• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 6:55 AM
MAWAIDHA YA KIISLAMU: Sheikh Muhammad Swalihu alikuwa ni mfano bora wa kuigwa

MAWAIDHA YA KIISLAMU: Sheikh Muhammad Swalihu alikuwa ni mfano bora wa kuigwa

NA ALI HASSAN

KWA jina lake Allah (SWT), mwenye kuneemesha neema kubwa kubwa na neema ndogo ndogo.

Tumejaaliwa leo hii, siku hii kubwa na tukufu ili kuambizana mawili matatu kuihusu dini yetu tukufu ya Kiislamu. Na pia kuhimizana kutenda mema, amali za kheri, na kukanyana dhidi ya mawi, dhambi (ziwe ndogo au kubwa).

Awali ya yote twachukua uzito wa nafasi hii kumhimidi, kumuenzi na kumtukuza Muumba wetu Mola Moliwa. Hakuna mwingine anayepaswa kuabudiwa ela ni Muumba wetu mmoja pekee: Mwenye-Enzi-Mungu.Ama baada ya kumtukuza na kumpwekesha Muumba wetu (SWT), twachukua nafasi hii kumtilia dua Mwombezi wetu (SAW).

Kwa hili nalo tujikaze na kujizika katika utendi wa mema na kumcha Mola wetu mmoja pekee. Leo hii ndugu yangu mada ya leo inahusiana na mauti. Nianze kwa kusema kuwa wepo miongoni mwetu wengi tu ambao tulikuwa nao jana, juzi, hata labda leo hii asubuhi, lakini nukta hii hawawezi kuyasoma makala haya.

Wametangulia mbele za haki. Vivyo hivyo, hatujui, ni lini mimi na wewe tutachukuliwa na Muumba wetu. Ela tunachokijua, kwa yakini ya mia fil mia, ni kuwa mimi na wewe, ipo siku, nukta na sekunde ambapo tutatangulia mbele za haki.

Dini yetu ya Kiislamu imetufunza kuwa kila nafsi itayaonja mauti. Tunaambiwa kuwa kullu nafsin zaikatul mauti.

Hivi tunavyozungumza ni kuwa umma wa Kiislamu nchini unaomboleza kufuatia kifo cha imamu wa msikiti wa Jamia, jijini Nairobi marehemu Muhammad Swalihu. Jana tu alikuwa miongoni mwetu. Tukila, kucheka, kupigana makamama na kufurahia naye. Leo hii sio tu ametangulia mbele za haki, lakini twatanguliza marehemu kwenye jina lake.

Mengi yamesemwa sana kumhusu marehemu. Na yatazidi kusemwa hadi tutakapokutana naye majaaliwa. Leo hii tutanukuu mawili matatu ambayo tunaweza kujifunza kutokana na marehemu imamu wetu, kipenzi chetu Muhammad Swalihu.

Wiki hii kwenye mitandao imekuwepo hotuba ya marehemu, hasa mtandao wa Horizon TV, alipokuwa akiwahutubia wanaumma wa Kiislamu. Siku hiyo ilikuwa ni Aprili, tarehe 29 mwaka huu. Sawa na tarehe 28 mwezi mtukufu wa Ramadhan 1443. Kwenye hotuba hii, marehemu anaeleza ni kwa namna gani amekuwa akitoa hotuba yake ya mwisho, kwa maana ya kila Ijumaa ya mwisho ya mwezi mtukufu wa Ramadhan. Ijapo siku hii hakutoa hotuba, lakini ilikuwa ni kauli ya kuushukuru umma wa Kiislamu. Marehemu alitoa dua. Akatokwa na kilio.

Aidha, kwenye hotuba hiyo, tulijifunza mlahaka mzuri aliokuwa nao marehemu na wanakamati wa benki hiyo, hadi kuhakikisha kuwa imamu wetu anafika msikitini siku hiyo. Mola ajaalie mshikamano kama huo miongoni mwetu. Na hili la umoja, na mshikamano lilithibitishwa kwa kauli ya Shekhe Abdullatif Essajee ambaye alimsifia marehemu Muhammad Swalihu Muhammad kwa kuwa nao kwa utulivu karibia miaka ishirini na saba.

Naye Shekhe Ahmad Athman alikumbukia namna marehemu alivyokuwa na wanafunzi aliowafunza dini kote duniani. Na kila Jumapili baada ya swala ya Isha hadi saa nne usiku, ‘angekutana’ nao kupitia mitandao kama ya WhatsApp, na kuendeleza dini.

Shekhe Juma Amir anakumbuka ni kwa vipi marehemu alimtia shime katika kazi ya da’awa. “Siku zote marehemu angekutikana katika jambo la kheri, iwe ni kusomesha, kuswalisha, kupatanisha, kuozesha na kadhalika. Yaani ibada tu”

Mimi na wewe ndugu yangu tunaelewa ni kwa namna gani msikiti uisokuwa na imamu madhubuti na kamati tahbiti jinsi ambavyo inavyoweza kuyumbishwa, kusambaratika na kuishia malumbano na chuchuhu.

In Shaa Allah Mola utujalie hatima njema na kwa siku zetu zilizosalia ziwe za kheri amin.

Ijumaa Kareem!

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: Uhuru wa mahakama usifanyiwe masihara

Raila arudi mitaani kujumuika na raia

T L