• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 9:55 AM
MITAMBO: Hii ‘honey press’ itakukamulia asali unavyotaka

MITAMBO: Hii ‘honey press’ itakukamulia asali unavyotaka

NA RICHARD MAOSI

ZOEZI la kukamua asali kutoka kwenye masega yaani honey combs huchukua sehemu muhimu katika shughuli nzima ya kilimo biashara cha kuwafuga nyuki.

Aidha, ni kazi ambayo inahitaji utaratibu wa aina yake kwa kuzingatia usafi na umakini wa hali ya juu kabla ya asali kupitia katika kichujio, kwa ajili ya matumizi ya binadamu.

“Hivyo basi kutumia teknolojia mahususi kutawasaidia wafugaji wa nyuki kupata soko na vilevile kutengeneza bidhaa nyinginezo kama vile nta zinazotokana na nyuki,” anasema Paul Mutua mtaalam wa masuala ya kutengeneza bidhaa za nyuki.

Isitoshe, sekta ya ufugaji nyuki imetoa fursa ya ziada kwa wakulima ambapo wahusika wamejitosa kwenye uga wa kutengeneza mizinga (langstroth hives), vyombo vya kurina asali pamoja na magwanda ya usalama.

Anashauri kuwa hatua ya kukamua asali mara tu baada ya kuvuna ni jambo la kimsingi kwani inapokaa sana huanza kuganda na hata ikapoteza thamani yake.

Anasema kuwa bado wakulima wengi nchini wanatumia mbinu za kiasili kama vile kitambaa au mikono kukamua asali.

Hata hivyo anashauri kuwa katika hatua ya kwanza kabla ya kukamua asali masega yanafaa kuhifadhiwa ndani ya ndoo na kufunikwa vizuri ili kuzuia bidhaa yenyewe isiweze kupata uchafu au kutangamana na unyevu.

Ndiposa uvumbuzi wa kifaa cha honey presser umekuja na manufaa makubwa kwani siku hizi mkulima anaweza kukamua hadi zaidi ya lita 30 ya asali kwa wakati mmoja.

Kifaa hiki ambacho kinaweza kununuliwa humu nchini ama kuagizwa kutoka kwenye mataifa ya nje kimeundwa kwa namna ambayo ni nyepesi kubebeka na ni rahisi kusafisha mara tu baada ya kutumika ikizingatiwa kuwa kimeundwa na stainless steel.

Kwa upande mwingine, mkulima John Njoroge kutoka eneo la Njoro Kaunti ya Nakuru anasema amefaidi pakubwa tangu anze kutumia kifaa cha honey presser kukamua asali kutoka katika masega.

Akiwa mshirika wa chama cha wakulima kutoka Njoro, anaungama kuwa pana mtambo mdogo ambao unaweza kuwawasidia wakulima wadogo wanaovuna asali kwa ajili ya matumizi ya nyumbani tu na mtambo mkubwa kwa matumizi ya viwandani.

Hatua za kukamua asali

Njoroge anasema kuwa katika hatua ya kwanza mara tu baada ya kuvuna asali , huyachukua masega yaliyokomaa na kuyaweka ndani ya kifaa cha honey presser.

John Njoroge akiunganisha mtambo wa presser ambao umebadilisha kabisa mchakato mzima wa kukamua asali. PICHA | RICHARD MAOSI

Anasema vifaa vinavyohitajika baada ya kuvuna ni mashine, ndoo ya lita 20, taulo safi ya kusunza mikono na maji ya uvuguvugu kusafisha sehemu ya nje ya honey presser.

“Ikumbukwe kuwa masega ni vyumba vidogo ambako nyuki hutengeneza na kutunzia asali,” asema.

Kisha mtambo wenyewe hufunikwa kwa kifuniko cha mashine, halafu huzungusha mkono wa chuma ambao hufanya kifuniko kushuka, na matokeo yake huwa ni kushindilia masega, ambayo hutoa asali.

Kisha asali hudondokea katika sehemu ya chini ambayo ina tundu ambapo ndoo huwa imewekwa.

Kuanzia hapo asali hupitizwa katika kichujio cha honey sieve ambapo makapi yote ya masega hutenganishwa na asali.

  • Tags

You can share this post!

UJASIRIAMALI: Kilimo Msitu kinavyohifadhi mazingira na...

Kesi zampa Uhuru muda zaidi Ikulu

T L