Usalama wa Ndani na Mikakati ya Serikali.

Maafisa wa polisi, kitengo cha kawaida na askari tawala (AP) wamekuwa wakivalia sare zinazokaribia kufanana na za Idara ya Jeshi (KDF).

Askari kawaida vilevile huvalia mavazi ya samawati, haswa za maafisa wa trafiki.

D Kinyua DK Kinyua, kupitia Facebook alishauri NPS akisema sare bora na zinazovutia zaidi ni zile za kitambo.

Wengi wanaonekana kukosoa hatua ya kubadilisha sare za polisi, baadhi wakitaka kujua aliyepewa tenda kuzishona.

“Swali ni je; Nani ameshinda kandarasi kuzishon?” @Regina Timothy alitaka kujua.

Badala yake, Wakenya wanataka maslahi ya askari hasa kimishahara na makazi kuangaziwa kikamilifu.

Majuzi, serikali ilitangaza nyongeza ya mishahara ya kati ya Sh1, 000 hadi Sh11, 000, kulingana na ngazi ya askari.

Hali kadhalika, wananchi wanashinikiza NPS kuweka mikakati maalum na kabambe kulainisha idara hiyo hasa kutokana na kuandamwa visa chungu nzima vya hongo.

 

 

 

 

  • Tags

You can share this post!

Thika mbioni kupata hadhi ya ‘smart city’

Wanaume Murang’a hutandikwa sana na wake wao –...

T L